Mwaka 2012, biashara kati ya Tanzania na Qatar ilikuwa dola milioni 1.24 za Marekani, lakini miaka sita baadaye ilikuwa imeshamiri na kuongezeka takriban mara 31 hadi kufikia dola milioni 38.23 huku taifa hilo tajiri la Mashariki ya Kati likiwa ndilo lililonufaika zaidi.

Kwa mujibu wa takwimu zilizopatikana kutoka kwenye Ubalozi wa Tanzania jijini Doha, Qatar, ongezeko hilo ni sawa na ukuaji wa takriban asilimia 3,000 hadi kufika mwaka 2018.

Balozi wa Tanzania nchini humo, Fatma Rajab, aliliambia JAMHURI hivi karibuni kuwa biashara baina ya nchi hizi mbili itaongezeka zaidi siku za usoni kutokana na kuwepo mikakati mahususi ya kuimarisha mahusiano ya kibiashara kati ya Qatar na nchi za SADC.

Katika kufanikisha hilo, mwaka jana mabalozi wa nchi za SADC walioko Qatar waliunda umoja unaolenga kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kimaendeleo na taifa hilo ambalo ni moja kati ya wazalishaji wakubwa wa gesi asilia duniani.

Balozi Fatma anasema umoja huo unapanga kuwa unaandaa maonyesho maalumu yatakayoonyesha fursa za uwekezaji na biashara zilizoko Qatar na katika nchi za SADC.

“Lengo kuu la kuanzisha umoja huu ni kuzidi kuimarisha ushirikiano baina ya nchi za SADC na Qatar, hasa katika sekta ya madini, viwanda, kilimo, elimu, michezo, utalii, biashara na uwekezaji,” aliliambia JAMHURI.

“Bidhaa za chakula na matunda zinahitajika sana kwenye soko la Qatar kama nyama ya ng’ombe na mbuzi, maharage, mbaazi na kunde, korosho na matunda kama maparachichi, embe, nanasi na mengine mengi,” anaongeza.

Bidhaa ambazo sasa hivi Tanzania inauza kwa wingi Qatar ni pamoja na kahawa, maua, njegere, maharage na magogo. Kutoka Qatar, inaagiza kwa wingi hasa bidhaa za mafuta pamoja na chuma.

Takwimu zilizotoka ubalozini Doha zinaonyesha kuwa bidhaa zilizouzwa Qatar mwaka 2018 zilikuwa na thamani ya dola milioni 16.57 za Marekani ukiliganisha na dola 18,211.29 mwaka 2012. Hili lilikuwa ni ongezeko la dola milioni 16.55 ambalo ni sawa  na ukuaji wa zaidi ya asilimia 90,000.

Bidhaa zilizoagizwa kutoka Qatar mwaka 2018 zilikuwa na thamani ya dola milioni 21.66 za Marekani wakati thamani ya manunuzi mwaka 2012 ilikuwa dola milioni 1.22.

Wakati mauzo yalikuwa dola milioni 11.37 mwaka 2017, manunuzi kutoka Qatar yalikuwa dola milioni 11.96. Huu ndio mwaka ambao Tanzania ilianza kufanya vizuri kwenye uhusiano wake kibiashara na Qatar kwani kabla ya hapo mauzo yake yalikuwa chini sana.

Mwaka 2016, iliuza bidhaa zenye thamani ya dola milioni 1.11 tu wakati ikitumia dola milioni 19.47. Mauzo mwaka 2015, 2014 na 2013 yalikuwa na thamani ya dola milioni 2.51, dola 714,891.1 na dola milioni 1.29 mtawalia, huku manunuzi yakiwa dola milioni 16.48, dola milioni 6.32 na dola milioni 15.51 mtawalia.

778 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!