Benki zaagizwa kuboresha huduma kwa akina mama

DODOMA

Na Costantine Muganyizi

Serikali imezipongeza benki zenye utaratibu maalumu wa kuwahudumia wanawake nchini ikisema kufanya hivyo si tu kunawapa ahueni ya maisha akina mama nchini, bali pia una tija na mchango mkubwa katika ujenzi wa taifa.

Pia utaratibu huo ni biashara nzuri kwa taasisi hizo kwani wanawake ni nguzo imara kiuchumi iliyosahaulika, chanzo kikubwa cha mapato endelevu ambacho hadi sasa hakitumiki vizuri na ni sehemu muhimu ya soko yenye uwezo wa kuzipatia benki faida maridhawa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye makongamano ya kuwainua wanawake kifedha kwa kuwasaidia kuimarisha na kuboresha shughuli zao za kijasiriamali yanayoandaliwa na kuendeshwa na Benki ya Biashara Tanzania (TCB), viongozi waandamizi wa serikali wamezishauri benki zote kulizingatia suala la huduma za kibenki na kifedha kwa akina mama kwa mtazamo mpya na wa kipekee.

Ubunifu na TEHAMA

Wakisisitiza ubunifu na matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHEMA), wamesema benki zina nafasi kubwa na ya kipekee ya kusaidia kumkomboa kifedha na kumpa uhuru stahiki mwanamke ili aweze kuchangia kikamilifu maendeleo ya taifa.

Lengo mama la juhudi hizo zote ikiwa ni kuchangia kumwezesha na kumkwamua mwanamke kiuchumi ili ashiriki kikamilifu katika kuusimamia uchumi wa taifa na kuwa sehemu ya kukua kwake kama yalivyo matamanio ya Rais Samia Suluhu Hassan.

“Naziomba na kuzichagiza benki zote hapa nchini kuhakikisha zinaboresha na kuongeza huduma maalumu kwa ajili ya akina mama kwani kufanya hivyo ni kwa faida ya taifa zima kwa ujumla,” Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Wenye Ulemavu, Ummy Nderiananga, ameziasa taasisi hizo wakati anafunga kongamano la ufunguzi na la kwanza la wanawake la TCB lililofanyika mwanzoni mwa mwezi uliopita jijini Dodoma.

Ameipongeza benki hiyo kongwe inayomilikiwa na serikali ambayo kabla ya kubadilishwa jina Julai mwaka huu ilikuwa ikiitwa Benki ya TPB, kwa kuja na wazo la makongano hayo. 

Malengo ya Serikali

Ummy anasema utaratibu huo umekuja wakati muafaka kwani unaendana na malengo ya serikali wa kuhakikisha wanawake wanapewa nafasi stahiki kwenye ujenzi wa taifa. Anazitaka benki nyingine kuja na ubunifu wa aina hiyo ili zichangie kumkomboa mwanamke kimaendeleo.

“Sisi kama serikali tupo tayari kuja na sera wezeshi na kuweka mazingira rafiki kwa hilo kufanyika na tayari kwa kiasi kikubwa hayo yote yapo ndiyo maana TCB imeanzisha utaratibu wa Kongamano la Wanawake na Biashara,” Naibu Waziri Ummy anatanabainisha.

Mgeni rasmi wa kongamno hilo la kwanza alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka, aliyeipongeza TCB kwa uwekezaji huo ambao alisema faida zake ni pamoja na kuiimarisha benki kibiashara na kuifanya kuwa mshindani sokoni.

Mtaka anazishauri benki nyingine kuiiga TCB ili nazo zipate fursa ya kuongeza idadi ya wateja wa uhakika kwani nidhamu ya fedha kwa wanawake ni ya kipekee. 

Anasema ili zinufaike na wateja wanawake ni lazima kubuni suluhisho kuzingatia mahitaji maalumu ya wateja hao na hadhi zao kifedha, kiuchumi na kijamii.

