C4.+Nape+akihamasisha+kwenye+mkutano+huo,+Kushoto+ni+Mlezi+wa+mkoa+wa+Dar,+Abdulrahman+Kinanahama Cha Mapinduzi (CCM) kimepokea malalamiko mengi juu ya ukiukwaji wa taratibu na kanuni kabla na wakati wa kura za maoni, hivyo sasa vikao vizito vya chama vinatarajiwa kufyeka wagombea watakaotiwa hatiani.

 CCM ina utaratibu wa kukata majina ya makada wake wanaoshutumiwa kutoa rushwa na kufanya vurugu baada ya taarifa kufikishwa ofisi ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana iliyoko mkoani Dodoma.

Miongoni mwa madai hayo ni mizengwe iliyotokea Jimbo la Msalala mkoani Shinyanga baada ya mbunge anayemaliza muda wake, Ezekiel Maige, kudaiwa kucheza rafu dhidi ya wapinzani wake. Maige amekatiwa rufaa ofisi ya CCM Wilaya ya Kahama na Mkoa wa Shinyanga.

Kutokana na mizengwe hiyo, tayari baadhi ya wapinzani hao wameanza kumshutumu Maige kwa kudaiwa kukata rufaa kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Kahama yaliyompatia ushindi Ezekiel Maige.

Habari zilizoifikia JAMHURI zinapasha kwamba mmoja wa wagombea aliyepeleka malalamiko hayo ndani ya CCM ngazi ya wilaya na mkoa ni John Tuli Sukili, ambaye anaelezwa kuwa hasimu mkubwa kisiasa wa Maige.

  Vyanzo vya habari kutoka jimboni humo vimeidokeza JAMHURI kwamba mgombea huyo, ambaye ameshika nafasi ya pili, alikata rufaa hiyo kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Kahama kupinga ushindi wa Maige, Agosti 3, mwaka huu.

  Kwa mujibu wa vyanzo hivyo vya habari, katika rufaa yake, mgombea huyo anadaiwa kulalamikia mwenendo mzima wa upigaji kura za maoni ndani ya CCM, ambao umedaiwa kugubikwa na vitendo vya rushwa ya wazi kulikofanywa na Maige kupitia wapambe wake.

Habari zinaeleza kwamba Maige kupitia wapambe wake, alifanya vitendo vya kifisadi kwa kudaiwa kutoa rushwa za waziwazi kwa wapiga kura usiku kucha, na miongoni mwa maeneo yanayodaiwa kutumika kama sehemu za kugawia rushwa hizo ni ofisi ya chama ya Jumuiya ya Vijana.

“Ndugu mwandishi, naomba nikueleze kwamba vitendo hivi vilifanyika waziwazi na Mwenyekiti wa Vijana wa Wilaya ya Kahama, Solomon Mataba, aliyetumika kwa kiasi kikubwa kugawa fedha kwa wajumbe ili kufanikisha ushindi wa Maige na ushahidi wa hilo upo wazi,” kimeeleza chanzo hicho cha habari.

Kwa mujibu wa habari, Mwenyekiti huyo wa CCM Wilaya alionekana eneo la Kakola Agosti moja, mwaka huu, akigawa fedha kwa wapiga kura, jambo ambalo ni kinyume na utaratibu ndani ya sheria za chama na nchi.

Suala jingine walilolilalamikia ambalo wanachama hao wakereketwa wanaomuunga mkono mgombea namba mbili, ni jambo zima la upigaji kura za maoni kutokuwapo kwa picha za wagombea, badala yake wametumia majina. Jambo hili liliwachanganya wajumbe waliopiga kura ambao pamoja na mambo mengine walilazimishwa pia kumpigia kura Maige.

Mizengwe mingine inayodaiwa kufanywa na Maige ni kushawishi mmoja wa wagombea, Werema Lukumba, kujitoa kuwania nafasi hiyo naye akafanya hivyo na taarifa za kujiondoa kwake zilijulikana Julai 21, mwaka huu, lakini cha ajabu siku ya kupiga kura hizo za maoni kwenye karatasi za kupigia kura, jina la mgombea huyo lilionekana.

“Baada ya kupatikana taarifa za kujiondoa kwa mgombea huyo, tuliona kwamba hashiriki katika kampeni ndani ya chama lakini cha ajabu siku ya kupiga kura jina lake lilionekana katika karatasi za kura na kufanya idadi ya wagombea kufika saba,” kimeeleza chanzo hicho cha habari.

Madai mengine ambayo JAMHURI imedokezwa kuharibu uchaguzi huo ni kwa wasimamizi wa uchaguzi wakiongozwa na Mataba wakisaidiana na katibu wa mbunge anayemaliza muda wake, Maige, aitwaye Lutego, kuwa mstari wa mbele kugawa fedha waziwazi.

