*Ni za wale waliokiri makosa, wakalipa faini kwa DPP, sasa yadaiwa fedha hazikwenda serikalini

*Ofisa mmoja adaiwa kuchukua kodi ya nyumba iliyotolewa serikalini kwa ‘plea bargaining’

*Wadau waomba fedha za kikosi kazi nazo zikaguliwe

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu 

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, ameanzisha ukaguzi wa fedha za faini za watuhumiwa waliokiri makosa ya uhujumu uchumi; JAMHURI linaripoti.

Katika shughuli hii, CAG anakagua kesi zao zilivyokuwa ili kujiridhisha kuhusu kiasi kilichokusanywa.

Akizungumza katika Ikulu ya Chamwino, Dodoma, Machi 30, mwaka huu wakati akimkabidhi Rais Samia Suluhu Hassan Ripoti ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2020/2021, CAG amesema ukaguzi huo pia utahusisha mali zilizotaifishwa na serikali.

“Nimeanzisha ukaguzi wa fedha na utaratibu wa kesi zilizohitimishwa kwa kufuata sheria ya makubaliano ya kukiri kosa, yaani plea-bargaining ya mwaka 2019 kujiridhisha na taratibu zote na kiasi kilichokusanywa kutokana na utaratibu huo. Ukaguzi huu pia utahusisha mali zilizotaifishwa na serikali,” amesema.

Ukaguzi wa CAG umekuja wakati baadhi ya wanasheria na wadau mbalimbali wakihoji kuhusu akaunti ya malipo ya fedha za fidia zinazolipwa na washitakiwa wa makosa ya jinai, yakiwamo uhujumu uchumi na utakatishaji fedha kwa wanaokiri makosa.

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Biswalo Mganga, ndiye aliyefungua akaunti maalumu Benki ya Tanzania (BoT) ya kupokea na kuhifadhi fedha za fidia zinazolipwa na watuhumiwa kupitia plea-bargaining.

Kuna hofu kwamba huenda fedha hizo zilipelekwa katika akaunti hiyo huku ikiwa kama ya mtu binafsi, hivyo kuwapo kwa shaka katika matumizi ya fedha hizo.

Kwa upande mwingine, aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, amewahi kuliambia Bunge kuwa jumla ya Sh bilioni 35.07 zilipokewa na serikali kutoka kwa watuhumiwa mbalimbali waliokiri makosa.

Naye CAG, kupitia taarifa ya ukaguzi ya mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2020, amesema hadi wakati huo, akaunti hiyo ilikuwa na Sh bilioni 52; fedha zilizokaa kwenye akaunti kwa sababu hakuna sheria inayoelekeza matumizi yake.

Tuhuma za matumizi ya fedha, mali

Chanzo kimoja cha habari (jina lake linahifadhiwa kwa sasa) kimelidokeza Gazeti la JAMHURI kwamba baadhi ya mali zilizotaifishwa kutoka kwa watuhumiwa waliokiri makosa hazijapelekwa serikalini kama inavyotakiwa.

Chanzo hicho kinatoa mfano kuwa kuna mtuhumiwa mmoja wa makosa ya utakatishaji fedha alikiri makosa na kuweka nyumba yake iliyopo Mbezi Beach, Dar es Salaam, iwe fidia na kutaifishwa na serikali, lakini alipotoka mahabusu akagundua mpangaji wake analipa kodi kwa ndugu wa ofisa mmoja mwandamizi wa Ofisi ya DPP wa zamani.

“Mambo mengine yanashangaza kweli, kwa sababu baadhi ya mali zimeangukia mikononi mwa watu binafsi, hasa ndugu wa baadhi ya maofisa waandamizi wa DPP.

“Huyu ndugu yangu alitoa nyumba ya Mbezi Beach ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya kukiri makosa na alivyotoka mahabusu akakuta mpangaji wa nyumba yake anamlipa kodi mjomba wa ofisa mmoja mwandamizi wa serikali.

“Sasa wewe jiulize, hiyo ni nyumba moja tu. Je, kuna mali ngapi nyingine hatuzijui zimekwenda kwa hao jamaa badala ya serikalini?” amehoji.

