Rais Jakaya Kikwete
Rais Jakaya Kikwete
Mwenyekiti Mkoa atoboa siri nzito
Wakati kukiwa na dalili za kuwapo uchaguzi mdogo Jimbo la Arusha Mjini, hali ya mambo ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeelezwa kuwa mbaya.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Onesmo ole Nangole, ameonyesha wasiwasi wake juu ya kukosekana kwa mshikamano na umoja ndani ya chama hicho kikongwe.

Kufanyika kwa uchaguzi huo kutawezekana tu endapo Mahakama Rufani itabariki hukumu ya Mahakama Kuu kumvua ubunge aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Godbless Lema (Chadema).

Katika mahojiano na JAMHURI, Nangole anakiri kuwa CCM ina nguvu katika Jimbo la Arusha na Mkoa mzima wa Arusha, lakini inakwazwa na makundi yanayozaliwa baada ya kura za maoni.

“Chama kina nguvu kubwa, lakini ni ukweli kwamba kimegawanyika…kuna mpasuko mkubwa unaosababishwa na kura za maoni. Watu wakishindwa kwenye kura za maoni wanaendeleza makundi.

“Chadema hawana nguvu, kinachowafanya waonekana wana nguvu ni baada ya kura za maoni ndani ya CCM. Baadhi ya wanaoshindwa wanakwenda kuisaidia Chadema. Mfano mzuri ni pale aliposimama Batilda (Dk. Batilda Burian) na Mrema (Felix Mrema). Hiyo ndiyo inayosaidia kuifanya Chadema iwe na nguvu.

“Kwenye kura za maoni za Arumeru Mashariki wapo walioshindwa wakaamua kupita mitaani kufanya kampeni za kusema ‘chagua mtu, usichague chama’, tena wanasema wazi ‘chagua mtu wa Chadema’. Hii imetuumiza sana kwenye kampeni,” amesema Nangole.

Kuhusu Arumeru Mashariki, Mwenyekiti huyo anasema kitafanyika kikao cha tathmini ili kuwatambua waliosababisha mgombea wa CCM ashindwe.

“Tunafanya hivyo kama njia ya kujisahihisha, sasa ni wakati mwafaka wa kujichunguza,” anasema.

Anatamba kwamba pamoja na kushindwa Arumeru Mashariki, CCM haina wasiwasi endapo kutaitishwa uchaguzi mdogo Jimbo la Arusha Mjini.

“Hayo ni mapambano, unaposhindwa unakubali kushindwa, lakini si kushindwa kwa kuhujumiana ndani ya chama. Chama chetu (CCM) kinajiumiza chenyewe kwa makundi,” anasema.

Duru za kisiasa mkoani Arusha zinaonyesha kuwa muda mfupi baada ya Lema kuvuliwa ubunge, baadhi ya wana-CCM wamegawanyika katika makundi makuu mawili.

Kundi la kwanza ni lile linaloamini kuwa kufanyika kwa uchaguzi mdogo, kunaweza kusaidia kulirejesha jimbo hilo katika himaya ya CCM.

Kundi la pili ni lile lililoona kuwa hukumu iliyotolewa na Jaji Gabriel Rwakibarila iliyomvua ubunge Lema, inaiweka CCM majaribuni ikiwa ni siku chache baada ya kuangushwa kwenye uchaguzi mdogo Jimbo la Arumeru Mashariki.

Katika uchaguzi huo, Joshua Nassari alimshinda kwa kura takribani 7,000 mgombea wa CCM, Sioi Sumari.

Mjini Arusha, wanachama wengi wa CCM wanaamini kuwa uchaguzi mdogo ukiitishwa leo, Chadema itawagaragaza kama ilivyowatokea Arumeru Mashariki. Wanaamini kuwa Arusha bado ni ngome imara ya chama hicho.

Wanaona uamuzi wa Jaji Rwakibarila unazidi kuwaweka majaribuni, na kwa maneno mengine wanaona heri hukumu ingekuwa tofauti na ilivyotolewa.

Hata hivyo, uamuzi wa Chadema uliotangazwa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, mwishoni mwa wiki wa kukata rufaa katika Mahakama ya Rufani Tanzania, umepokewa kwa bashasha na baadhi ya wana-CCM.

Furaha yao ni kuona kuwa kama inawezekana kisheria, Lema abaki na ubunge na wao waendelee kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka 2015. Wanaona kufanyika kwa uchaguzi mdogo kunaweza kuwasononesha kutokana na nguvu kubwa walizonazo Chadema.

Lakini kwa upande wao, wafuasi wa Chadema wameonyesha kutofurahishwa na uamuzi uliotangazwa na Mbowe. Wanachotaka wao ni kuona uchaguzi mdogo unafanyika haraka ili waiadhibu tena CCM kama ilivyotokea Arumeru Mashariki.

 

 

 

1511 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!