Hali ya soka nchini hususan mwenendo wa michezo ya ligi kuu si ya kuridhisha. Kumekuwa na lawama kutoka kwa wadau wa soka zinazoelekezwa kwa waamuzi wa mechi mbalimbali, lakini kwa upande mwingine, vilevile kumekuwa na malalamiko dhidi ya Bodi ya Ligi Tanzania Bara.

Wakati waamuzi wakilalamikiwa  kutokuwa imara na makini katika baadhi ya mechi wanazosimamia, Bodi ya Ligi imekuwa ikishutumiwa kutokana na ‘ubutu’ wake katika kupanga ratiba ya ligi hiyo kuu.

Wiki iliyopita pale mkoani Morogoro kulikuwa na mtanange mkali kati ya Mtibwa Sugar na Yanga katika Uwanja wa Soka wa Jamhuri. Katika mechi hiyo goli lililofungwa na mshambuliaji wa Yanga, Hamis Tambwe, lilikataliwa na mwamuzi wa pembeni baada ya mwamuzi huyo kunyoosha kibendera akiashiria kuwa mshambuliaji huyo alizidi (offside), hali iliyozua malalamiko kutoka kwa baadhi ya wadau wa soka nchini.

Ukitazama kwa umakini utabaini kuwa malalamiko ya aina hiyo yamekuwa yakichomoza kutoka kwa  timu nyingi za ligi kuu.

Lakini wakati hayo yakihusu udhaifu wa waamuzi, malalamiko mengine yamekuwa yakihusu Bodi ya Ligi kwamba timu za ligi kuu zimecheza michezo zaidi ya 30 isipokuwa timu ya Simba SC.

Smba imekwisha kucheza mechi 23, tofauti na timu nyingine zilizocheza mechi zaidi ya 30. Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wadau wa soka nchini wamekuwa wakiitazama Bodi ya Ligi kwa jicho la wasiwasi, kwa madai kuwa imepanga ratiba inayoipendelea Simba na hata kusababisha kupanga matokeo ya mechi hizo za viporo ili hatimaye timu hiyo itwae ubingwa.

Bodi ya Ligi inayoongozwa na Boniface Wambura nayo imekuwa ikijitetea kwamba sababu ya kupanga ratiba ya namna hiyo imechangiwa na Simba kushiriki michuano ya kimataifa kwa mujibu wa ratiba ya CAF kuhusu michuano ya Klabu Bingwa Afrika, sababu ambayo hata hivyo bado inatajwa kutokujitosheleza kwa baadhi ya wadau wa soka wanaoamini kuwa idadi hiyo ya viporo imezidi kwa kulinganisha na timu za mataifa mengine zinazoshiriki michuano hiyo ya barani Afrika kama ilivyokuwa kwa Simba.

Kwa mfano, nchini Afrika Kusini licha ya timu ya Mamelodi Sundowns kushiriki katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika, wamecheza jumla ya mechi 26 na kubakisha kiporo kimoja mkononi, maana yake ni kwamba Chama cha Soka Afrika Kusini (SAFA) kinaendesha ligi kwa namna ambayo haiwezi kuleta manung’uniko kwa baadhi ya mashabiki na wadau wa soka nchini humo.

Hiyo ni kwa upande wa Ligi ya Afrika Kusini inayojumuisha timu 16. Kwa upande wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Bodi ya Ligi nchini humo haina tofauti kwa kiasi kikubwa na Tanzania. Huko baadhi ya timu zimecheza mechi  30, timu za Muungano na Nyuki, wakati baadhi ya timu zimecheza mechi 24 hadi  25, lakini TP Mazembe imecheza mechi 25, hivyo ni miongoni mwa timu zilizosalia na mechi nyingi mkononi.

Kule Morocco licha ya Wydad Casablanca kushiriki mashindano ya Klabu Bingwa Afrika, wamecheza mechi 24 katika ligi yao inayojumuisha timu 16. Wydad Casablanca haina kiporo chochote mkononi, kwa hiyo chama cha soka nchini Morocco kimejitahidi katika kupanga kwa umakini ratiba ya ligi kuu.

Kule Tunisia msimamo wa ligi umekaa hivi, licha ya timu ya Esperance de Tunis kushiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika, imecheza michezo 19 sawa na timu zingine 14 zinazoshiriki ligi kuu ya nchini humo.

Ratiba iliyopo hapa nchini, kwa sasa Simba inalazimika kucheza mechi kila baada ya siku tatu ili kwenda sambamba na timu zingine za ligi kuu Tanzania Bara. Leo Simba itakuwa katika dimba la CCM Kirumba jijini Mwanza kupepetana na timu ya Alliance.

1181 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!