Chanzo kingine cha JAMHURI kimedai kuwa baadhi ya maofisa waandamizi wa Ofisi ya DPP wa zamani wamejitajirisha kupitia fedha za watuhumiwa waliokiri makosa ya uhujumu uchumi.

Mbali na maofisa hao, pia chanzo hicho kinadai kuwa wapo baadhi ya maofisa wa Wizara ya Fedha na Mipango na wakuu wa mikoa waliotumia fedha hizo kujilimbikizia mali kwa kujenga nyumba za kifahari zisizoendana na kipato halisi cha mishahara ya utumishi wa umma.

Pia kinadai kuna tetesi zinazosema kuwa maofisa wengine walizihamisha kwenda kuzihifadhi fedha hizo katika benki za nje ya nchi; baadhi wakijenga hoteli za kifahari mkoani Morogoro na kununua nyumba katika mitaa ya mkoa mmoja Kanda ya Ziwa.

Wamtaka CAG akague fedha za ‘Task Force’

Katika hatua nyingine, wasamaria wema wamemtaka CAG afanye ukaguzi wa fedha zote zilizokusanywa na Kikosi Kazi (Task Force) kilichoundwa na Wizara ya Fedha na Mipango.

Mmoja wa watu hao amesema lengo la kuanzishwa kwa kikosi hicho lilikuwa jema, lakini likaharibiwa na watu wachache waliopewa kazi hiyo.

“Serikali ilikuwa na nia njema kabisa ya kukusanya madeni ndipo ikaunda Kikosi Kazi, lakini hao waliopewa kazi ya kukusanya ndio waliokuwa na shida. Baadhi yao wametajirika wao binafsi kupitia ukusanyaji wa madeni ya serikali.

“Walikuwa wanakwenda kwa wafanyabiashara wanawatisha na kuwabambikia madeni makubwa. Wakileta ubishi, wanaambiwa watafunguliwa mashitaka ya uhujumu uchumi au utakatishaji fedha,” amesema mtoa taarifa wetu.

JAMHURI limeelezwa kuwa CAG anatakiwa kukagua fedha hizo ili ajue uhalali wake, kiasi halisi kilichokusanywa na kupelekwa serikalini na mwenendo wa matumizi yake ulivyokuwa.

“Wafanyabiashara wengine waliofuatwa kudaiwa madeni hayo nje ya ofisi zao kulikuwa na watu maalumu wameshika pingu. Kwamba wakibisha, wanabebwa. Na walikuwa wanaanza kudai kiasi kikubwa cha fedha kuliko uhalisia.

“Si hivyo tu, pia wakasababisha baadhi ya wafanyabiashara kupata magonjwa ya moyo na shinikizo la damu. Lakini hizo fedha nyingi walizokusanya ziliishia mikononi mwao na kiasi kidogo kupelekwa serikalini,” amesema mwanasheria mmoja aliyewatetea watuhumiwa wa kesi za aina hiyo.

Zaidi ya Sh bilioni 100 zilitarajiwa kurejeshwa 

Septemba 30, 2019, Biswalo akiwa DPP, alinukuliwa akisema watuhumiwa 467 wa uhujumu uchumi na utakatishaji fedha walikiri makosa na kuomba msamaha wakati akiwasilisha ripoti kwa Rais Dk. John Magufuli.

Biswalo akasema kiasi cha Sh bilioni 107.84 zitarejeshwa na watuhumiwa hao, na kwamba serikali imetaifisha madini, nyumba na magari yao huku baadhi ya maombi yakiwa yamekwama magerezani na katika ofisi za mikoa.

Baadhi ya washitakiwa wa uhujumu uchumi waliokiri makosa na kulipa fedha ni Harbinder Singh Sethi aliyetuhumiwa kutokana na ufisadi wa Akaunti ya Tegeta Escrow; na mwandishi wa habari za uchunguzi, Erick Kabendera.

Washitakiwa wengine ni aliyekuwa mtuhumiwa wa uhujumu uchumi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Astery Ndege, aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na maofisa wa Benki ya Stanbic, Shose Sinare na Sioi Sumari.

By Jamhuri