Binadamu awe mtu mmoja mmoja, kundi la watu au jamii fulani  wanapenda mabadiliko lakini wanahofia mabadiliko yenyewe yatakuwaje. Muasisi au waasisi wa mabadiliko huwa na wasiwasi kuhusu hayo wayatakayo kama yatafaulu au laa.Kwa sababu hawana uhakika na matokeo yake.

Watu wanapotaka mabadiliko lazima wapwe na sababu za msingi na makini za kutaka mabadiliko. Siyo kwa sababu tu wafanye hivyo kwa vile wanahamu au ushabiki wa kuwa na mabadiliko kama mtindo mpya wa kuishi au kwa sababu wenzao katika familia, kundi, jumuiya au taifa fulani waliwahi kufanya hivyo na wakafanikiwa.

Kuiga matendo kama hayo si mabadiliko ni mfano na maigizo ya kuwa na mabadiliko. Ukweli hayatatoa malengo ya kuwa na mabadiliko. Ni vyema ikaeleweka kwamba mabadiliko ni mageuzi ni mapinduzi yanashabihiana. Hivyo watu hawana budi kuwa makini na waangalifu katika kutaka mabailiko.

“Mapinduzi ni mabadiliko ya haraka katika jamii, mabadiliko ambayo yanawanyang’anya wachache madaraka waliyokuwa wakiyatumia kwa manufaa yao na kuyaweka madaraka hayo mikononi mwa walio wengi ili kuendeleza masilahi yao.” ( ibara ya 2, Mwongozo wa TANU, 1971).

Napenda kukumbusha kwamba Chama cho chote cha siasa madhumuni makuu yake ni kushika dola. Vyama vingi vya siasa vinapoanzishwa ndani ya jamii,  ndoto za viongozi wake ni kutaka kutawala. Kwa mantiki hiyo viongozi hufanya kila hila na mbinu na wao wapate kuongoza na kutawala.

Siku zote taratibu za kutaka kushika dola ndizo zinazogomba kwa sababu kila kundi au Chama huchagua njia yake ya kuking’oa chama kilichopo madarakani kiwe kinafanya vizuri au vibaya, lazima kiondolewe. Lengo ni viongozi kutaka kutimiza masilahi yao. Wakati wa mchakato huo viongozi hao hutumia mbinu na hoja zenye maneno matamu ya kuwavutia wananchi wawakubali kama ni viongozi watakao leta mabadiliko.

Wakati mwingine mbinu kama hizo hushindwa. Viongozi huanzisha  mapigano ya wananchi ya wenyewe kwa wenyewe, au uvamizi kwa kufanya mambo kwa pupa na ghafla; au mageuzi kwa kuleta mabadiliko ya kijamii ya kisiasa, kitamaduni na kiuchumi; au mapinduzi ya kuwaondoa madarakani viongozi wa serikali kwa kutumia nguvu ambazo hutafasiriwa ni mabailiko ya haraka. Mwenyezi Mungu atuepushe na balaa hilo. Inshallah!

Leo, Watanzania tunashuhudia vyama vya siasa nchini vinavyoshughulika usiku na mchana kutaka kuking’oa Chama Cha Mapinduzi madarakani kwa sababu kimekaa muda mrefu na kimeshindwa kuondoa maadui ujinga, maradhi na umasikini na badala yake kimelea rushwa na ufisadi.Ndivyo vinavyodai.

Watanzania jambo la kuzingatia ni mabadiliko yepi tunayoyataka. Tusibabaishwe na baadhi ya viongozi wetu kwani tumepata kuwasikia katika mikutano yao ya hadhara wakisema kuwa mabadiliko ni lazima na polisi wetu wametakiwa wawapishe! Aidha, wamewaita wataalamu kutoka ughaibuni kuja nchini kufanya utafiti kuona mtu gani mwenye sifa ya kukubalika na kupendwa na watanzania. Mtu mwenye sifa hizo ndiye turufu ya kupiku madaraka yaliyopo.

Tunasahau wataalamu hao ndiyo walewale wanaopora na kula mali zetu. Ni wale waliotunyonya na kutunyanyasa kwa muda mrefu. Leo wanataka tena tuondoe serikali iliyomadarakani wapate nafasi ya kuendelea kutunyonya kiurahisi kupitia vibaraka wao. Tuwe waangalifu na makini na KITO cha fedha kilichopakwa rangi ya dhahabu, tukakiona ni dhahabu.

Vyama hivyo vya upinzani vipatavyo 21 baadhi yao kila kimoja kinajigamba na kujitapa pindi kipatapo ridhaa ya Watanzania ya kushika dola wataondoa umasikini na kujenga Tanzania huru na mpya itakayoleta maendeleo chanya kwa watanzania.

Ukweli maendeleo ya nchi yapo ukilinganisha na huko tulikotoka mwaka1961 (Tanganyika) na mwaka 1964 (Zanzibar) kuanzia kwenye ustawi wa jamii, elimu, afya, maji safi, barabara n.k. hadi hapa tulipo. Mfano mzuri ni ongezeko la watu kutoka milioni 9 mwaka 1961 hadi kufikia milioni 47 mwaka 2012. Kama afya ingekuwa mgogoro idadi hiyo isingepatikana.

Watanzania wanapotaka mabadiliko maana yake nini? Kweli ni kutaka vyama vya siasa virumbane katika kishika dola hata kama hakuna hoja za kukifu haja? Ni kweli wanataka kuona viongozi wanavyobadili vyama na kauli zao mithili ya mnyama kinyonga katika mazingira fulani? Hapana! Hapana hata kidogo!

Jibu kuntu linatolewa na Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipozungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu y Taifa ya Chama Cha Mapinduzi, mjini Dodoma mwaka 1995, alisema, nanukuu

Teuweni mgombea ambaye atakidhi matarajio ya wananchi. Acha matarajio yako wewe mpiga kura. Tupeni mgombea ambaye atakidhi matarajio ya Watanzania. Watanzania wanataka mabadiliko. Wasipoyaona wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM.

Watanzania wamechoka na rushwa. Nchi yetu bado masikini, Chama cha kimasikini si chama cha matajiri. Wafanyakazi na Wakulima ni masikini. Udini na ukabila ni mambo ya hovyo.

Tunataka nchi yetu itoe kiongozi safi. Kiongozi safi hawezi kutoka nje ya CCM. Nyinyi wapiga kura mnaweza kutupatia kiongozi safi kwa kura zenu. Basi tupatieni kiongozi safi kwa kura zenu.” mwisho wa kunukuu.

Nimenukuu maneno hayo machache kukupa kama bashraf. Uangalie yasemwayo na yatendwayo na viongozi. Wetu yanaoana au yanakinzana na falsafa ya Mwalimu Nyerere. Tafakari.

By Jamhuri