Marekani yatumia Bunge kumwengua Waziri Mkuu Pakistan 

Na Nizar K Visram

Imran Khan, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Pakistan, ameondolewa madarakani baada ya Bunge la nchi hiyo kupiga kura ya kutokuwa na imani naye. 

Kura hiyo ilipigwa Aprili 9, mwaka huu baada ya mvutano mkali baina ya Chama chake (Pakistan Tehreek-e-Insaf -PTI) na upinzani. Hatimaye wapinzani wakapata kura 174 kati ya 342, hivyo kufanikiwa kumuondoa Khan madarakani.

Hii ilifanyika baada ya Chama cha MQM-P kuvunja ushirikiano na PTI, hivyo Khan akapoteza wabunge saba waliojiunga na upinzani. Inasemekana makamanda wa jeshi walikubaliana na upinzani. Mwaka 2018 walimuunga mkono Khan akachaguliwa, sasa wamemgeuka.  

Katika kura ya kutokuwa na imani, Bunge liligawanyika karibia nusu kwa nusu, upinzani ukishinda kwa kura mbili tu. Bunge likamchagua Shehbaz Sharif kama Waziri Mkuu mpya atakayeongoza serikali hadi uchaguzi mkuu utakapofanyika. 

Khan alijaribu kukwepa kura ya kutokuwa na imani kwa kumshawishi Spika atangaze kuwa si halali. Iliposhindikana, akamtaka Rais avunje Bunge na kuitisha uchaguzi mpya. 

Lakini Mahakama Kuu ya Pakistan ikasema hatua hiyo ni kinyume cha katiba, hivyo ikaamuru Bunge lipige kura. 

Mara baada ya kuchaguliwa kuwa Waziri Mkuu, Shehbaz Sharif akatangaza kuwa ataifanya Pakistan ‘paradiso’ ya wawekezaji. 

Hatua ya kwanza atakayochukua ni kuendeleza mazungumzo na Shirika la Fedha Duniani (IMF) litoe dola bilioni sita alizoahidiwa Khan mwaka 2019. Khan alitekeleza masharti ya IMF kwa kupunguza ruzuku katika bidhaa muhimu. Pia alibinafsisha mashirika ya umma. Wenyewe wanaita ‘sera ya kurekebisha uchumi’.  

Hata hivyo, IMF wakamtaka aongeze kodi na tozo na kufuta kabisa ruzuku. Hii ikaibua hasira miongoni mwa wananchi na Khan akalazimika kurejesha ruzuku katika gesi na umeme. IMF wakazuia fedha, ndipo wapinzani wakapata fursa ya kumshambulia Khan. 

Waziri Mkuu mpya, Shehbaz Sharif, ni mdogo wa Nawaz Sharif, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Pakistan mara tatu mpaka alipoenguliwa na Mahakama Kuu mwaka 2017 kwa shutuma za ufisadi na rushwa kwa mujibu wa nyaraka za ‘Panama Papers’. 

Mahakama ikamhukumu Nawaz kifungo cha miaka 10 kwa rushwa na kumiliki nyumba za anasa nne zisizoelezeka jijini London ambako anaishi. Binti yake, Maryam, naye alihukumiwa miaka saba na mumewe Safdar akahukumiwa mwaka mmoja jela. 

Shehbaz na Nawaz Sharif pia wametuhumiwa kuwa waliwaua raia 14 na kuwajeruhi 80 katika Chuo cha Minhaj al Quran Academy mjini Lahore.

Waziri Mkuu Shehbaz Sharif ni mfanyabiashara ambaye amekuwa Waziri Kiongozi wa Jimbo la Punjab mara tatu. Yeye naye ameonekana na hatia katika kashfa ya rupia bilioni 17 kuhusiana na biashara ya sukari. 

Ametuhumiwa na mwanawe Hamza kwa kosa la kutakatisha rupia bilioni 16 za Pakistan kupitia Kampuni ya Ramzan Sugar Mills. (rupia moja ya Pakistan ni sawa na Sh 12).

Kwa upande wa pili, Imran Khan hajawahi kufunguliwa kesi yoyote ya ufisadi au ubadhirifu. Alipokuwa waziri mkuu aliikwaza Marekani kwa sababu alichukua msimamo wa kutofungamana na upande wowote katika sera ya kimataifa.

Marekani ilikasirika zaidi pale Khan alipotembelea Urusi na kukutana na Rais Putin Februari 24, mwaka huu, siku Urusi ilipoishambulia Ukraine. Khan akasaini mkataba wa kununua tani milioni 2 za ngano pamoja na gesi kutoka Urusi.

Halafu akasaini makubaliano na China kuanzisha mradi wa ushoroba wa kiuchumi (economic corridor) kati ya China na Pakistan kwa gharama ya dola bilioni 62. Marekani ikazidi kukasirika.

Machi 1, 2022 mabalozi 22 kutoka Umoja wa Ulaya na kwingineko wakamuandikia Khan barua ya pamoja ikimtaka kuunga mkono Azimio la Umoja wa Mataifa likiilaani Urusi kwa kuishambulia Ukraine. 

Khan akawajibu kwa jeuri akisema: “Hivi mnatuona sisi ni watumwa wenu?”

