Mwanahabari, Jamal Khashoggi, aliuawa katika vita katika Ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul, runinga ya taifa hilo imesema ikinukuu uchunguzi wa awali.

Naibu Ofisa Mkuu wa Idara ya Ujasusi, Ahmad al-Assiri na Mshauri Mkuu wa Mwanamfalme Mohammed Bin Salma Saud al-Qahtani walifutwa kazi kufuatia kisa hicho.

Wakati huohuo, Uturuki imeapa kufichua maelezo yote kuhusu mauaji ya mwandishi huyo baada ya Saudia kukiri kwa mara ya kwanza kwamba aliuawa katika ubalozi wake mdogo mjini Istanbul.

“Uturuki haitaruhusu mauaji yake kufichwa,” anasema msemaji wa chama tawala cha taifa hilo.

Saudia imesema siku ya Ijumaa kwamba, Khashoggi, ambaye ni mkosoaji maarufu wa Saudia alifariki dunia alipokuwa ‘akipigana ngumi’.

Maofisa wa Uturuki awali walikuwa wanasema kwamba aliuawa kwa makusudi ndani ya ubalozi huo na mwili wake kukatwakatwa.

Mapema wiki iliyopita maofisa wa Uturuki ambao hawakutaka kutajwa majina yao waliviambia vyombo vya habari kwamba walikuwa na ushahidi wa sauti na kanda za video kuthibitisha hilo.

Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema kuwa kile kilichotokea hakitakubalika lakini akaongezea kuwa Saudia ni mwandani wake mkuu.

Hii ni mara ya kwanza kwa ufalme huo kukiri kwamba Khashoggi amefariki dunia. Saudia inasema kwamba haikushiriki katika kutoweka kwa mkosoaji wake mkubwa wakati alipoingia katika ubalozi mdogo mjini Istanbull Oktoba 2, mwaka huu ili kutafuta vyeti vya ndoa yake.

Ufalme wa Saudia ulikuwa umeshinikizwa kuzungumza kuhusu kutoweka kwa Khashoggi baada ya maofisa wa Uturuki kusema kuwa aliuawa kwa makusudi ndani ya ubalozi huo na mwili wake kukatwakatwa.

Siku ya Ijumaa maofisa wa Polisi wa Uturuki waliendeleza upekuzi wao hadi katika msitu mmoja jirani ambapo maofisa wasiotaka kujulikana wanaamini mwili wake ulikuwa umetupwa.

Wachunguzi wanahoji iwapo washirika wa Saudia kutoka mataifa ya Magharibi wataamini madai hayo ya Saudia na iwapo itawashawishi kutochukua hatua zozote kali dhidi ya taifa hilo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza imesema kuwa inafikiria kuchukua hatua baada ya kutolewa kwa ripoti hiyo.

Uongozi wa Saudia sasa unatumaini kukiri kwake kwa kuchelewa kwamba Khashoggi alifariki dunia ndani ya ubalozi huo na kuchukua hatua za kuwafuta kazi maofisa wake na kuwakamata wengine kutatosha kufunika yaliyotokea.

Hii ni hatua mojawapo ya kuchapisha ukweli wa kile kilichotokea.

Kutokana na hatua ya uongozi wa Saudia kukataa kukiri kuhusu kuuawa kwa Khashoggi, haijulikani iwapo viongozi wake wangekiri bila shinikizo la kimataifa.

Serikali ya Saudia inasema nini?

Taarifa kutoka kwa mwendesha mashtaka wa Saudia inasema kuwa vita ilizuka kati ya Khashoggi, ambaye alikuwa amekosana na Serikali ya Saudia na watu aliokutana nao katika ubalozi huo na kuuawa.

Uchunguzi ambao bado unaendelea, unaonyesha raia 18 wa Saudia wamekamatwa. Mamlaka ya Saudia bado haijatoa ushahidi wowote ili kuunga mkono hoja yake.

Maofisa ambao hawakutaka kutajwa majinja yao waliozungumza na vyombo vya habari – Reuters na New York Times wanasema kuwa raia wa Saudia hawakujua mwili huo ulikopelekwa baada ya kupatiwa washirika wake ili kuukatakata.

Nani amefukuzwa kazi?

Saud al-Qahtani ni mtu maarufu wa Ufalme wa Saudia na mshauri wa Mwanamfalme Mohammed bin Salman. 

Meja Jenerali Ahmed al-Assiri ndiye msemaji mkuu wa ufalme wa Saudia kuhusu vita ya Yemen. Alizungumza na BBC mwaka 2017 kuhusu mzozo huo akitetea vitendo vya Saudia.

Mfalme Salman pia amedaiwa kuamrisha kuundwa kwa kamati inayoongozwa na Mwanamfalme Mohammed, kubadilisha idara ya ujasusi.

Saudia inasema ilitumia habari zilizotolewa na mamlaka ya Uturuki ikiwa mojawapo ya uchunguzi wake kuwahoji baadhi ya washukiwa.

Please follow and like us:
Pin Share