Wakulima wa pamba wameonya huenda zao hilo likatoweka iwapo serikali haitaacha kupanga bei yake isiyozingatia uhalisia na vigezo vya soko la dunia.

Wamesema uingiliaji huo wa bei unawaongezea umaskini, kwani katika msimu unaoelekea ukingoni kwa sasa, wamelazimika kuuza pamba yao kwa mkopo au chini ya bei elekezi ya Sh 1,200 kwa kilo.

Kwa mantiki hiyo, wanaitaka serikali iachane kabisa na upangaji wa bei ya zao hilo ili kuwawezesha wanunuzi kushindana kulingana na bei katika soko la dunia.

Wamesema bei huria itafaidisha wakulima, wanunuzi na serikali kwa ujumla.

Imeelezwa bei elekezi ya Sh 1,200 kwa kilo iliyotangazwa na serikali Mei 2, 2019, iligomewa na wanunuzi wa pamba kutokana na kushuka kwa bei ya zao hilo duniani.

Mdororo huo wa bei katika msimu wa mwaka 2018/2019, unatajwa kukolezwa na vikwazo vya kibiashara vilivyowekwa na Serikali ya Marekani dhidi ya China vikihusisha ushuru katika bidhaa nyingi.

Kwa mujibu wa taarifa, wanunuzi wengi wa zao hilo nchini walikuwa tayari kununua kwa bei isiyozidi Sh 1,100 kwa kilo moja, ili wakidhi uendeshaji wa kazi zao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika Mkoa wa Simiyu, wakulima wengi wa pamba wametaka upangaji wa bei elekezi usiozingatia uhalisia wa soko la dunia ufike ukomo.

“Tumechoka kupangiwa bei ya pamba. Watuache tuuze wenyewe kulingana na soko litakavyokuwa. Unauza unakopwa muda mrefu, hata ukiwa na mgonjwa unashindwa kumuuguza. Tumeanza kukata tamaa na kilimo cha pamba. Bei elekezi waifanye huko kwenye mabasi na daladala.

“Mbegu zenyewe ninakopa, dawa za kunyunyizia wadudu shambani ninakopa, shamba ninakodisha halafu ninauza pamba ninakopwa…aisee!

“Watu waliolima pamba wakipimwa akili leo hii, dunia itashangaa. Naamini wengi tutakuwa na kichaa kidogo, kwa sababu ya kukopwa pamba yetu,” amesema Maduhu Joseph.

Wamesema bei ya Sh 1,200 iliyotangazwa na serikali katika msimu unaoelekea tamati kwa sasa, si tu imewatia hasara, bali imewakatisha tamaa kuendelea na kilimo cha zao hilo.

Taarifa zinaonyesha kuwa asilimia 40 ya Watanzania wanajihusisha na kilimo cha pamba katika mikoa ya Magharibi na Ziwa Victoria.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Watanzania nusu milioni wameajiriwa kwenye shughuli zitokanazo na zao hilo la pamba.

Kutokana na hali hiyo, upo ulazima wa kuwekwa mikakati wezeshi msimu ujao ili kuzinufaisha pande zote tatu; mkulima, mnunuzi na serikali.

Kauli ya Serikali

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Dk. Fredrick Saganiko, amekiri mamlaka yake kuathirika na wakulima kukopwa pamba yao msimu huu kwa sababu hadi sasa hawajalipwa fedha za ushuru.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba, amekiri kuwa suala la bei ya pamba katika msimu unaomalizika limekuwa ni changamoto kubwa.

Hata hivyo amesema suala hilo limeipa serikali funzo kubwa na kubainisha kuwa kuanzia msimu ujao, bei ya pamba itapangwa baada ya kufanya marejeo ya bei katika masoko ya nje.

“Wakati tunatangaza bei elekezi ya Sh 1,200 bei katika soko la dunia ilikuwa juu kama senti 75 za dola. Tulitarajia ingepanda zaidi. Lakini, badala ya kupanda ikashuka tena chini senti 10 hivi. Hii ndiyo ilileta shida. Tumejifunza na msimu ujao makosa haya hayatajirudia,” amesema Waziri Mgumba.

Kilio

Wakulima wanasema kutokana na mdororo huo wa bei, wengi wao wamelazimika kuuza pamba kwa mkopo au chini ya Sh 1,000, kitendo wanachodai kimewaathiri kiuchumi na kisaikolojia.

“Mbona kule madukani, nguo, mitumba na hata viatu na miswaki serikali haiwapangii bei?” amehoji mkulima mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Samuel Mboje.

“Mwaka huu serikali iliamuru tuuze pamba kwa Sh 1,200 kwa kilo. Lakini wanunuzi wamegomea na anayeumia ni mkulima. Mambo gani haya?” amehoji Marco Simon na kuongeza:

“Wanunuzi walionekana kutaka kununua kwa Sh 1,100. Wakalazimishwa Sh 1,200… wasomi wanasema bei ya serikali ipo juu ya soko la dunia, matokeo yake wakulima ndio tumeteseka.”

