CHADEMA Lindi kushiriki mapokezi ya Lissu

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mkoa wa Lindi kimepanga kushiriki mapokezi ya makamu mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho upande wa Tanzania bara,Tundu Lissu. 

Hayo yameelezwa leo Januari 20,2023 na Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Lindi, Zainabu Lipalapi wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Lindi. 

Lipalapi amesema Mkoa wa Lindi ni miongoni mwa mkoa ambao utashiriki kwani halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea ina idadi kubwa ya madiwani wa chama hicho kuliko halmashauri zote hapa nchini. Kwahiyo ni lazima washiriki mapokezi hayo. 

“Katika halmashauri ya wilaya ya Nachingwea ambayo katika Mkoa wa Lindi kuna madiwani takribani saba waliopitia tiketi ya chama chetu.Hakuna halmashauri yenye idadi kubwa ya madiwani wa CHADEMA kuliko Nachingwea.Kwa maana hiyo Lindi ni miongoni mwa ngome za CHADEMA,” amesema Lipalapi. 

Mwenyekiti huyo amesema kila wilaya itapeleka wawakilishi katika mapokezi hayo yanayotarajiwa kuwa ya aina yake. Ambapo wilaya ya Lindi pekee itawakilishwa na wanachama 20. 

Mbali na hayo Lipalapi amemsifu, kumpongeza na kumshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kufanyika maridhiano ya 1111 imani ya hadhara ya vyama vya siasa. 

Amesema Rais Dkt.Samia, anatakiwa kupongezwa na kuungwa mkono na kila mpenda amani, demokrasia na mshikamano.Huku akiweka wazi kurejea kwa Lissu na wenzake nchini ni matokeo ya nia njema ya Rais ya kutaka umoja na mshikamano bila kujali tofauti za itikadi za vyama vya siasa.

Tundu Lissu na wenzake, Godbless Lema na Hezekia Wenje waliokimbilia ughaibuni wanatarajiwa kurejea nchini Januari 26, mwaka huu.