Na Nizar K. Visram

Ethiopia ni moja ya nchi kubwa katika Bara la Afrika, ikiwa na wakaazi takriban milioni 115 na makabila zaidi ya 80.

Aprili 2018, Abiy Ahmed, aliapishwa kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo na mwaka uliofuata akatunukiwa Nishani ya Amani ya Nobel kutokana na jitihada zake za kutatua mgogoro kati ya nchi yake na Eritrea.

Abiy alirithi Serikali ya Ethiopia iliyokuwa ikiongozwa na watu wa Jimbo la Tigray na Chama chao cha TPLF. Huu ni mfumo wa majimbo, kila jimbo likiwa na mamlaka ya utawala wake. 

Watu wa kabila la Watigray ndio walikuwa wakiongoza Ethiopia tangu mwaka 1991 walipouangusha utawala wa Mengistu Haile Mariam aliyekimbilia Zimbabwe.  

Alipoingia madarakani, Abiy akaamua kuvunja nguvu za Watigray kushika hatamu ya nchi. Akavunja chama tawala na kuunda Chama kipya cha Prosperity Party ili kuunganisha majimbo yote.

TPLF ikakataa kuungana na chama kipya. Wakajitoa katika serikali ya Abiy na kurudi jimboni Tigray ambako chama kikashika hatamu ya serikali ya jimbo. Wakategemea kuwa katika uchaguzi wa kitaifa watamuangusha Abiy.

Uchaguzi wenyewe ulipangwa kufanyika Agosti 2020, lakini Abiy akauahirisha kwa sababu ya Uviko-19. TPLF ikaamua kuendelea na uchaguzi wake katika Jimbo la Tigray. Abiy akakataa kuutambua uchaguzi huo na akaamuru majeshi yake kuidhibiti Tigray. 

Novemba mwaka jana Abiy Ahmed akatuma majeshi yake katika Jimbo la Tigray kwa lengo la kuupindua utawala wa TPLF. Mapigano makali yakazuka baina ya majeshi ya Ethiopia (EDF) na TPLF na mamilioni ya watu wakalazimika kuyakimbia makazi yao. 

Kufikia Juni mwaka huu, TPLF ilidai imechukua sehemu kubwa ya Tigray na ikatangaza kwamba inalenga  kuyachukua maeneo jirani ya Amhara na Afar. Yaani TPLF ikazidi kusonga mbele.

Abiy akazuia misaada ya kimataifa kuingia Tigray akidai kuwa mashirika ya misaada yanawasaidia wapiganaji wa TPLF. Alidiriki hata kuwafukuza watoa misaada na wengine akawakamata. Asilimia 90 ya raia wa Tigray (milioni 5.2) wakakosa chakula.   

Miezi miwili baada ya kuanza kwa vita, zaidi ya Watigray 56,000 wakakimbilia Sudan. Majeshi ya Ethiopia, wakisaidiwa na majeshi ya Eritrea, walifunga njia ya Sudan na Watigray wakakosa pa kukimbilia.

Tigray, jimbo lenye wakazi zaidi ya milioni saba likakosa mawasiliano na nchi za nje. Simu ikakatwa na wanahabari walizuiwa kuingia jimboni na walio ndani wakazuiwa kuwasiliana na nje.  

Wakati huo huo, Ethiopia imekuwa soko kubwa la silaha na hii inazidi kuchochea vita. Katika miaka mitano iliyopita silaha zenye thamani ya dola milioni 92 zimeingia nchini humo. 

Russia imeuza silaha za dola milioni 69, Marekani milioni 10, Israel milioni 4, China milioni 4, Ufaransa milioni 2 na Ujerumani milioni 2. 

Baada ya vita kuendelea kwa mwaka mmoja, Watigray wakaungwa mkono na mikoa ya jirani, hasa ile ya Amhara na Afar. Ndipo TPLF ikapata nguvu na kuanza kusonga mbele kuelekea Addis Ababa, mji mkuu wa Ethiopia, na Makao Makuu ya Umoja wa Afrika (AU).  

Baada ya kuona vita inaendelea zaidi ya mwaka mmoja na TPLF inazidi kupata nguvu, AU ikaamua kutumia diplomasia kuinusuru nchi isimeguke. Hali hii itaiathiri hata AU ambayo inategemea amani nchini Ethiopia, kwani bila amani italazimika kuhamisha makao yake!

AU ikateua jopo la marais wastaafu watatu kusuluhisha. Nao ni Joaquim Chissano wa Msumbiji, Bi Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia na Kgalema Motlanthe wa Afrika Kusini. Hata hivyo baada ya jitihada zao za mwezi mzima walishindwa kuleta matokeo yoyote.

Ndipo Agosti mwaka huu, AU ikamteua rais mstaafu wa Nigeria, Olesegun Obasanjo. Yeye alikutana mara kadhaa na viongozi wa serikali kuu na wa TPLF, kisha akasema ana matumaini kuwa atafanikiwa kuzifanya pande mbili zikae pamoja na kuzungumza.

Obasanjo alisema ugomvi huu hauwezi kutatuliwa kwa njia ya vita, kwani hata upande mmoja ukishika madaraka kwa mtutu wa bunduki, amani ya kudumu haitapatikana nchini. Ndipo akazitaka pande zote ziache mapigano na kuanza mazungmzo.

