OR-TAMISEMI

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Deogratius Ndejembi amesema Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba ameshaelekeza Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kupatiwa Sh. Bilioni 30 ili iweze kutatua changamoto ya barabara kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Mhe.Ndejembi ametoa kauli hiyo leo bungeni jijini Dodoma wakati akichangia hoja ya dharura iliyowasilishwa na Mbunge wa Rorya mkoani Mara, Mhe Jafar Chege kuhusu ubovu wa barabara kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Naibu Waziri Ndejembi amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua changamoto ya kuharibika kwa barabara nchini kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyeesha na hatua za haraka za kukabiliana na changamoto hiyo zimeshaanza kuchukuliwa.

“ Niwaondoe hofu Wabunge wote kwamba changamoto hii inakwenda kutatuliwa kwa sababu tayari fedha zimeshaingia TARURA. Mhe Waziri wa Fedha baada ya kukaa na Mhe Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI ile Bilioni 350 iliyoletwa TARURA kama nyongeza kutoka kwenye ile Bilioni 810 iliyopitishwa na Bunge kama bajeti ya TARURA ianze kutumika na kazi hizo zitangazwe ili changamoto hii iishe mara moja.:

“ Lakini kipekee nimshukuru Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiongeze nguvu TARURA ambapo ameiongezea bajeti kutoka Sh Bilioni 226 aliyoikuta hadi Sh Bilioni 810. Haya ni mapenzi makubwa ameyaonesha kwa watanzania katika kuhakikisha anakaboresha miundombinu ya barabara kwenye maeneo mbalimbali nchini,” amesema Mhe Ndejembi.

By Jamhuri