Rais wa Iran Ebrahim Raisi, Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir-Abdollahian na wengine kadhaa wamethibitishwa kufariki dunia katika ajali ya helikopta iliyotokea Jumapili kaskazini-Magharibi mwa Iran.

Helikopta hiyo ilipatikana kaskazini magharibi kwenye mteremko wa kilima katika eneo la Varzaghan, karibu na mpaka wa Azerbaijan Mashariki.

Mapema saa saba hadi nane zilizopita iliripotiwa kuwa ndege hiyo imepata ajali na wataalamu walianza kuisaka mara moja huku hali mbaya ya hewa ikitajwa kama chanzo cha ajali hiyo.

Ebrahim Raisi ameingia madarakani kuiongoza Iran mwaka 2021 na hiyo ni baada ya kugombea kiti cha urais mwaka 2017 na kushindwa.

Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 63 kwa muda mrefu amekuwa akichukuliwa kama mrithi wa asili wa Kiongozi Mkuu Ayatollah Ali Khamenei, mamlaka ya juu zaidi nchini Iran.

Rais Ebrahim atakumbukwa zaidi kutokana na msimamo mkali na mwenye uhusiano wa kina katika mahakama na wasomi wa kidini.