Aidha, Mtaka anasema Jukwaa la Wanawake na Biashara la TCB linaendana na mpango wa Rais Samia wa kuongeza ushiriki wa akina mama katika kusimamia na kumiliki uchumi wa taifa.

“Kwa muktadha huo, benki na taasisi nyingine za fedha zina wajibu wa kushiriki kutekeleza ajenda hiyo ya serikali na TCB imeonyesha mfano kupitia uzinduzi wa Kongamano la Wanawake na Biashara,” anasema Mtaka.

Jukwaa la uwezeshaji

TCB inasema kupitia makongamo hayo imejipanga kuwa taasisi kinara ya kuwahudumia wanawake ili kuwakwamua kiuchumi kupitia suluhisho la kifedha kwa kuzingatia changamoto zao kama wajasiriamali.

Katika kutimiza azima hiyo, warsha hizo zitatumika kama jukwaa kuchochea maendeleo yao binafsi, familia, jamii na taifa. 

Na ili kuwa na matokeo chanya, makongamano kama hayo tayari yamefanyika Mbeya na midahalo mingine imepangwa kufanyika Zanzibar, Morogoro, Mwanza, Arusha na Dar es Salaam kuanzia mwezi huu.

Makongamano hayo yatawapa wanawake hasa wajasiriamali fursa ya kuifahamu vizuri TCB na huduma zake wezeshi huku wakibadilishana mawazo na uzoefu wa mambo mbalimbali. 

Wanawake na uchumi

Maofisa waandamizi wa TCB wamesema kimsingi lengo la jukwaa hilo si tu kuwawezesha wanawake wa Kitanzania kiuchumi, bali pia kuwaimarisha kifedha na kuwajenga kibiashara.

“Jukwaa hili litazingatia sana nafasi ya wanawake kuwa chachu ya uchumi na maendeleo na jinsi wanavyoweza kutumia fursa za kibiashara zinazotolewa na TCB kupitia huduma zake za kibenki na suluhisho mbalimbali za kifedha,” Ofisa Mtendaji Mkuu wa TCB, Sabasaba Moshingi, anasema.

Akizungumza wakati wa kongamano la Mbeya lililofanyika Septemba 24, 2021, Moshingi amekiri kuwa akina mama ni wateja wazuri linapokuja suala la kurejesha mikopo na kuweka akiba, kwa hiyo ni muhimu kwao kibiashara.

Anasema sasa hivi wanawake ni nusu ya wateja milioni moja wa benki hiyo ambayo iko vizuri na tayari kuwahudumia, kwani iko imara kifedha na ina wigo mpana wa huduma na mtandao mkubwa wa kuzifikisha huduma zake popote na kwa wakati.

“Tuna mtandao mpana wenye jumla ya matawi 82, makubwa yakiwa 46 na madogo 36, ambayo yametapakaa nchi nzima,” Moshingi amewaambia washiriki wa kongamano hilo.

Uwezo wa TCB

Kiongozi huyo alitumia takwimu za mafanikio ya TCB katika kipindi cha miaka kumi ya mabadiliko yake makubwa kuonyesha uwezo wa kifedha wa benki hiyo kuwahudumia na kuwawezesha akina mama.

Mapato yake yaliongezeka kutoka Sh bilioni 20 mwaka 2010 hadi Sh bilioni 155 mwaka jana, huku mizania ikipanuka kutoka Sh bilioni 136 hadi zaidi ya Sh trilioni 1.04.

Ukopeshaji wa TCB nao umeimarika zaidi huku akina mama wakikopeshwa zaidi ya Sh bilioni 120 hadi sasa.

Mgeni rasmi kwenye kongamano la Mbeya alikuwa Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, ambaye amesema TCB italisaidia sana taifa, hasa serikali, kuhakikisha hakuna mwanamke anayeachwa nyuma kiuchumi na kimaendeleo.

Kongamano hilo la pili lilifungwa na Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi, aliyesema wanawake ni jeshi kubwa kiuchumi linalohitaji kuhudumiwa kwa namna ya pekee.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya TCB, Sabasaba Moshingi