Jumatano iliyopita, baadhi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka kata mbili za Azimio wilayani Temeke na Tandale, Wilaya ya Kinondoni mkoani  Dar es Salaam, waliandamana ili kupinga hujuma walizodai zinavuruga uchaguzi mkuu wa ndani wa chama hicho na jumuiya zake zote unaoendelea hivi sasa.

Huku wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali, wanachama hao walidai kuwa baadhi ya wabunge na madiwani katika jiji hilo, wamekuwa wakiwapanga watu wanaotaka wawe viongozi na kuwaacha waliohangaika kwa miaka mingi  wakikitumikia chama hicho.

Miongoni mwa tuhuma zilizotolewa katika maandamano hayo ni kukithiri kwa rushwa, na kwamba baadhi ya wagombea wamekuwa wakitamba kuwa “wana watu hadi ngazi ya taifa”, kitu ambacho kinawavunja moyo wasiokuwa na kiongozi yeyote wa kuwabeba.

Siku moja kabla ya maandamano hayo kufanyika, Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama hicho (UVCCM) wa Mkoa wa Dar es Salaam, Omar Ng’wanang’walu, naye alitangaza kusimamisha uchaguzi wa jumuiya hiyo katika baadhi ya kata kutokana na kasoro kadhaa ambazo zimetokea.

Akitumia mamlaka yake kama Mkurugenzi wa Uchaguzi wa UVCCM wa Mkoa huo, Katibu huyo alizitaja baadhi ya kata zilizokumbwa na matatizo hayo kuwa ni Mbagala Kuu iliyopo wilayani Temeke; Magomeni, Makurumla na Kawe za wilaya ya Kinondoni.

“Nimewaita watendaji na wagombea (wa kata hizo ili) tujadiliane, hii ni kutokana na baadhi yao kuhisi kuna upendeleo umefanyika katika urudishaji majina kutoka wilayani, hivyo ni lazima niwasikilize kabla ya kutoa uamuzi,” alisema kama alivyonukuliwa na vyombo vya habari akizungumzia suala hilo.

Uchaguzi mkuu wa ndani wa CCM ulioanza Februari, mwaka huu, unatazamiwa kumalizika Novemba, wakati utakapofanyika Mkutano Mkuu ili kuchagua Mwenyekiti, Makamu Wenyeviti (Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar), Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na jambo hilo kuhitimishwa kwa kuchagua Wajumbe wa Sekretarieti ya Taifa.

Hitimisho hilo litakuwa ni kukidhi matakwa ya Ibara za 110(1) – (7), 111(1) – (4) na 112(1) –    (4) za Katiba ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 1977 Toleo la 2010, ukurasa wa 171 – 176.

Kasumba moja chafu waliyonayo baadhi ya viongozi wa kisiasa barani Afrika, ni kutotaka kung’oka madarakani, ugonjwa ambao umeathiri idadi yao kubwa kuanzia ngazi za chini kabisa mpaka wakuu wa nchi au serikali zake.

Wakati wanapobembeleza wachaguliwe hasa kwa mara yao ya kwanza huzungumza kwa makini, hekima, busara na kila aina ya mvuto na ushawishi kwa wapiga kura wao, wale ambao siku zote huahidi kutenda haki sawa kwa wote na kutumia nyadhifa zao kwa faida ya kila mmoja.

Ajabu inayokuja wakishachaguliwa na kuanza kazi, hubadilika na kuwa miungu watu, wale wanaotaka waabudiwe na kila mmoja wakiwamo waliokuwa wakiwapigia hadi magoti ili kuwaomba kura mikutanoni, majumbani au kwenye vikao maalumu.

Wanabadilika na kutotaka kabisa kufanana kwa namna zote na wapiga kura wao, badala yake hutaka wanyenyekewe, wabembelezwe na kuombwa kwa kila jambo hata wanalopaswa kufanya kwa sababu ni kazi yao. Huo ndiyo msingi unaosababisha wabunge na madiwani kwa mfano katika CCM kutotaka kung’oka iwe mwaka 2015, 2020 na kuendelea huku wengine wakifikia hadi hatua ya kuwaza au kutamani hata wafie madarakani.

