Na Andrew Chale, JamhuriMedia, Dar

SHIRIKA la Utamaduni la Maendeleo Afrika Mashariki (CDEA) linaendesha mradi wa mafunzo maalum kwa Vijana wanamuziki wanaochipukia wa Mkoa wa Dar es Salaam, kwa ufadhiri Braid Arts and Culture Fund, ambao watawawezesha Vijana hao kujifunza aina mbalimbali za uandishi wa muziki wa jukwaani, na mikogo ya kufanya maonesho ya jukwaani (techniques on stage performance).

Akizungumza meneja mradi wa ubunifu wa CDEA, Angela Kilusungu amesema kuwa, mradi huo unahusisha vijana watano ambao wameweza kunufaika na Midundo Online radio kwa kazi zao kuchezwa kwenye radio hiyo.

“Vijana hawa wamepatikana kupitia kazi zao ambazo zimeweza kuchezwa katika Midundo Online Radio, ambapo wameweza kupata nafasi ya kuhojiwa katika vipindi mbali mbali na kupewa fursa ya kushiriki mafunzo.

Ambapo vijana hao Wakike wawili na Wakiume watatu na watakuwa kwenye mafunzo kwa muda wa miezi mitatu, kwa kufundishwa kwa vitendo, lakini pia kuandaa namna mbalimbali ya ujuzi katika kile walicho jifunza ikiwemo kuandaa wimbo maalum ambao utafanyika na mkufunzi wao.

Katika mafunzo hayo, Bi, Angela Kilusungu amesema vijana hao wapo chini ya gwiji wa muziki mkongwe John Kitime ‘Anko Kitime’ ambaye anawanoa kwa muda wa wiki moja na kisha kufanya nao mazoezi maalum ya wimbo watakaoshirikiana nao kaundaa.

Aidha, Vijana hawa wataendelea kusimamiwa na CDEA katika shughuli zao kimuziki kwa kutafutiwa nafasi ndani ya Afrika Mashariki kwenye majukwaa ya Sanaa na Utamaduni.

Mradi huo wa uwezeshaji Vijana katika muziki wa moja kwa moja (Live performance) ni wa kwanza kufanyika chini ya CDEA ambapo unatarajiwa kuwa wa manufaa makubwa kwa vijana Tanzania wenye umri wa miaka 18 hadi 35,kwani unaenda kuinua Vijana hao wanaochipukia kuwa katika kiwango cha juu na cha kimataifa katika sanaa yao ya muziki wa jukwaani.

CDEA imekuwa ikijihusisha na miradi mbalimbali ya Sanaa na Utamaduni ikiwemo Atamizi ya Sanaa bunifu(Creative Economy Incubator) ambayo hutoa mafunzo ya fani na biashara kwa wabunifu mbalimbali wakiwemo ; Wabunifu mavazi, filamu, pamoja na muziki kupitia radio ya taasisi hiyo ya Midundo Online Radio.

By Jamhuri