Abiy akaweka masharti ya kuzungumza na TPLF. Aliwataka kwanza waache kuyashambulia majeshi yake, kisha watoke katika majimbo ya Amhara na Afar waliyoyateka. Tatu, aliwataka waitambue serikali yake. 

Kwa upande mwingine, TPLF walikataa kutoka maeneo hayo. Badala yake waliukamata mji wa Kemise ulio kilomita 325 kutoka Addis Ababa. Wakasema nia yao ni kuuteka mji mkuu.

TPLF walisema wataanza kuzungumza pale tu majeshi ya Abiy yatakapoacha kulizingira Jimbo la Tigray na kuruhusu watu wapokee misaada kutoka UN na mashirika mengine.

Wakati huo huo Mamlaka ya Maendeleo katika Pembe ya Afrika (Intergovernmental Authority on Development – IGAD), imejihusisha baada ya kuhisi kuwa vita ya Ethiopia inaweza ikaathiri vibaya nchi jirani. Ndipo Rais Uhuru Kenyatta akawasili ghafla jijini Addis Ababa na kuonana na Abiy.

Katika mapigano haya inasemekana pande zote mbili zimewashambulia raia wasio na hatia wala silaha. Kama ni kweli basi huu ni uhalifu wa sheria ya kimataifa. Tayari ripoti za UN na tume ya haki za binadamu nchini Ethiopia zimesema kuna ushahidi kuwa katika Jimbo la Tigray yamekuwako mauaji ya halaiki, utesaji na ubakaji.

Michelle Bachelet, mkuu wa tume ya UN kuhusu haki za binadamu, amesema pande zote mbili zimehalifu sheria ya kimataifa. 

Uchunguzi mmoja, kwa mfano, umedhihirisha jinsi mauaji ya raia zaidi ya 100 katika mji wa Axum (Tigray) yalivyofanywa na majeshi ya Eritrea Novemba 28, mwaka jana. Majeshi hayo yalimkamata mzee wa miaka 70 na watoto wake wawili. Wakawalaza chini kisha wakawapiga risasi kichwani. 

Na Novemba 9 na10, ripoti inasema, kijana wa Kitigray aitwae Samri aliwaua raia zaidi ya 200 wa kabila la Amhara katika Mai Kadra (Tigray magharibi) akisaidiwa na polisi, wanamgambo na wapiganaji wa TPLF.

Haya yameorodheshwa katika ripoti yenye kurasa 156 iliyotokana na watu 269 kuhojiwa, wakiwa wahanga na mashahidi. Wanawake 30 walieleza jinsi walivyobakwa. 

Mmoja anaeleza jinsi alivyochukuliwa na wanajeshi wa Eritrea, wakamzuia kwa muda wa siku 11 huku akibakwa na askari 23. Wakamtelekeza akiwa mahututi na akaokotwa na kulazwa hospitalini akitibiwa kwa miezi minne.

Eritrea ilikataa kukutana na wachunguzi, na waziri wake wa mambo ya nje alikataa kuzungumza alipohojiwa na waandishi.

Kwa upande wa pili, Abiy alisema anaikubali ripoti ingawa ‘ina makosa makubwa’. Akaongeza kuwa ni vizuri ikakumbukwa kuwa ripoti hailaumu serikali yake kama serikali. 

Hata hivyo, akaahidi kuwa atateua kikosi kazi kikiwa na raia na wanajeshi ili kuchunguza shutuma. Abiy akasema tayari kuna wanajeshi wachache ambao wamefikishwa mahakamani kwa shutuma za mauaji na ubakaji.

Nayo ofisi ya mambo ya nje ya Tigray imesema ripoti ina matatizo ya kimsingi, kwa sababu wachunguzi hawakufanya jitihada ya kuonana na utawala wa Tigray. Pia ofisi ilisema uchunguzi ulifanywa na tume ya haki za binadamu iliyoteuliwa na serikali ya Abiy, kwa hivyo haingewezekana wao kutopendelea. Lakini ofisi ilipoulizwa kuhusu mifano ya uhalifu wa Tigray hakukuwa na majibu.

Habari za hivi karibuni zinasema Waziri Mkuu Abiy Ahmed, mshindi wa tuzo ya kimataifa ya amani, sasa anakusudia kuongoza vita yeye binafsi.

Ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa Twitter: “Nitakuwa ninaongoza majeshi nikiwa katika medani ya vita. Wale wana wa Ethiopia wanaotaka kuilinda nchi yao tukutane huko.”

Amesema haya wakati majeshi ya upinzani yanayoongozwa na TPLF yanasonga mbele kuelekea Addis Ababa, wakidai tayari wanaudhibiti mji wa Shewa Robit ulio kilometa 220 kutoka mji mkuu. 

Wengine wanafananisha hali hii na ya Afghanistan ilipotekwa na wapiganaji wa Taliban, wakiyatimua majeshi ya Marekani. 

Abbas Haji Gnamo, mchambuzi wa masuala ya Ethiopia kutoka Chuo Kikuu cha Toronto anasema bado kuna wanaotumaini kuwa pande mbili zinaweza kusuluhishwa. 

“Abiy hawezi kushinda vita hii. Majeshi yake hayana uwezo huo, naye kuingia katika uwanja wa vita hakutasaidia chochote. Mazungumzo ni njia pekee,” anaongeza. 

[email protected]

By Jamhuri