Wiki iliyopita imekuwa ya kihistoria nchini Canada, kwani serikali ya nchi hiyo baada ya kufanya utafiti kwa muda mrefu hatimaye imefikia uamuzi wa kuruhusu matumizi binafsi ya bangi kwa watu wake.

Maduka yalianza kuuza bangi saa 06:01 usiku wa kuamkia Jumatano wiki iliyopita, baada ya awali serikali ya nchi hiyo kuwa imetumia miaka miwili kutunga sheria za kurasmisha matumizi ya bangi.

Wacanada wengi walifurahia hatua hiyo ya serikali kwa kiwango cha kuishangaza dunia, kutokana na wanachokiita kuwa wanatumia “bangi kwa burudani”, kitu ambacho sheria za nchi hiyo kwa muda mrefu zimewakosesha.

Hata hivyo, furaha ya Wacanada hao inaelekea itakuwa ya muda mfupi, kwani siku mbili baada ya bangi kurasmishwa imekwisha madukani.

Imekuwapo misururu mirefu ya wananchi wanaojipanga nje ya maduka rasmi kununua bangi hiyo, ila kuna tishio sasa kuwa kuna upungufu mkubwa wa bangi nchini humo.

Maajabu ya dunia hayaishi. Polisi wa nchi hiyo wamelazimika kuitwa usiku wa manane kuwasaidia wauza duka ambao wamezidiwa na idadi ya wateja wanaotaka kununua bangi, huku wananchi wengi wakisukumana kwa hasira baada ya kupata taarifa kuwa bangi inaelekea kwisha madukani.

Bill Blair, ambaye ni Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu wa Toronto, ameliambia Shirika la Utangazaji la Canada (CBC) kuwa nchi haina bangi ya kutosha mahitaji ya wateja.

“Tunatarajia, kama unavyofahamu, baadhi ya maduka yanaweza kuishiwa (bangi) na kutakuwapo kukimbizana katika upatikanaji (wa bangi),” amesema. “Lakini unajua wanayo mifumo mizuri na naamini itafanya kazi,” ameongeza.

Jumatano iliyopita Canada imekuwa nchi ya kwanza kati ya nchi zilizoendelea kurasmisha matumizi ya bangi. Kidunia inakuwa ya pili kuruhusu matumizi ya bangi baada ya nchi ya Uruguay. Hata hivyo, wataalamu wanasema pamoja na kwamba Canada imefanya utafiti, wanasubiri kuona hali itakuwaje hasa kwa madereva wanaoendesha magari kwa muda mrefu.

Chini ya sheria mpya, kila mwananchi anaruhusiwa kuwa na msokoto wenye gramu 30 hadharani na kila familia inaruhusiwa kupanda miche minne ya bangi karibu na nyumba yao.

Matumizi ya bangi kama tiba nchini Canada yaliruhusiwa tangu mwaka 2001, na Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau, ametumia miaka miwili kubadili sheria kuruhusu matumizi ya “bangi kwa burudani.”

Kwa mujibu wa takwimu rasmi, inatarajiwa kuwa wananchi wa Canada wapatao milioni 5.4 watanunua bangi kutoka kwenye maduka rasmi mwaka huu (2018). Idadi hii ni asilimia 15 ya Wacanada. Kwa sasa Wacanada wanaotumia bangi ni karibu milioni 4.9.

Taasisi ya Lift iliyopo Vancouver nchini Canada inayotetea matumizi salama ya bangi, inasema inaamini sekta ya bangi ina uwezo wa kuzalisha kati ya kilo 400,000 na 500,000 kwa mwaka. Je, Canada itakuwa tayari kuagiza bangi kutoka nje ya nchi na baadhi ya mikoa kama ya Kanda ya Ziwa na Pwani nchini Tanzania? Fuatilia.

Please follow and like us:
Pin Share