Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila leo Septemba 26,2023 amekutana na wakandarasi wanaosafisha mito katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo, Wenyeviti wa mitaa, wasafishaji wadogo wa mito na wachimbaji wa madini mchanga, wataalam wa bonde na Kikosi kazi kinachoratibu usafi wa mito na utunzaji wa mazingira ndani ya mkoa.

RC Chalamila amekutana na wadau hao pamoja na wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa halmashauri zote za Mkoa huo ikiwa ni muendelezo wa Serikali ya mkoa huo kujipanga au kufanya maandalizi ya kukabiliana na mvua kali za EL-Nino ambazo zimetabiliwa kunyesha katika Kipindi cha hivi karibuni kwa mujibu wa utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa ( TMA ).

Mkuu wa Mkoa katika kikao hicho alipata wasaa wa kuwasikiliza wadau hao namna wanavyotekeleza majukumu yao maoni na ushauri wao ambao ulionyesha sura nzima ya nini kinafanyika na Changamoto wanazokutana nazo wakandarasi wanaosafisha mito wanaotumia na machepe katika usafishaji huo.

Aidha RC Chalamila baada ya kuwasikiliza wadau hao ametoa maagizo yafuatayo ikiwemo Kikosi kazi pamoja na miongozo iliyoko ya usafishaji mito iboreshwe, kupitia upya uongozi ulioko wa wakandarasi, kikosi kazi kurudi tena kuangalia malalamiko ya wadau yana hoja, kupitia muda wa utoaji vibali vya mikataba, Wenyeviti wa mitaa watengeneze fursa za ajira kwa vijana katika mitaa yao, hatua dhidi ya uchimbaji holela zichukuliwe na Viongozi katika Wilaya zote, baadhi ya wakandarasi kuacha mara moja kuzoa mchanga badala ya kusafisha mito.

Kwa upande wa wadau mazingira pamoja na wenyeviti wa Serikali za Mitaa wamemuhakikishia Mkuu wa Mkoa kupokea maagizo yake yenye tija katika pande zote ili kuweza kuboresha mfumo mzima wa Utendaji kazi na usimamizi mzuri wa usafishaji mito kwa masilahi mapana ya watu na kupambana na athari zinazotokana na uharibifu wa mazingira hususani katika mito iliyoko ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam.

By Jamhuri