Leo ni leo katika historia ya mashindano ya Klabu Bingwa barani Ulaya (UEFA Champions League), ambapo hakuna historia isipokuwa rekodi maridhawa, wakati Tottenham Hotspurs ya Uingereza ikipambana na Ajax ya Uholanzi, huku kesho mabingwa wenye historia zinazofanana wakimenyama katika dimba la Camp Nou.

Ajax imechukua taji hilo mara tatu mfululizo (back to back) kuanzia mwaka 1971 hadi 1973. Imechukua taji hilo kwa mara ya mwisho mwaka 1995, huku ikiwa imefika fainali mara sita.

Wakati hiyo ikiwa ni rekodi ya Ajax, wapinzani wao Tottenham Hotspurs, kwenye kumbukumbu rasmi na vitabu vya UEFA, hakuna rekodi yoyote inayoihusu Tottenham, kwa maana ya kufika fainali ya michuano hiyo yenye mvuto barani Ulaya, nyuma ya Kombe la Dunia.

Kumbukumbu za UEFA Champions League zinamtaja mshambuliaji wa Tottenham, Harry Kane, kama mfungaji bora wa wakati wote kutoka kwa wakali hao wa Jiji la London akiwa ameifungia klabu hiyo jumla ya magoli 14, akifuatiwa na Son Heung-Min, magoli 9. Huku wakali wengine wakiwa ni Peter Crouch (7), Allan Smith (6), Jones (4).

Rekodi nyingine inayoihusu Klabu ya Tottenham ni ile ya wachezaji waliocheza mechi nyingi katika michuano ya UEFA, inamtaja Son Heung-Min mechi 24, Moussa Sissoko mechi 22, Christian Eriksen mechi 21, golikipa Hugo Lloris mechi 21 na Devies mechi 20.

Katika kutafuta hatua ya kusonga hatua ya fainali, timu zote zimekuwa na takwimu za kuogopesha hali inayosababisha wapinzani wote kuogopana, hiyo inaonyesha michezo yote miwili itakuwa ya tahadhari kwa timu zote.

Ajax, hadi kufikia hatua ya nusu fainali imekuwa na takwimu za kibabe kama ifuatavyo; imefunga jumla ya magoli 19, katika michuano hii ya UEFA, kinara wa magoli katika timu hii ni Dusan Tadic ambaye hadi sasa amepachika magoli 6 katika mechi 10.

Magoli matano akiyafunga kwa mguu wake wa kushoto na goli moja mguu wa kulia, huku akiwa amepiga mashuti 17 langoni, takwimu zinaonyesha ametoa pasi nne za magoli.

Ajax wanaonekana kuwa na uchu wa magoli kwani wamepiga mashuti 159 katika lango la timu pinzani walizokutana nazo kuanzia hatua za makundi, huku wakifunga magoli 19.

Ajax ni wapambanaji hadi kufikia hatua ya nusu fainali wamepoteza mechi moja, dhidi ya Real Madrid, huku wakitoka sare nne, na hawakupoteza mchezo wowote katika hatua ya makundi huku kiungo wao Hakim Ziyech akipiga pasi nne za mabao.

Tottenham, Vijana wa Kocha Muargentina, Mauricio Pochetino, wana takwimu za kutisha hadi kufika katika hatua hii ya nusu fainali. Hadi kufika hatua ya nusu fainali wamekwisha kufunga magoli 17, huku wakipiga mashuti 147 katika lango la timu pinzani walizokutana nazo.

Majogoo wa Merseyside, Liverpool watakuwa na kibarua kigumu mbele ya FC Barcelona, katika mchezo wa kwanza utakaopigwa katika dimba la Camp Nou, mashabiki watatarajia kuona endapo Barcelona wenye rekodi lukuki wataendeleza ubabe wao mbele ya majogoo wa Liverpool.

Barcelona imechukua ubingwa wa UEFA mara tano kama ilivyo kwa Liverpool na Bayern Munich. Rekodi katika mashindano ya msimu huu zinawabeba Barcelona, maana hawajapoteza mchezo wowote.

Lionel Messi anaongoza kwa idadi ya magoli msimu huu akiwa amefunga jumla ya magoli 10, kabla ya mechi ya leo. Amepiga mashuti 44 golini, amecheza mechi nane, dakika 657, amepiga jumla ya pasi 526, kati ya hizo 441 ziliwafikia walengwa na 85 zilipokwa na timu pinzani.

Messi ana wastani wa mechi moja, magoli 1.3, mguu wake wa kushoto umefunga magoli 7 huku ule wa kulia ukiwa umefunga magoli 3, nidhamu yake haina maswali maana hajaonyeshwa kadi ya njano wala nyekundu.

Barcelona wamepiga pasi 7,169, wakati pasi zilizokamilika ni jumla ya pasi 6,434 sawa na asilimia 83.4, huku pasi hizo zikiwa sawa na umiliki wa asilimia 60, wamepiga krosi 117. Anayeongoza kwa kupiga pasi nyingi Barcelona ni Sergio Busquets, ambaye amepiga pasi 834.

Liverpool, vijana wa Kocha Mjerumani, Jurgen Klop, kesho watakuwa na kibarua kigumu watakapokaribishwa na Barcelona lakini kinachowapa matumaini makubwa na takwimu kali kimchezo.

Baada ya Barcelona na Ajax kufunga magoli mengi Liverpool nayo haiko mbali, maana wamefunga magoli 18 hadi wanaingia katika hatua hii ya nusu fainali.

Nyota wao Mohammed Salah ndiye kinara wa kupachika magoli baada ya kufunga magoli 4, sambamba na washambuliaji pacha Roberto Firmino na Sadio Mane. Washambuliaji hao wametengeneza muunganiko ambao unatisha.

Please follow and like us:
Pin Share