Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeshindwa kujifunza au kimepuuza matokeo ya migawanyiko na anguko kwa serikali mbalimbali duniani ziliendekeza tawala za kiimla dhidi ya haki, utu na usawa.

Anguko la tawala dhalimu zilizodumu madarakani kwa ubabe na kukosa nguvu za hoja zilizokataliwa na kuanguka kwa kishindo ambazo CCM, imeshindwa kujifunza kwa kujidanganya kuwa itatawala milele ni kama zile Zaire (sasa Jamhuri ya Kimekrasia ya Kongo), Libya, Misri, Afrika ya Kusini (iliyokuwa chini ya utawala wa makaburu),Urusi na serikali zingine zilizoporomoka.

Kujisahau kwa CCM kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na watawala na mfumo wenyewe utawala ambao hautaki kwenda kulingana na majira yaliyopo sasa na pengine uvivu wa fikra ambao ni ugonjwa hatari unaowasumbua watanzania wengi kwa nusu karne sasa.

Mtaji mkubwa unaotumiwa na tawala chovu na dhalimu duniani hasa nchi zilizokosa demokrasia ya kweli yenye kulenga kukuza uchumi kwa wananchi wake na faida ya nchi yao kwa ujumla ni ujinga, umaskini, rushwa, ubabe na kutojitambua kwa wananchi.

 

Ujinga

Ujinga ni mtaji mkubwa kwa watawala wenye hofu. Hawa hawatapenda kuona wananchi wakipata elimu bora kwa kushinikiza mifumo ya elimu kwa matabaka. CCM wamefaulu kutumia njia hii; watoto wa maskini watamudu kuwapeleka watoto wao shule zinaoitwa za kata zinazokabiliwa na ukosefu wa vitendea kazi na walimu lengo wasipate elimu bora.

Ni wazi kwamba katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu wako watu ambao kwa ujinga walionao watakuwa ni sehemu ya mtaji wa CCM. Watu wa namna hii wamejihakikishia kuwa wao ni wajinga wa kudumu, hususani wale waishio maeneo ya vijijini. Hawatapenda kuona wananchi wote wakinufaika na elimu bora zaidi ya watoto wao wanaoandaliwa kuwatawala watoto wa kimaskini kila siku.

 

Umaskini 

Kete ya umaskini ni mtaji mkubwa kwa tawala dhalimu duniani. Ni rahisi kumtawala maskini kama upendavyo kwa kumsababishia umaskini wa kumtosha. CCM wamefanya hivyo, wanafanya hivyo na wanaendelea kufanya hivyo.

Kutokana na umaskini wa watanzania wengi huku kikundi cha watu wachache kikinufaika na rasilimali za nchi na kujigeuza mawakala wa wanyonyaji waliokaribishwa tena kwa majina ya kupendeza ya “wawekezaji,” wakitwaa rasilimali za nchi watakavyo na kupewa misamaa ya kodi. Haya ndio matokeo ya kuwaamini viongozi wasiojitambua.

Mwishoni mwa wiki iliyopita nilikuwa napewa habari na kada mmoja wa chama kinachoondoka madarakani sasa (CCM) kwamba mgombea mmoja wa nafasi ya ubunge katika jimbo la Ukonga jijini Dar es Salaam, kwa nguvu yake ya fedha amepita kwa kishindo katika kura za maoni baada ya kuwapa chakula, vinywaji na rushwa ya Sh. 10,000/- kwa kila aliyealikwa. Huu nao ni upuuzi uliovuka mipaka unaotumika kuwahadaa watanzania maskini.

 

Rushwa 

Serikali ya CCM imekuwa na wimbo mzuri usemao “rushwa adui wa haki,” lakini ndio kinara wa kuendekeza rushwa kama mtaji wake mkubwa kisiasa. Nape Nnauye, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM ni miongoni mwa miamba ya rushwa iliyoibuka katika kura za maoni za chama hicho. Ni wazi kwamba huwezi ukaitenganisha rushwa na CCM. Viongozi wake ndio hawa akina Nape na wengine waliokuwa wakinyukana kwa ushupavu wa kugawa rushwa. Watanzania tusikubali upuuzi huu! Viongozi wanaopatikana kwa rushwa ni wachovu, hawafai kamwe.

Watanzania kukubali kuwaajiri viongozi wanaogawa rushwa, tena Sh. 3,000/- na 10,000/- kwa mtu mmoja ni kukumbatia upuuzi mtupu ambao unawadidimiza kwa miaka mingi. Kama anayetaka uongozi anahoja za msingi, kwa nini atoe rushwa? Hii ndio CCM ya sasa ya akina Mwenyekiti, Jakaya Kikwete. Ushindi bila rushwa haiwekani!

Ubabe na kutojitambua kwa wananchi

Tangu Chama Cha Mapinduzi kipoteze dira kama ilivyo kwa serikali zingine zilizoanguka kwa kishindo duniani kwa kuendekeza ubabe na kutojitambua kwa wananchi wake bado kina ndoto hizo. Ubabe wa kutegemea vyombo vya dola kuwatala wananchi una kikomo chake, kwani wapinzani wanaposhika madaraka hawaji na majeshi yao wala idara zao za ujasusi au usalama wa taifa.

Hatupaswi kudanganywa katika hili. Mapambano ya kujinasua katika makucha ya wakoloni wazawa ndani ya nchi zao, dhidi ya wananchi wao yanapata ushindi kwa kuleta mabadiliko ya kweli ya mfumo wa kiutawala. Tunamtaka mtu ama watu watakaotukwamu katika dimbwi zito la umaskini huu ndani ya nchi yetu tajiri yenye rasilimali lukuki.

Tatizo tuna viongozi wanaougua ugonjwa uvivu wa kufikiri hivyo wanapaswa kusaidiwa kwa kupumzishwa ili waingie wengine wenye nia ya dhati ya kuwakwamua watanzania kwenye dimbwi la umaskini.

1556 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!