WASHINGTON, MAREKANI

Ikulu ya Marekani imependekeza bajeti ya dola trilioni 6 kwa ajili ya mwaka wa fedha 2022. Wakati mapendekezo hayo ya bajeti yakitolewa, Rais Joe Biden amejiandaa kutoa maelezo ya mipango yake ya kifedha katika kipindi cha kati.

Atatoa maelezo hayo wakati atakapolihutubia Baraza la Congress.

Bajeti hiyo inalenga kuweka matumizi endelevu katika kipindi cha zaidi ya nusu karne, katika mipango inayolenga kuwanufaisha watu wa kipato cha kati, ikikadiria nakisi ya zaidi ya dola trilioni moja katika kipindi cha muongo mmoja ujao.

Bajeti hiyo iliyopendekezwa na Ikulu ni kama chambo cha Rais Biden kwa Baraza la Congress, akilishawishi likubaliane na sera zake.

Hata hivyo, inatarajiwa kuwa bajeti hiyo itafanyiwa marekebish kadhaa kabla haijapitishwa kuwa sheria.

Wajumbe wa Chama cha upinzani cha Republican ndani ya Congress tayari wameshatoa tahadhari kuhusiana na bajeti hiyo na nakisi yake, mambo ambayo walikuwa hawayatolei maoni katika kipindi cha Rais Donald Trump.

Pamoja na mambo mengine, wajumbe hao wamehoji mipango ya matumizi katika maeneo yanayolenga kukuza uchumi.

Bajeti hiyo iliyowasilishwa Ijumaa iliyopita imepanga kuongeza matumizi hadi kufikia zaidi ya dola trilioni nane ifikapo mwaka 2031.

Tayari Rais Biden ameshatoa mapendekezo makubwa mawili – mpango wa kuwapatia Wamarekani ajira na mpango wa kuzisaidia familia za Wamarekani – kama njia ya kuilinda jamii nchini humo.

Bajeti hiyo imewasilishwa wakati makundi mawili kwenye mabunge yakibishana kuhusiana na mpango mkubwa wa Rais Biden unaolenga kufufua miundombinu na kuongeza ajira nchini humo.

Wajumbe wa Baraza la Seneti wa Chama cha Republican walitoa bajeti mbadala ya miundombinu ya dola bilioni 928, ambayo ni pungufu kwa dola trilioni moja ukilinganisha na mapendekezo waliyoyatoa wakati walipokutana na Rais Biden walipokutana Ikulu kwenye majadiliano ya awali.

Awali, Rais Biden alipendekeza bajeti ya dola trilioni 2.25 kwa ajili ya ufufuaji wa miundombinu nchini humo na kujikita kwenye matumizi ya nishari jadidifu.

Mapendekezo ya wajumbe wa Republican yanalenga kufanya uwekezaji mkubwa kwenye barabara kuu, madaraja na miradi mikubwa (dola bilioni 506); barabara nyingine (dola bilioni 98; dola bilioni 46 kwa ajili ya reli za mizigo na abiria; dola bilioni 21 kwa ajili ya usalama; dola bilioni 22 kwa ajili ya bandari ya njia za majini; dola bilioni 56 kwa ajili ya viwanja vya ndege; dola bilioni 22 kwa ajili ya utunzaji wa maji; dola bilioni 72 kwa miundombinu ya maji na dola bilioni 65 kwa miundombinu ya mkongo wa mawasiliano).


Rais wa Marekani, Joe Biden, akizungumza na waandishi wa habari akiwa pamoja na Makamu wake, Kamala Harris.
Please follow and like us:
Pin Share