Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Serikali imeiagiza wenye maabasi nchini kuhakikisha madereva na wahudumu wao wote wa usafiri wa umma nchini wanapata  mafunzo ya namna ya kutoa huduma ya kwanza ndani ya kipindi cha miaka mitatu.

Imesema mafunzo hayo ni muhimu kwani yatasaidia kuokoa maisha ya abiria inapotokea ajali kwasababu madereva na wahudumu watakuwa na uwezo wa kuwapa abiria wao huduma ya kwanza.

Serikali pia imekipongeza Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na mkuu wake wa chuo, Profesa Edda Lwoga kutonana na ubunifu wake wa kuanzisha kozi nyingi.

Baadhi ya wahudumu wa mabasi waliohitimu CBE leo na kupewa vyeti vyao

Agizo hilo lilitolewa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, wakati akifunga mafunzo na kutoa vyeti kwa wahudumu wa mabasi yaliyoendeshwa na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).

“Naiagiza LATRA iwasilishe mpango mkakati  serikalini wa namna ya kuhakikisha wahudumu wote wa mabasi na madereva wanapata mafunzo ya namna bora yaa kuwahudumia abiria wakati wa dharura ili tujue mwaka wa kwanza mtafanya nini hadi mwaka wa tatu mtafikia lengo gani,” alisema Kihenzile.

Kihenzile alitoa wito pia kwa vyuo vingine kuiga CBE kwasababu mahitaji ya mafunzo ya aina hiyo ni makubwa na chuo hicho hakiwezi kutoa mafunzo kwa wahudumu wa mabasi yote yanayokadiriwa kufikia 5,000.

Akipongeza chuo cha CBE kwa ubunifu mkubwa wa mafunzo hayo ambayo alisema yamekuja wakati mwafaka kwani sekta ya usafiri itapata heshima.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile akikabidhi cheti kwa mhudumu wa mabasi aliyehitimu katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), katika hafla iliyofanyika jana chuoni hapo. Kulia ni Mkuu wa chuo hicho. Profesa Edda Lwoga.

“Kusema kila mtu anaweza kusema, kupanga kila mtu anaweza kupanga lakini kwenye utekelezaji watu wengi wanashindwa kutekeleza lakini hapa CBE mmekuwa mkipanga na mnatekeleza,” alisema

“Wewe Profesa Lwoga kwa umri wako mdogo umefanya mambo makubwa, taifa linamatarajio makubwa sana kwako na kwa uwezo wako wewe ni uthibitisho kwamba wanawake wanaweza kufanya mambo makubwa wakipewa nafasi,” alisema

Alisema moja ya maeneo ambayo watanzania wanalalamikiwa ni eneo la utoaji wa huduma ambapo baadhi ya waajiri wanalazimika kwenda nje ya nchi kutafuta watumishi wa kufanya nao kazi.

Mkuu wa Chuo cha CBE, Profesa Edda Lwoga tangu waanze mafunzo hayo mapema mwaka huu wameshatoa wahitimu wako 42.

Profesa Lwoga alisema sekta ya usafiri wa umma inakabiliwa na uvunjifu wa sheria na mmomonyoko wa maadili ndivyo sababu CBE iliamua kuanzisha mafunzo hayo ili kukabiliana na changamoto hizo kwenye usafiri wa umma nchini.

“Katika kuunga mkono juhudi za serikali tuliamua kuanzisha mtaaala huu mwaka jana na ukasajiliwa na LATRA kwa hiyo mafunzo haya yanatolewa kwa mujibu wa sheria ndiyo maana tunawahimiza wenye mabasi walete watumishi wao,” alisema

Alisema wahudumu hao wamejifunza kwa vitendo matumizi ya mifumo ya tiketi za kielektroniki na maadili wanayopaswa kuzingatia wakati wote wanapokuwa wakitoa huduma kwenye kazi zao.

Alisema Kampasi ya CBE Dar es Salaam ina wanafunzi 14,000, Dodoma wanafunzi 3,700, Mwanza 1,700, Mbeya wanafunzi 1,000.

Profesa Lwoga alisema CBE itaanza kutoa mafunzo kama hayo hivi karibuni kwenye kampasi zake za Dodoma Mwanza na Mbeya.

Naye Afisa Rasilimali Watu wa Shirika la Reli (TRC), Herick Foya, alisema TRC inasafirisha abiria zaidi ya 1,000  kwa kila safari moja hivyo mafunzo kama haya yana umuhimu mkubwa kwa shirika hilo.

 “Treni zetu bado zinaendelea na majaribio na umma utajulishwa lini hasa zitaaanza kutoa huduma kwa hiyo nasisi TRC tutakuwa na wahudumu wengi sana ambapo naona kuna umuhimu wa kuwaleta hapa CBE kupata mafunzo kama haya,” alisema

Naye Mwanasheria wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Joseph Ndosi, alikipongeza chuo hicho kwa kuja mafunzo hayo hasa wakati huu ambapo mmomonyoko wa maadili umekuwa mkubwa kwenye sekta ya usafiri wa umma.

“Wahudumu wanaopata mafunzo haya waende kusimamia mwongozo wa maadili wa vyombo vya usafiri wa umma ili sekta hiyo iwe na heshima yake na tuachane na kufanyakazi kwa mazoea,” alisema

Mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Tanzania Red Cross Society TRCS, Dk. Hilary  Ngude, alisema mpango wa kuwajengea uwezo wahudumu wa mabasi umekuja wakati mwafaka kwani huduma ya usafiri imekuwa muhimu na inapaswa kuwa rafiki kwa abiria.

“Sisi TRCS  kushiriki kwenye mafunzo ya wahudumu kama haya tunaona ni jambo la kujivunia kwasababu tunaongeza wigo wa ushiriki wa wananchi katika uokoaji yanapotokea majanga mbalimbali kwa hiyo nawapongeza sana CBE,” alisema

Aliomba serikali kusimamia sekta zote za usafirishaji ili wahudumu wake wapewe mafunzo ya aina hiyo ili kupunguza madhara yanapotokea majanga kama ya moto au kuzama kwa vyombo vya usafiri majini.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile akikabidhi cheti kwa mhudumu wa mabasi aliyehitimu katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), katika hafla iliyofanyika jana chuoni hapo. Kulia ni Mkuu wa chuo hicho. Profesa Edda Lwoga.