Na Waandishi Wetu

Nia ya uchambuzi huu ni kutoa ushauri kwa watu, hususan Wakristo, katika suala la kujikinga na Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19). 

Tunajua ugonjwa huu ni hatari na umeua watu wengi duniani kwa kipindi kifupi. Ni janga la dunia linalogusa kila familia kiafya, kiuchumi, kijamii na kiroho. Hivyo, ni muhimu Wakristo kuwa mstari wa mbele kujikinga na kuzuia maambukizi dhidi ya UVIKO – 19 kwa sababu zifuatazo:

Kwanza, katika kipindi hiki cha mlipuko wa UVIKO-19, kumekuwa na nadharia nyingi potofu zinazosababisha watu kuamini kwamba ugonjwa huu si wa kweli, kwamba hakuna janga la dunia (pandemic denialism), ugonjwa huu umetengenezwa, barakoa zimewekewa vimelea vya ugonjwa, mashine za kusaidia kupumua (ventilators) zinaua watu, chanjo hazifai na mambo mengine mengi yanayoshangaza. 

Kwa bahati mbaya, tetesi na nadharia potofu zimeshika kasi pengine kuliko habari sahihi na za kweli kuhusu ugonjwa huu na kinga zake. Nyingine zimechukua taswira ya kiroho, na kusababisha Wakristo wengi kuchanganyikiwa, wakikataa tahadhari za kinga, hasa chanjo. 

Nafasi ya kanisa ni kueleza ukweli juu ya afya na hatua za kisayansi. Hii ni sehemu ya Injili ambayo kanisa limeihubiri kwa muda mrefu kupitia hospitali zake.

Pili, Wakristo hufanya shughuli za ibada makanisani mahali ambapo kuna mikusanyiko ya watu wakiimba, kusali na kushirikiana kwa ukaribu. 

Kama pasipokuwa na tahadhari madhubuti, ibada zinaweza kuwa hatari kubwa sana ya kusambaza ugonjwa huu, na kusababisha watu kuugua na kupoteza maisha, labda bila hata wahusika kufahamu sehemu walikopatia maambukizi.

Tatu, tangu mwanzo wa janga hili hadi hivi karibuni, viongozi wa Kikristo (Kanisa Katoliki, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri, Kanisa la Waadventista Wasabato na Assemblies of God) wamekuwa wakitoa nyaraka mbalimbali kuwaasa waumini kuchukua tahadhari. Nyaraka hizo zimesaidia sana kupunguza maambukizi yaliyokuwa yanaongezeka kwa watu kutochukua tahadhari.

Watu huthamini sana miongozo ya kichungaji inayotoka kwa walezi wa kiroho pengine kuliko hata ile inayotoka kwa viongozi wengine wa jamii. Lakini kwenye suala la chanjo, viongozi wengi wamechelea kutoa mwongozo bayana kwa waumini na wengine wamefikia hata kuwaelekeza waumini wao kukataa chanjo. 

Makala hii inalenga kuzungumza  na Mkristo wa kawaida kuelimisha kuhusu njia za kujikinga na ugonjwa huu, na kujadili wajibu wa kila Mkristo katika kupambana na kuutokomeza kabisa ugonjwa ambao umeisumbua dunia kwa zaidi ya miezi 18 sasa.

Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19)

Ugonjwa huu husababishwa na virusi vya korona. Kwa kitaalamu vinaitwa Severe Acute Respiratory Syndrome Coronavirus 2 (SARS-Cov2), yaani aina ya pili ya virusi vya korona vinavyosababisha homa kali ya mapafu.

Ugonjwa huu umesambaa kwa kasi sana katika nchi zote, hivyo kuwa janga la ulimwengu (pandemic). Hadi tunapoandika uchambuzi huu (Septemba 12, 2021), duniani kuna visa vya maambukizi vilivyohakikishwa zaidi ya milioni 219 na vifo zaidi ya milioni 4.6!

Takwimu hizi ni za chini sana (underestimate) kwa sababu kuna watu wengi wanaugua na wanakufa kwa ugonjwa huu bila kupimwa au kutolewa taarifa kwenye vyombo husika na kuna nchi zisizotoa taarifa za ugonjwa huu au zimeshindwa kutoa taarifa sahihi. 

