Muswada huo wa Sheria ya Fedha wenye utata umepitia Kamati ya Bunge zima , ambapo wabunge walikuwa wakipiga kura ya marekebisho ya muswada huo, sasa unasomwa kwa mara ya tatu.

Hii ni baada ya wabunge 195 kupiga kura kupitisha muswada huo huku 106 wakipiga kura kukataa sheria iliyopendekezwa.

Wakati hayo yakijiri, makabiliano makali yamezuka katikati ya mji wa Nairobi baada ya Polisi kuwatawanya waandamanaji wakipinga muswada wa fedha wa 2024.

Umati wa waandamanaji ulikuwa umekusanyika katika barabara mbalimbali kupinga Muswada wa Fedha wa 2024 wakati makabiliano yalipozuka.

Polisi waliwarushia vitoa machozi waandamanaji waliokuwa wamejihami kwa maji na simu za rununu ili kueleza msimamo wao dhidi ya muswada huo.

Umati huo ulianza kukusanyika mapema saa moja asubuhi karibu na Hifadhi ya Kitaifa ya Kenya.