Wameeleza mbali na kuuza kwa mkopo, hadi sasa bado kuna baadhi ya wakulima wana pamba ambayo hawajaiuza majumbani mwao.

Wakulima hao wanaamini kuwa soko huria litaondoa mtanziko wa bei, unaoasisi umasikini miongoni mwao.

“Unauza pamba unakopwa na haujui lini utalipwa. Unakaa hadi msimu mwingine wa kilimo  unafika haujalipwa, nini maana yake?

“Mimi nimeuza pamba mwezi Juni kilo zaidi ya 400, sijalipwa. Sitaki tena kulima pamba, ni bora nilime miwa,” amesema Samora Kija.

Bima ya mazao

Ester Mboje, Emmanuel Samwel, Salu Ngeleja, Kwandu Mduma na John Malugu, wanashauri kuanzishwe haraka bima ya mazao nchini, wakiamini itakuwa mkombozi dhidi yao.

Wamesema pamoja na kuwa mkombozi wakati bei ya mazao inaposhuka, bima hiyo ya mazao itawasaidia pia pale mazao yao yanapoangamizwa na wadudu, mvua na ukame kulingana na mabadiliko ya tabianchi.

“Serikali kama inataka kumuenzi kwa vitendo Mwalimu Julius Nyerere, iwajali wakulima wa pamba na wengine wote.

“Na hata mbegu zije mapema kabla ya kufunguliwa kwa msimu, maana hapa napo kuna shida kubwa. Maendeleo ya mkulima ni maendeleo ya Tanzania,” Moga Makoye, mkazi wa Maswa amesema.

Baadhi ya wanunuzi wa pamba waliokataa kutajwa majina yao, wamesema mkombozi wa mkulima wa zao hilo ni bei isiyoegemea upande mmoja.

“Sasa hivi tunahangaika kukopa fedha tulipe wakulima tuliowakopa pamba tangu Juni. Hatujui tutalipaje deni benki,” amesema mnunuzi mmoja wa pamba.

Mnunuzi mwingine wa zao hilo Kanda ya Ziwa, amesema: “Unaniambia ninunue kwa bei ya hasara, mimi nitakwenda kuuza wapi? Au unataka tu kunikomoa?”

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Dk. Fredrick Saganiko, amekiri mamlaka yake kuathirika na ukopwaji wa pamba msimu huu.

“Hatujalipwa fedha zetu (za ushuru),” Mkurugenzi Dk. Saganiko alikaririwa wakati alipoulizwa iwapo kuna athari zozote mamlaka yake imepata kutokana na kutolipwa kwa wakati wakulima hao.

Chimbuko

Pamba ilionekana kwa mara ya kwanza Tanganyika mwaka 1858, wakati John Speke alipokuwa katika safari yake ya kutoka Bagamoyo kwenda Ujiji, Kigoma.

Taarifa zilizopo zinasema Tanganyika (sasa Tanzania) ilianza kupanda zao hilo mwaka 1900. Na ilianza kuiuza nje ya nchi mwaka 1920.

Takwimu za uzalishaji zinaonyesha mwaka 1922, marobota 7,250 yalipatikana. Uzalishaji bora wa pamba ulianza Ukiriguru mwaka 1932.

Mwaka 1947 ukaanza Ilonga. Kazi iliyofanywa na vituo hivi viwili vya utafiti ni kubwa na ya kusifika.

Bila kutumia matokeo yao ya utafiti, pamba isingekuwapo nchini, hasa kutokana na wadudu waharibifu.

Pamoja na hayo, uzalishaji wa pamba kwa eneo bado uko chini ikilinganishwa na mataifa mengine yalimayo zao hilo, kutokana na wakulima wengi kupuuza kanuni za kilimo.

Bodi ya Pamba nchini (TCB), kupitia Mkurugenzi wake, Marco Mtunga, imefanikiwa kuongeza uzalishaji wa tija wa zao hilo katika misimu miwili  – mwaka 2017/2018 – 2018/2019.

Wachambuzi wa masuala ya pamba wanashauri serikali na wanasiasa kujiweka kando na upangaji wa bei isiyozingatia soko la dunia, katika msimu ujao.

“Mnunuzi asilazimishwe kununua pamba kwa bei ya juu ya soko la dunia.

Ukifanya hivyo, lazima utamuumiza tu mkulima na serikali lazima iingie kwenye mgogoro.

“Ukibana pumuzi ya mnunuzi, huyu mkulima ndiyo atakuwa taabani kabisa. Uwekwe utaratibu mzuri ili mkulima, serikali na mnunuzi wote wanufaike,” amesema Gerald Musa, mchambuzi wa mambo ya pamba.

314 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!