Mfano, nchini Afrika Kusini, kwa mwaka 2020 kulikuwa na vifo vya ziada 70,000 kwa sababu zote zinazobabisha vifo ikilinganishwa na wastani wa miaka mitano iliyopita, wakati vifo vilivotajwa kuwa vya korona vilikuwa 28,469 tu. Hii ina maana kwa namna moja au nyingine, korona imechangia ongezeko hilo la vifo.

Janga la UVIKO-19 ni kubwa sana kuliko lile la SARS-Cov lililoanzia China mwaka 2003 na kusambaa nchi 26 (vifo 774) na janga la Middle East Respiratory Syndrome (MERS-Cov) lililoanzia Uarabuni mwaka 2012 na kusambaa nchi 27 (vifo 858).

UVIKO-19 husambaa kwa njia kuu tatu:- Kwanza, kwa kugusa au kushika sehemu zenye maambukizi. Pili, matone yatokayo kwenye kinywa kwa kupiga chafya, kukohoa, kuongea au kuimba na tatu njia ya hewani kama mvuke (aerosols) kutoka kwenye mapafu ya muathirika ambayo hutokea sana wakati wa kupumua, kuongea au kuimba (kuimba hutoa ‘aerosols’ zaidi ya kuongea kawaida).

Mvuke huu ambao unaweza kubeba virusi vya korona hukaa hewani kwa muda mrefu kama hakuna mzunguko mzuri wa hewa, kama ambavyo moshi wa sigara huweza kudumu chumbani kwa mvutaji kwa muda mrefu kama madirisha yamefungwa. 

Njia hii kwa kitaalamu huitwa ‘airborne transmission’, yaani maambukizi ya hewani, na ingawa haijaongelewa sana kwenye vyombo mbalimbali Tanzania, ndiyo njia kubwa zaidi ya nyingine zote ya kuenea kwa ugonjwa huu katika mkusanyiko wa watu, au matukio ya halaiki (super-spreader events). 

Njia kuu za kujikinga zilizothibitishwa kisayansi ni:

 1. i. Kunawa mikono mara kwa mara kwa maji-tiririka na sabuni – kupunguza maambukizi kwa njia ya kugusa.
 2. ii. Kuvaa barakoa kwenye mkusanyiko wa watu – kupunguza maambukizi kwa njia ya matone na hewani (airborne). 
 3. iii. Kuepuka misongamano ya watu – kupunguza maambukizi ya hewani (airborne). Ikibidi kukutanika inashauriwa: 
  1. a) Kuacha nafasi kati ya mtu na mtu (kama mita 2). 
  2. b) Kukutana nje kwenye mzunguko mzuri wa hewa (kama ni ndani, basi milango na madirisha viwe wazi) – ili kupunguza maambukizi ya hewani. 
  3. c) Kupunguza muda wa kukutanika.
  4. d) Kama kuna mtu ana dalili za maambukizi kama kukohoa, homa na mafua, inashauriwa asije kundini siku hiyo, kwa sababu uwezekano wa kuambukiza wengine kwa njia ya hewani ni mkubwa sana.
  5. e) Kuvaa barakoa.
 4. iv. Kupata chanjo ambazo zimethibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).
 5. v. Chanjo hizi hupunguza uwezekano wa kupata, kueneza maambukizi ya virusi na muhimu zaidi, huzuia kupata ugonjwa mkali na vifo vitokanavyo na UVIKO-19. 
 6. vi. Ushahidi wa kisayansi juu ya ufanisi wa chanjo ni mkubwa sana kiasi kwamba tuna wajibu wa kulifikiria suala la chanjo kwa makini sana kama Wakristo.

Kutokana na maelezo hayo hapo juu, sisi kama Wakristo na wanazuoni, tunapenda kuainisha kwa maelezo sababu 10 za kwanini ni muhimu kila Mkristo kupata chanjo. 

 1. 1. Chanjo zinaokoa maisha

Kwa zaidi ya mwaka sasa, Wakristo kote ulimwenguni wamekuwa wakifanya maombi rasmi mara nyingi Mungu atoe suluhisho la janga la UVIKO-19. Chanjo nyingi zilianza kufanyiwa utafiti na baadhi kuthibitishwa kuwa na ufanisi wa kuzuia ugonjwa huu. 

