Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Zanzibar

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Rais wa Mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi kilichotokea Februari 29, 2024 jijini Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa leo Machi 1, 2024 na Naibu Katibu Mkuu Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu imeeleza kuwa Mwinyi atakumbukwa kwa namna alivyosimamia mageuzi ya sera za kiuchumi za   na kuruhusu mifumo ya uhuru wa soko.

“Chadema inaungana na Watanzania kuomboleza msiba huu wa kitaifa. Aidha, chama kinatoa pole kwa Mheshimiwa Dk Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, wajane wa marehemu, familia, ndugu, jamaa na marafiki” imeeleza taarifa hiyo.

Chama hicho kimesema kinaungana na Watanzania wote katika kuomboleza msiba huo na kuenzi mchango wa Mwinyi katika utumishi wake.

Aidha, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe ataongoza ujumbe wa Chadema katika maziko yaliyopangwa kufanyika kesho Mjini Unguja.

By Jamhuri