Wanataka ubunge ama udiwani ugeuke kuwa miliki yao na watoto wao, hivyo ili kuulinda hufanya kila wanavyoweza ili wasitoke. Hapo ndipo wanapopandikiza vibaraka katika uongozi wa ndani ya chama na kazi yao huwa ni moja tu: kuwalinda kwa nguvu zao zote, maarifa yao yote na uwezo wote walionao kutoka midomoni hadi kwa njia ya maandishi.

Wanakuwa tayari kufanya chochote ili kuhakikisha diwani au mbunge aliyewasaidia kupata nafasi hizo hatoki ili nao wasitoke, jambo linalosababisha mitafaruku isiyokuwa na maana wala faida yoyote kwa chama.

Sina kielelezo chochote cha kuyaunga mkono maandamano ya wana-CCM kutoka Tandale na Azimio katika upande wa kwanza, na pia sina ushahidi wowote wa kuiunga mkono au kuikataa hatua iliyochukuliwa na Ng’wanang’walu kwa UVCCM katika upande mwingine.

Ninachoweza kukiri katika makala yangu haya ni ukweli kuwa lipo tatizo kubwa kwa baadhi ya madiwani, wabunge na viongozi wengine wa CCM, UVCCM, Umoja wa Wazazi na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kupandikiza watu wao kila unapofika uchaguzi, wale wanaofanya hivyo ili waweze kushika nafasi za utawala, utendaji na uongozi kwa ajili ya faida zao wenyewe.

Wanakuwa tayari kwa kauli na vitendo kuwatetea kwa namna zote ili majina yao yapitishwe na kila kikao cha uteuzi, jambo linalofanywa kwa kuwarubuni baadhi ya wajumbe ikiwamo kutumia njia chafu ya kuwapa rushwa na kadhalika. Wanashindwa kuheshimu katiba ya chama chao inayozuia kwa namna zote vitendo vya rushwa iwe kwa kutoa ama kupokea, na pia wanashindwa kuheshimu maadili wala kanuni zozote wakati wowote na mahali popote.

Mathalani, Ibara ya 18(1) – (3) ya Katiba hiyo inasema, ni mwiko kwa kiongozi “kutumia madaraka aliyopewa kwa ajili ya manufaa yake binafsi au kwa upendeleo, au kwa namna yoyote ambayo ni kinyume cha lengo lililokusudiwa kupewa madaraka hayo”. Inazuia kiongozi “kupokea mapato ya kificho, kutoa au kupokea rushwa, kushiriki katika mambo yoyote ya magendo au mambo mengine yaliyo kinyume cha lengo lililokusudiwa” na mwisho, katiba hiyo inasema “miiko mingine ya viongozi itakuwa kama ilivyowekwa katika Kanuni zinazohusika”.

Wanaoshiriki katika vitendo hivyo wakiwamo madiwani na wabunge, viongozi wa chama hicho chenyewe, UVCCM, UWT na Wazazi wakilenga kujijengea mazingira ya kutong’oka madarakani, wakataka wabaki maisha yao yote hata kama kwa njia chafu ndio virusi katika CCM. Hao ndiyo chama hicho kilichopo madarakani, jumuiya na ofisi zake zote kwa kila ngazi inabidi kibuni na kuweka utaratibu maalumu wa kuwafuatilia kwa kina, kuwabaini na wale wanaothibika kufanya uovu huo watimuliwe mara moja.

Bila ya kuchukua hatua ngumu na madhubuti dhidi ya vitendo vya rushwa, upendeleo na uonevu vinavyofanywa na baadhi ya viongozi wakiwamo madiwani, wabunge na wajumbe wa vikao vinavyochuja majina ya wanachama wanaoomba kugombea uongozi, vitaendelea bila woga na hata kikomo.

Hapo ndipo Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama, na wasaidizi wake wote wanapopaswa kuilinda, kuihifadhi na kuitetea kwa nguvu zao zote katiba ya chama hicho ikiwamo kuchukua hatua za haraka hasa kwa kila mwanachama na kiongozi anayekwenda kinyume chake.

Kama hata Mwenyezi Mungu aliyetuumba ameweka kanuni, sheria na masharti ya kuishi na adhabu kwa watu wote wasiokubali kumtii, kwa nini wanaoihujumu CCM na taasisi zake wasitimuliwe mara moja?

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa Simu Na. 0659 220 220 na 0762 633 244

 

1161 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!