Upatikanaji wa chanjo bora na salama, ndani ya muda mfupi sana katika historia ya utengenezaji wa kinga ya magonjwa ya mlipuko, umeonekana na wengi kuwa kama ‘muujiza wa kisayansi’. 

Hadi sasa kuna chanjo 29 zilizoidhinishwa na nchi mbalimbali. Lakini ni saba tu zimeidhinishwa na WHP na kuwekwa kwenye mpango wa COVAX, ulioanzishwa kusaidia nchi maskini kupata chanjo kwa gharama nafuu. Chanjo hizo ni:

 1. 1. Pfizer/BioNtech (BNT162) 
 2. 2. Moderna (mRNA-1273)
 3. 3. Oxford/Astrazeneca (AZD1222)
 4. 4. Covishield (Oxford/AstraZeneca inayotengenezwa India)
 5. 5. Johnson & Johnson (Ad26.COV2.S)
 6. 6. Sinopharm (BBIBP-CorV)
 7. 7. Sinovac (CoronaVac)

Chanjo hizi zimeonyesha ufanisi wa hali ya juu sana katika kuzuia ugonjwa mkali na vifo. Ufanisi hupimwa kwa njia kuu mbili:

 1. (i) Utafiti wa Majaribio ya Kitabibu (Randomised Controlled Trial [RCT]) – huthibitisha ufanisi wa kitafiti (efficacy). Matokeo ya majaribio hayo husababisha chanjo kuidhinishwa kama ikionekana ni salama na ina ufanisi. Kwa kuwa mazingira ya majaribio mara nyingi hayafanani sana na mazingira ya maisha ya kawaida, huwa ni vema kuendelea kufuatilia utendaji kazi wa chanjo baada ya kuidhinishwa.
 1. (ii) Utafiti Halisia (Real-World Study) – huangalia ufanyaji kazi wa chanjo kwa kuzifuatilia baada ya kuidhinishwa kwa ajili ya matumizi. Kama katika mazingira ya kawaida chanjo huonekana zinafanya kazi vizuri, basi ufanisi hubadilishwa jina na kuitwa ‘ufanisi halisia’ (effectiveness). Ufanisi halisia huthibitisha utendaji kazi wa chanjo, maana utafiti wa aina hii umefuatilia chanjo zilivyofanya kwenye maisha ya kawaida. 

Pamoja na kwamba chanjo hizo saba zimeonyesha ufanisi wa hali ya juu katika utafiti wa majaribio ya kitabibu zilizosababisha kuidhinishwa kwa matumizi, baadhi ya nchi zimefanya utafiti halisia wakati wa matumizi na chanjo hizo zimeonyesha tena ufanisi halisia wa hali ya juu sana. 

Nchi hizi ni Uingereza (Pfizer na Oxford/Astrazeneca), Israeli (Pfizer), Marekani (Pfizer, Moderna na Johnson & Johnson), na Bahrain (Sinopharm, Pfizer, Oxford Astrazeneca na Sputnik).

Baada ya kuja kwa aina mpya ya kirusi cha korona kiitwacho delta (Mei 11, 2021), ufanisi wa chanjo dhidi ya maambukizi ulionekana kupungua kidogo, lakini bado chanjo zimeonekana kuwa thabiti katika kuzuia ugonjwa mkali, kulazwa na vifo vitokanavyo na delta.

Kwa mfano, hivi karibuni nchini Afrika Kusini chanjo ya Johnson & Johnson imeonekana kuwa na ufanisi mkubwa katika kukabiliana na delta pamoja na aina nyingine za kirusi cha korona.

 1. 2. Chanjo ni jibu la maombi kwa Mungu kutukinga na UVIKO-19

Chanjo za korona zilizoidhinishwa na WHO si za ‘majaribio’ bali zimethibitishwa kuokoa maisha ya watu wengi sehemu mbalimbali duniani. 

Kwa mfano, ufuatiliaji wa karibu wa takwimu za afya ya jamii nchini Uingereza, unaonyesha hadi juma linaloishia Agosti 26, 2021, mwitikio wa chanjo umekadiriwa kuzuia ugonjwa mkali na kulazwa (hospitalisation) kwa watu 143,000; na kuepusha vifo vya watu kati ya 102,500 na 109,500.

