Kama unahitajika ushahidi kuwa upo umuhimu wa kuruhusiwa kwa wagombea huru ndani ya Katiba ya Tanzania, basi umejitokeza sasa baada ya matukio ya hivi karibuni yaliyomo ndani ya siasa za Tanzania.

Tukio lililohitimisha ukweli huo ushahidi ni kuhama kwa Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Kwa maelezo yake, amehama kutoka CCM kwenda CHADEMA kwa sababu “…mchakato wa kuteua wagombea uligubikwa na mizengwe, ukiukwaji wa maadili, uvunjifu wa Katiba, na taratibu za uchaguzi ndani ya CCM.”

Aliendelea kusema: “Zaidi ya hayo uchaguzi ulisimamiwa kwa upendeleo zaidi na chuki iliyokithiri dhidi yangu.” Kilichotokea Dodoma, kwa mujibu wa maelezo yake, ni kubaka demokrasia.

Amehamia CHADEMA akiamini kuwa yale yaliyomkuta ndani ya CCM hayawezi kutokea ndani ya CHADEMA. Na dalili ni nzuri kwake mpaka sasa kwa sababu CHADEMA hawakuchukuwa muda mrefu na walimpa nafasi ya kugombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, nafasi ambayo CCM haikumpa. Hatimaye amepitishwa kuwa ni mgombea urais wa muungano wa vyama vya siasa vinavyojulikana kama UKAWA.

Mwalimu Nyerere amenukuliwa na Lowassa akitamka kuwa CCM siyo baba yake [Mzee Nyerere Burito], wala mama yake [Mugaya wa Nyang’ombe] na kuwa akikosa mabadiliko ndani ya chama hicho, basi atayatafuta nje ya chama hicho. Mheshimiwa Lowassa amekosa mabadiliko ndani ya CCM na anaamini atayapata ndani ya CHADEMA na UKAWA. Swali ambalo halijaulizwa ni hili: asiyeona mabadiliko ndani na nje ya CCM anakuwa mtoto wa nani?

 Kwangu mimi haipo sababu ya msingi ya kuwapo yatima wa kisiasa nchini. Jawabu ni kuwapo kwa mfumo wa kikatiba unaoruhusu wagombea huru kama nguzo ya tatu kwenye siasa. Wagombea huru watatoa fursa kwa wanachama waliokosa macho ya kuona na masikio ya kusikia fursa za mabadiliko zilizomo ndani ya chama tawala na ndani ya vyama vya upinzani kutafuta mabadiliko hayo kwingineko kama wagombea huru, au kama watetezi wa wagombea huru.

 Kuna mengi ambayo mtu anaweza kuunga mkono ndani ya sera za vyama tofauti vya siasa, lakini akawa pia hakubaliani na kipengele cha sera kwenye vyama hivyo hivyo. Aidha, kuna uamuzi ambao unaweza kupitishwa na chama anachokiunga mkono ambao hauwaafiki. 

Mtu wa aina hii anapaswa kupewa fursa ya kikatiba ya kupenyeza mawazo yake bila kulazimika kuchukua uamuzi ambao tunausikia kwa baadhi ya watu wa kustaafu siasa au kuachia wadhifa wake ndani ya chama cha siasa, kwa sababu tu haoni chama ambacho kinawakilisha matakwa yake kwa wakati huo.

 Kinadharia, chama kinachotawala au chama cha upinzani kinachobaini hali hiyo kitatambua ukomo wa kile ambacho mimi naita ‘jeuri ya chama’, au uhakika wa chama cha siasa kuwa kile kinachoidhinishwa na uamuzi rasmi au usio rasmi wa chama ndiyo mwisho wa mjadala na kufungwa kwa kikao. Mfumo wa wagombea huru unaweza kuwa kama sehemu ya mwisho ya kukata rufaa kwa wananchi kwa sababu hiyo ya uwepo wa kukinzana kwa mitazamo baina ya mtu na mienendo ya chama alichokiunga mkono.

 Woga mkubwa wa washiriki wa siasa za siku hizi ni kushindwa uchaguzi, siyo kung’ang’ania misimamo ambayo nyakati hizi imeitwa imepitwa na wakati.

 Kwenye nadharia ya siasa chama cha siasa kinapaswa kuwa tayari kushindwa kwenye uchaguzi kwa sababu kinaamini kwa dhati juu ya misimamo mbalimbali ambayo kimekuwa kikiunga mkono kwa mujibu wa sera zake. 

Kwenye miaka ya mwanzo baada ya Tanganyika kupata uhuru, Mwalimu Nyerere, akiwa waziri mkuu wa wakati ule, alipingana na baadhi ya wawakilishi wa chama cha TANU bungeni na wa Serikali yake, ambao wakati wa kujadili muswada wa uraia wa Tanganyika walidai kuwa uraia wa Tanganyika uwe haki ya Watanganyika wenye ngozi nyeusi tu. 

Katika kupinga msimamo wa wenzake na akiwa anatetea hoja kuwa kila Mtanganyika anayo haki ya kuwa raia bila kubaguliwa kwa rangi ya ngozi yake, Mwalimu Nyerere alisema kuwa Serikali yake itakuwa tayari kushindwa kwenye kura bungeni na kuondoshwa madarakani lakini haiwezi kukiuka misingi ya haki na usawa ambayo yenyewe iliipigania na kuitetea.

 Leo hii ndani ya siasa tunashuhudia kuwa misimamo ni kama mashati ambayo hubadilishwa kwa mujibu wa mahitaji yanayojitokeza.

 Kwa mtazamo wangu, vyama vyote vya siasa vinaweka mikakati ya kufika Ikulu tu, kwa kushinda Uchaguzi Mkuu ujao. Kwa CCM ni kupigana kufa na kupona kuhakikisha kuwa Edward Lowassa hawi rais wa tano wa Tanzania.

 Kwa UKAWA hali hii ni dhahiri kuliko kwa CCM. Hatutarajii kuwa jambo rahisi kwa vyama vinne vya siasa kukubaliana kwa yote yaliyomo kwenye sera zao. Itakuwa “Rais wetu akishaapishwa tutajua la kufanya.”

 Ukweli haupingiki kuwa lipo pengo ndani ya siasa ambalo linalazimisha sehemu fulani ya wapiga kura ya Watanzania kuwapo kwenye siasa za vyama ambazo haziwakilishi kikamilifu matakwa yao. Suluhisho ni wagombea huru. Hawatamaliza hitilafu zilizopo lakini watazipunguza kwa kiasi kikubwa.

1872 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!