Chini ya uongozi wa Khan, Shirika la Ndege la Pakistan (PIA) likajikwamua kutoka katika madeni. Serikali yake ikaanzisha miradi 6,000 iliyoajiri watu 800,000 hata wakati wa mlipuko wa Uviko-19. Akadhibiti  maambukizi ya Uviko bila ya kuwafungia raia ndani. Akahamasisha upandaji wa miti bilioni moja.

Khan aliona familia maskini zikilala barabarani nyakati za kipupwe. Akaanzisha mradi wa kuwajengea makazi. Akawa anawatembelea na kula nao. 

Ukusanyaji wa kodi uliongezeka na kufikia rupia bilioni 6,000. Vijana wajasiriamali wakapewa mikopo jumla ya rupia bilioni 30 hadi 50. Kwa mara ya kwanza Pakistan ikaanza kuzalisha simu janja pamoja na baisikeli za umeme na mashine (processor) za kompyuta.

Huyu ndiye Imran Khan ambaye alipigiwa kura ya kutokuwa na imani na wabunge. Wananchi milioni moja wakamiminika barabarani wakimuunga mkono. Akawaonyesha barua ya kidiplomasia kutoka Marekani ikisema Imran Khan anastahili kuenguliwa na Bunge la sivyo hapatakalika. Akasema: “Huu ni uchochezi wa kigeni.”

Khan alisema kuwa ofisa mwandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani anayeshughulikia Asia Kusini, Donald Lu, alimtahadharisha Balozi wa Pakistan nchini Marekani, Asad Majeed kuwa: “Kutakuwa na matokeo mabaya iwapo kura ya kutokuwa na imani na Khan haitafanikiwa.”

Khan akasema hayuko tayari kusalimu amri kwa ubeberu na ndiyo maana aliiwasilisha barua hiyo mahakamani na kwa wakuu wa jeshi akitaka uchunguzi ufanywe, lakini hakuna hatua iliyochukuliwa.

Mwishowe kamati ya usalama wa taifa ikakutana. Uamuzi wa pamoja ukachukuliwa kuwa Marekani inapaswa ikemewe. Baada ya hapo Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan ikamwita Balozi wa Marekani na kumpa karipio.  

Kwa vile kulikuwa na njama za kimataifa za kumpindua, ndipo Khan akaamua kuzuia kura ya wabunge dhidi yake kwa sababu alijua kuwa njama zilifanywa kuwanunua wabunge. Hiyo ikashindikana kwa sababu mahakama iliamuru kura iendelee.  

Rais Joe Biden wa Marekani alikataa kuonana au hata kuzungumza kwa simu na Khan alipokuwa waziri mkuu. Katika historia ya Pakistan, watawala wake wamekuwa wakipokea miongozo kutoka Marekani. Mawaziri wakuu wa zamani Moeen Qurashi na Shaukat Aziz walipendekezwa na IMF inayoongozwa na Marekani. 

Khan amesema alipewa ushahidi na usalama wa taifa ukionyesha jinsi kura za wabunge zilivyonunuliwa. Wakuu wa majeshi wakatangaza kuwa wao hawatafungamana na upande wowote. 

Khan akasema inasikitisha kuwa walinzi wa taifa wanakaa kimya wakati nchi ya kigeni inaingilia mambo ya ndani kwa kupanga njama ya kuipindua serikali halali.

Hivi ndivyo Pakistan ilivyo, kwani mwaka 2001 aliyekuwa waziri mkuu, Jenerali Pervez Musharraf, alipokea simu kutoka Marekani ikimwambia aungane na Marekani kuishambulia Afghanistan la sivyo na Pakistan nayo itapigwa mabomu. Musharaf akafyata mkia. 

Aidha, wengi wanaamini kuwa majasusi wa Marekani walihusika katika kuuawa kwa viongozi wa Pakistan kama Liaquat Ali Khan, Zulfiqar Bhutto, Zia al Haq na Benazir Bhutto. Inasemekana na Imran Khan naye angeshughulikiwa kama angebaki madarakani.

Kwa muda mrefu jeshi la Pakistan limekuwa na uhusiano wa karibu na Marekani. Ndiyo maana mara nyingi Marekani huwa inatumia jeshi hilo.  

Ndipo tunaona tangu Pakistan kuzaliwa mwaka 1947 wakuu wa jeshi wamepindua katiba na kukamata serikali mara nne. Nao ni Field Marshal Ayub Khan (mwaka 1958 hadi 69), Jenerali Yahya Khan (1969-71), Jenerali  Muhammad Zia-ul-Haq (1977-88) na Jenerali  Pervez Musharraf (1999-2008).

Halafu kuna mawaziri wakuu kuondolewa madarakani kabla ya kumaliza muda wao, kama Benazir Bhutto (1988-90 na 1993-96) na Nawaz Sharif (1990-93 na 1997-99). Wote wawili walienguliwa na rais wa Pakistan kwa matakwa ya jeshi. Uwezo huu wa kijeshi uliingizwa katika katiba mwaka 1985 wakati nchi ilipokuwa ikitawaliwa na Jenerali Zia.

Habari za hivi karibuni zinasema Mahakama ya Pakistan imeahirisha hadi Aprili 27 kesi ya waziri mkuu, Sharif na mwanawe Hamza. Hamza anagombea nafasi ya waziri kiongozi katika Jimbo la Punjab.

Naye Imran Khan amesema inasikitisha kuwa nchini Pakistan mtu anayekabiliwa na kesi za ufisadi, pamoja na familia yake, anakuwa waziri mkuu.

[email protected]