Tukiangalia matokeo haya kwa jicho la Kikristo, hatuachi kustajaabia kazi kubwa ambayo Mungu ameifanya kwenye kipindi kifupi sana kupitia wahudumu wa afya na wanasayansi; ya kuokoa maisha ya watu wengi waliokuwa wakifa, kwa mamia na maelfu kila siku.

Wakristo kukosa mwelekeo bayana na chanya kuhusu chanjo, inamaanisha kwamba hatutambui kazi kubwa ambayo Mungu tayari amekwisha kuifanya kujibu maombi ya watu wake dunia nzima, waliomlilia usiku na mchana, kuomba suluhisho la ugonjwa huu.

Pia inatukumbusha enzi zile za Agano la Kale, wakati Musa alivyomsimamisha nyoka wa shaba jangwani:

Watu wakaenda kwa Musa wakamwambia: “Tumetenda dhambi kwa sababu tumemnung’unikia Mungu na wewe. Mwombe Mungu atuondolee hawa nyoka.” Kwa hiyo Musa akawaombea watu. BWANA akamwambia Musa: “Tengeneza nyoka na umweke kwenye nguzo. Na itakuwa kila anayeumwa, akimwangalia huyo nyoka atapona.” Kwa hiyo Musa akatengeneza nyoka wa shaba naye akamweka juu ya nguzo. Na kila mtu alipoumwa na nyoka na kumwangalia huyo nyoka alipona.’ (Hesabu 21:7-9).

Ni maombi yetu kwamba Wakristo wengi wasikatae chanjo na kuangamia kwa kukosa elimu ya chanjo au maarifa yatakayowasaidia kufanya uamuzi sahihi. Ni maoni yetu kwamba, viongozi wa makanisa mbalimbali wangetamka waziwazi kuwashauri waumini wapate chanjo kwa ajili ya kujikinga wao binafsi, na kuwakinga wengine dhidi ya UVIKO-19.

 1. 3. Kila Mkristo ana wajibu wa kujilinda na kulinda afya za wengine

Ingawa dawa na afua (interventions) za kiafya (pamoja na chanjo) huwa ni hiari ya mtu, chanjo ni tofauti na afua nyingine za afya kwa sababu ina faida mbili.Kwanza, kutoa kinga binafsi kwa yule aliyechanjwa. Pili, kutoa kinga ya jumla kwenye jamii (community immunity/herd immunity).

Faida hiyo ya pili ni ya muhimu zaidi kuliko ya kwanza. Hii ni kwa sababu ndiyo inasaidia kutokomeza janga la magonjwa yanayozuilika kwa chanjo. Ingawa kupata chanjo ni hiari, matokeo ya kupata au kutopata chanjo, yanaathiri jamii nzima, ama kwa faida au kwa hasara.

Mtu anayekubali chanjo, huwa amechangia kuleta kinga ya jamii. Anayekataa chanjo, ingawa hajachangia kinga ya jamii, hufaidika kwa uamuzi wa yule aliyekubali chanjo. Lakini watu wengi wakikataa chanjo, basi wanapunguza au kuzuia jamii kwa ujumla kufaidika na kinga. Kadiri watu wengi zaidi wanavyochanjwa ndivyo jamii inavyopata kinga ya jumla.

Chanjo hupunguza sana uwezekano wa kupata au kusambaza maambukizi ya korona. Kwa mfano, chanjo iliyopo nchini Tanzania sasa hivi ya Johnson & Johnson, imeonyesha uwezo wa kupunguza uwezekano wa maambukizi kwa asilimia 76.7. 

Ina maana bado kuna uwezekano asilimia 23.3 wa kupata na kueneza maambukizi, uwezekano ambao ni mdogo na wa muda mfupi sana, kwa sababu wanaopata maambukizi baada ya kuwa na kinga kamili ya chanjo (breakthrough infections) huugua kidogo na kwa muda mfupi tu (siku kama 3-4). 

Asiyepata chanjo, na bila kuchukua tahadhari yoyote, huwa na uwezekano mkubwa (asilimia 100) wa kupata na kueneza maambukizi kwa watu wengine, hata kama yeye binafsi hana dalili yoyote – huweza kueneza maambukizi kwa muda wa siku 10 au zaidi.

