Idadi ya vifo vilivyotokana na shambulizi la jana Jumapili katika jimbo la Dagestan kusini mwa Urusi imeongezeka na kufikia 19.

Kulingana na Kamati ya uchunguzi mapema leo, washambuliaji watano pia waliuawa kwenye shambulizi hilo.

Shirika la habari la AFP limeinukuu kamati hiyo, iliyosema waliouawa ni maafisa wa usalama 15 na raia wanne, miongoni mwao ni mchungaji wa Kanisa la Orthodox.

Shambulizi hili linafanywa miezi mitatu tu baada ya kundi la wanamgambo linalojiita Dola la Kiislamu kuwaua zaidi ya watu 140 waliokuwa katika ukumbi wa kuandaa tamasha mjini Moscow.

Msemaji wa Ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov amepuuzilia mbali kitisho cha kurejea kwa mashambulizi kwenye eneo la Kaskazini, alipoulizwa kuhusiana na wasiwasi huo.