Jambo jingine lililolalamikiwa na mashabiki wa kisiasa wa Sukili ni wanachama wengi wasiokuwa na kadi kupiga kura kwa kukatiwa kadi zenye mfumo wa BVR peke yake, na jambo hilo limedaiwa kutokea katika kata za Segese na Chela.

JAMHURI ilipomtafuta mgombea anayedaiwa kupinga matokeo hayo kuthibitisha suala hilo, alikiri kufanya hivyo lakini alikataa kuzungumza chochote kuhusu rufaa aliyoiwasilisha kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Kahama kupinga matokeo hayo ya kura za maoni.

“Ni kweli nimepinga matokeo yaliyompa ushindi Maige lakini siwezi kuzungumza jambo hili kwenye vyombo vya habari kwa sababu kanuni za chama haziniruhusu kufanya hivyo,” amesema Sukili na kukata simu.

Jimbo la Msalala ni miongoni mwa majimbo mengi nchini yanayodaiwa kucheza rafu kwa kuhonga wajumbe wakati wa kura za maoni.

Baadhi ya majimbo yanayodaiwa kulalamikiwa ni Kilindi lililokuwa likiongozwa na mbunge anayemaliza muda wake Beatrice Shulukindo, Jimbo la Segerea lililokuwa likiongozwa na Makongoro Mahanga ambaye baada ya kutopitishwa kwenye kura za maoni amekihama chama chake na kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Mbali ya Jimbo la Msalala, ‘madudu’ mengine yaliyojitokeza katika Jimbo jipya la Itilima (zamani Bariadi Mashariki). Tayari baadhi ya wagombea walioshiriki hatua ya kura ya maoni wanadai kuwa taratibu, kanuni na maadili vilikiukwa.

Katibu Mkuu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, amesema, “Tutafanyia kazi madai na malalamiko yote yaliyowasilishwa,” yakiwamo madai ya Njalu Daudi Silanga anayedaiwa kucheza rafu wakati wa kampeni na upigwaji kura za maoni huko Itilima.

Inadaiwa kuwa wakati wa kampeni, Silanga alikodisha watu wawili waliochukua fomu kwa gharama wakijifanya kuwa ni zao ilhali walipewa na mgombea huyo kuonesha dhana ya kukubali, kitu ambacho si kweli.

Wanaodaiwa kukodishwa kufanya kazi hiyo ni Hillu Kubilu na Kulwa Subi ambao, mbali ya kumchukulia fomu Silanga, walitumika kutukana makada wengine wakibezwa viwango vya elimu zao za juu ikilinganishwa naye ambaye ni mhitimu wa shule ya msingi tu. Hata hivyo, makada hao – Kubilu na Subi – wamekana tuhuma hizo walipohojiwa na gazeti hili.  

Taarifa zinasema kwamba Silanga alikuwa akiwatumia vijana hao kutangulia kwenye mikutano ya kampeni ambako walikodi vijana wenzake kwa kuwanunulia pombe kali aina ya viroba na chakula kwenye migahawa ili anaposimama mgombea huyo awe anashangiliwa. Anadaiwa kufanya hivyo kwenye kata za Mwamapala, Nkoma na Mwalushu.

Hata hivyo, Silanga akizungumza na gazeti jana alisema, “Kama mimi na wasaidizi wangu uliowataja Hillu Kubilu na Kulwa Subi tungekuwa tumetoa hiyo rushwa si ningekamatwa na Takukuru? Jamani watu zaidi ya 44,000 unaweza kuwahonga?” anahoji Silanga aliyezungumza kwa niaba ya wasaidizi wake na kuendelea: “Kuhonga watu hao ningetoa shilingi ngapi kwa kila mmoja? Sijahonga kushinda kura za maoni.”

Taarifa hizo zinasema kwamba siku ya kupiga kura, Agosti mosi, mwaka huu viongozi wa ngazi ya matawi (mwenyekiti na katibu) kila mmoja alipewa Sh 100,000 na Silanga ambaye pia aligawa Sh. 10,000 kwa kila mjumbe wa kamati ya siasa ili wamtangaze mshindi.

Taarifa zinasema kwamba kura zilipigwa usiku wa kuamkia siku ya kupiga kura ambako mawakala walipofika usiku, walikuta masanduku yamejaa karatasi za kupigwa kura na walipohoji walifukuzwa na wengine kupewa fedha ili kuyakubali. 

Inaelezwa kuwa kwa mawakala waliobaki, kila mmoja alipewa Sh 20,000 kabla ya matokeo kupangwa katika kata za Sawida, Mbita na Mwaswale.

2680 Total Views 2 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!