Ukisikia mtu mwenye mkosi katika maisha ya siasa basi ni mimi Mzee Zuzu, ninayeishi huku Kipatimo. Naishi maisha magumu sana tangu nchi hii ilipopata Uhuru hadi imekomaa kwa Uhuru wake.

Nimepigana usiku na mchana tangu nikiwa barobaro hadi naingia utu uzima, na sasa machweo ya uzee sijabahatika kuwa hata mjumbe wa nyumba kumi, alimaarufu balozi huku kijijini kwetu.

Nimewaza mambo mengi ikiwamo kwenda kwa waganga wa kienyeji kuosha nyota yangu, lakini sijafanya hivyo kwa kumhofu Mwenyezi Mungu, nimewaza kuuza rasilimali zangu za kimaskini ili nipate fedha kwa ajili ya kuwahonga wajumbe na wapigakura nikaona huo ndiyo mwanzo wa kufa na presha kabla ya siku zangu.

Nimejuta na mengi kwa kipindi chote cha kutumia haki yangu ya kupiga kura, lakini pia nimeendelea kujuta na mengi kwa haki yangu ya kukosa kupigiwa kura kama mwananchi halali wa Tanzania huru yenye demokrasia. Bado nimewaza mengi kwanini ndoto zangu hazitimii katika ulingo wa siasa, na sasa sina nguvu tena ya kumuua tembo kwa ubua, kuche kuchele.

Nimejuta na mengi, kwanza nilidhani nilikuwa nakosa nafasi kwa sababu ya mfumo wa chama kimoja cha siasa, lakini ukaja mfumo wa vyama vingi, hali imekuwa ileile na tete zaidi. Tukiwa katika uteuzi wa viongozi wa ngazi mbalimbali, naambiwa sifa zangu hazitoshi, hata kuwa mjumbe wa mtaa, vigezo na masharti vimekuwa vikiniengua kila uchao, naendelea kujuta.

Nimejitathmini na kujipima kwa muda mrefu, nikajiuliza maswali mengi yanayohusu suala la uongozi nikaona sasa ni vyema nikaangalia ustaarabu mwingine wa maisha.

Nikaona hakuna mjadala kwamba kwa kipindi changu cha maisha kilichobakia siwezi tena kuwa kiongozi, sina mtu wa kumuongoza, kila mtu ni mwerevu, kila mtu ana mipango yake ya maisha, kila mtu anajali la mbele yake, kila mtu anahitaji fedha ili apigiwe kura, kila mtu ana mtu wake isipokuwa mimi Mzee Zuzu.

Sasa nimeamua kuacha kuwa mwanasiasa, nimeamua kuacha kugombea nafasi yoyote ya uongozi hata ndani ya nyumba yangu, sitaki hata kugombea uongozi katika ngazi ya kaya kwa kuhofia kutotosha katika vigezo vya uongozi, najaribu kufikiria uwezo wangu wa fedha na ushawishi.

Nafikiria kazi ya kufanya, nimepewa ushauri na watu wengi sana. Wapo waliosema niwe mpambe wa viongozi wanaogombea, huko nimearifiwa kuwa kuna posho ya kutosha, maisha yangu naweza kuyamalizia vizuri. Wapo walionishauri niendeleze mila kwa kuwa mganga wa asili na mtabiri, wapo walionishauri nianzishe chama changu cha siasa na niwe mgombea binafsi bila kukinzana na mtu.

Wapo walionishauri nishike upya jembe la mkono kwa kuwa sera zilizopo ni kumwinua mkulima, lakini ndiyo ziko katika mchakato, ushauri huo pia naufanyia kazi. Wapo walionishauri niende katika vyama vya kijamii kwenda kuomba hifadhi ya maisha yangu yaliyosalia, wapo wanaonibeza kwa kunishauri niende katika hifadhi ya majumba ya wazee na watoto yatima kwa kuwa sasa sina nguvu tena.

Yote ni mawazo ambayo nimepewa na kwa kweli yamenivuruga na nisijue nifanye lipi na niache lipi. Nikiangalia sababu kubwa ya mtafaruku huu katika kichwa changu zinatokana na kuvurugwa na siasa, kujifanya najua kumbe sijui, kujifanya mwanasiasa kumbe kuna watu wanajua nadandia siasa, kujifanya mwaminifu kumbe wapo wanaonijua kuwa mimi sitoshi.

Kuna maneno ambayo nilikuwa nasikia kuwa siasa ni mchezo mchafu, sitaki kuamini mpaka nithibitishe kuwa ni mchezo mchafu, sitakuamini mpaka nitakapogundua kuwa nachezewa shere, sitaki kuamini mpaka nitakapojiridhisha kuwaona viongozi wa kisiasa wakilalamika juu ya kudanganywa na kuenguliwa kama mimi. Kwa ufupi sitaki kuamini nikiwa ndani ya mfumo nataka niyaone nikiwa nje ya mfumo.

Najua wapo watakaonirubuni nirudi katika siasa, napenda kuwataarifu kuwa mimi sitaki tena, najua sitakiwi kwa sababu sitoshi, najua wapo watakaonifuata ili wapate ulua kwa kunihadaa; napenda niseme wazi kuwa mimi sina hela ya kumpa mtu kwa kunisifu.

Nakaribisha mawazo kutoka kwenu lakini yasiwe ya siasa. Sitaki kuwa king’ang’anizi – sikupata nikiwa barobaro leo hainisaidii kabisa sina nguvu tena, nipeni mawazo nifanye nini, nianze kulima, niwe mganga wa asili, niwe mshauri, au niwe mpambe?

 

Wasaalamu

Mzee Zuzu

Kipatimo.

1851 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!