CCM yashinda udiwani Kigoma Ujiji

Msimamizi wa uchaguzi Mwantumu Mgonja (katikati) akitangaza matokeo ya udiwani Kata ya Kasingirima

Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Kigoma

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeshinda kiti cha udiwani katika Kata ya Kasingirima Manispaa ya Kigoma Ujiji, baada ya mgombea wa chama hicho Mlekwa Mfamao Kigeni kuibuka mshindi kwenye uchaguzi mdogo wa udiwani kwenye kata hiyo uliofanyika Machi 20,2024.

Msimamizi wa uchaguzi huo, Mwantumu Mgonja kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi alimtangaza Mlekwa Kigeni  wa CCM aliyeibuka mshindi baada ya kupata kura 437, huku minzani wake wa karibu  Ahamad Alumbula  wa ACT Wazalendo akipata kura 233. Vyama 12 vilisimamisha wagombea, ambapo vyama hivyo vingine hakuna mgombea aliyepita kura zaidi ya 10.

Diwani mpya wa wa Kata ya Kasingirima Kigoma Ujiji mkoani Kigoma, Mlekwa Kigeni akizungumza baada ya kutangazwa matokeo (Picha zote na Fadhil Abdallah). 

Msimamizi huyo wa uchaguzi amesema wapiga kura  713 walijitokeza katika uchaguzi huo, kati ya wapiga kura 1960 walioandikishwa, ambapo kura halali zilikuwa 699 na kura 14 zilikataliwa.

Uchaguzi huo mdogo umefanyika kufuatia kujiuzulu kwa aliyekuwa diwani wa kata hiyo, Abdallah Kiembe aliyepata ajira ya serikali katika halmashauri ya Kondoa mkoani Dodoma.