Serikali kupitia Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu imeanza kukabiliana na changamoto ya upungufu wa kina cha maji cha mto Ruvu na mto Wami kwa kuanza kutoa vibari kwa mamlaka za maji kuchimba visima vitakavyosadia kupunguza adha ya maji kwa wananchi wa maeneo ya Dar es Ssalaam, Dodoma na Morogoro.

Akizungumza jana katika kikao kilichowakutanisha wadau na watumia maji, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu Elibarik Mmassy alisema Bodi hiyo imeamua kutoa vibari vya uchimbaji wa visima katika maeneo yaliyoanishwa ili kuwapunguzia adha ya upatikanaji wa maji kwa wananchi katika kipindi hiki cha ukame.

“Tumeshatoa taarifa kwa mamlaka na wadau mbalimbali wa maji maeneo ambayo wanaweza kuchimba visima ambavyo vinaweza kuwa mbadala kwa maeneo ambayo maji hayawezi kufika, ingawa sehemu nyingine maji yanaweza kuwa ya chumvi kidogo lakini tumeona ni bora watu wapate maji na watafute kidogo ya kunywa.”amesema Mmassy Mkurugenzi Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu.

Amesema Bodi ya maji Bonde la Wami la Wami Ruvu limeanza kuchua hatua mbalimbali za muda mfupi ikiwemo kufanya ukaguzi kwenye vyanzo vya maji ili kuhakikisha kiwango cha maji kilichopo kiwezi kukidhi mahitaji ya watumia maji wa majumbani.

“Zoezi la kulinda vyanzo vya maji tunaendelea nalo na mpaka sasa hakuna mtu yeyote aliyechepusha maji na kuzuiya maji kutoka kwenye vyanzo vyetu vya maji, tumeendelea na doria kwenye milima ya uluguru na maeneo yote ya vyanzo vya maji.” amesema Mmassy.

Amesema mwaka huu haukuwa na mvua toshelevu na kufanya kupungua kwa kina cha maji kwenye mito mingi ambapo mpaka sasa maji yaliyopo kwenye mto Ruvu ni lita 2580 huku mililita 1870 zikiwa kwenye mto Wami ambapo mahitaji ya maji ya kiujumla ni lita 9000 na mahitaji ya majumbani ni lita 5800. .

“Miaka ya kawaida kwa tarehe kama ya leo kunakuwa na ujazo wa mililita 14,000 kwenye mto lakini kutokana na mabadiliko ya tabianchi, na kutokuwepo na mvua za kutosha za masika na vuli, na ukame katika mwezi huu wa Oktoba hali imekuwa tofauti, na hali kama hii hutokea mwezi wa Novemba mwishoni wakati mvua za masika zinaanza kunyesha na kufanya kutokuwa na shida ya maji” amesema Mkurugenzi huyo

Aidha amesema Bodi ya maji Bonde la Wami Ruvu katika kulinda vyanzo vya maji imelazimika kusitisha vibali 12 vya watumiaji maji ili kupunguza matumizi ya maji na kukabiliana na hali ya ukame iliyopo inayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.

Hivyo aliwataka wadau wa maji kuzingatia vipaumbele vya utoaji wa vibali ikiwemo utunzaji wa mazingira, matumizi ya majumbani na kulingana na upatikanaji maji ambapo alisema kupunguza matumizi ya maji kutasaidia kupambana na upungufu wa maji ikiwemo kuacha shughuli za kumwagilia ikiwemo maua majumbani.

Amesema katika kikao hicho wamejadili mambo mengi yenye nia chanya ya kujenga na kuhifadhi vyanzo vya maji kwenye bonde hilo kwa njia ya kushirikiana kwenye kutunza na uwekaji wa mipaka kwenye vyanzo vya maji na kuwekeza kwenye miundombinu ya kutunza maji kipindi cha masika.

Amesema kwa wadau wa wafugaji nao waliendelea kuwapa taarifa huku wakijenga mabirika 6 yanayogharimu kiasi cha sh mil 60 na matano yakiwa kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kama mfano kwa wafugaji kuweza kujenga wenyewe hasa kwa wale wenye ng’ombe wengi kuanzia 1000 na kuendelea anauwezo wa kujenga kwa ajili ya kupata maji na malisho.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya maji Bonde la Wami Ruvu Hafsa Mtasiwa amesema ifaamike kuwa hali hiyo kwenye mzunguko wa maji huwa inatokea na ndio maana Rais Samia Suluhu Hassan aliwekeza kujenga bwawa la Kidunda ambalo linakaribia kufanya kazi ambapo Waziri wa maji Juma Aweso ametoa kipaumbele cha ujenzi wa mabwawa madogo madogo matano kwenye safu za milima ya Uluguru yatakayobea kiasi cha maji ya mita za ujazo kuanzia mililita 19 mpaka 21 ili kupunguza changamoto iliyokuwepo.

Nae Mkurugenzi wa Sheria Wizara ya maji Simon Nkanyemka amewataka wadau na watumia maji kutunza vyanzo vya maji pamoja na kufuta sheria za rasilimali za maji za mwaka 2009 na ya mazingira ya mwaka 2004 ambazo haziruhusu shughuli zozote za kibinadamu kufanyika ndani ya mita 60 ya chanzo cha maji.

By Jamhuri