Kwa maana hiyo, mtu aliyekataa chanjo anaweza kupata maambukizi kwa urahisi sana na kuyasambaza kwa wengine. Kwenye ibada, kama kuna mtu mmoja mwenye virusi vya korona, na mtu mwingine mwenye udhaifu (vulnerable) na wote hawajapata chanjo, wala hawajavaa barakoa, ni rahisi sana kueneza maambukizi na kusababisha mtu kuugua ugonjwa mkali, na hata kufa kwa UVIKO-19, ugonjwa ambao kwa sehemu kubwa unazuilika. 

Ingawa chanjo hazipunguzi maambukizi kwa asilimia 100, afua zote za kinga zikichukuliwa kwa pamoja – yaani chanjo pamoja na barakoa, kukaa mbalimbali, kupunguza muda wa mkusanyiko na kunawa mikono mara kwa mara; – uwezekano wa maambukizi hupunguzwa kwa kiasi kikubwa sana. 

Mambo mengine yasiyozuilika au tusiyoyajua, hudhibitiwa na Mungu mwenyewe ambaye tumeshamuomba. Lakini Mungu anatutegemea sisi tujipatie maarifa na kutenda yaliyo sahihi katika uwezo wetu aliotupatia, kwa kumtii na kumpenda yeye, ikidhihirishwa na jinsi ambavyo tunawatendea binadamu wengine – kwa kuwajali na kuwakinga.

Mwanafunzi Mpendwa wa Yesu alilitambua hilo alipoandika ujumbe huu:

Mpenzi wangu, nakutakia mafanikio mema ya kila aina; nakutakia afya njema 

ya mwili kama ulivyo nayo rohoni.’ (1 Yohana 3: 1)

 1. 4. Kupata chanjo ni kutenda haki, kusambaza upendo na kujenga amani

Neno la Mungu na Injili ya Yesu Kristo inasisitiza kupenda na kutoa haki. Tunaelezwa kuwa ufalme wa Mungu ni haki, amani na upendo. Mambo haya matatu yanategemeana. Haki huimarisha amani na upendo. 

Kazi kuu ya Ukristo ni kujenga ufalme wa Mungu na tunajenga ufalme huu kwa kutenda matendo ya haki, amani na upendo. 

Haki inaanza na kuwajibika (angalia sababu ya pili hapo juu) kwa uamuzi wako binafsi ambao una athari kwako mwenyewe, unamuathiri mwingine au kuathiri jamii kwa ujumla. 

Kwa kuwa chanjo haikulindi wewe tu bali pia jamii nzima, ni muhimu kwa kila Mkristo kupata chanjo kama tendo la haki kwenye jamii. 

Aidha, chanjo ni ishara ya upendo, maana ni tendo la kujali wengine. Kama Wakristo, tunausiwa kumpenda jirani yetu. Bwana Yesu Kristo anasema: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.”

Hivyo, ingawa chanjo ni hiari, Mkristo ana jukumu la kufanya uamuzi unaozingatia upendo. Tena Bwana Yesu anatuambia hiyo ni moja ya amri kuu. 

Tukitafakari hili kwa kina tunaona umuhimu wa Mkristo kupata chanjo. Chanjo inajenga amani kwa kuwa ugonjwa wa UVIKO-19 ni hatarishi kwa usalama wa dunia, pia kwa watu binafsi. 

Kwa muda mfupi, watu wengi duniani na nchini Tanzania wamekufa kwa ugonjwa huu kuliko waliokufa kwa vita au machafuko ya kisiasa. Hivyo, tuko kwenye vita ambayo suluhisho lake ni amani. Chanjo ni njia mojawapo fanisi zinazoweza kuleta amani katika jamii. Hivyo, Mkristo akipata chanjo, ametenda haki, kujenga upendo na kusambaza amani.

Kwa kuwa kuna viongozi wa kiimani wamepinga chanjo kama suala la kiroho, ni muhimu Wakristo waelimishwe kuhusu umuhimu wa chanjo kwa kuangalia Injili ya Kristo na mafunzo ya kweli yanayozingatia neno la Mungu na kazi ya kanisa duniani. 

 1. 5. Kupata chanjo ni tendo la imani

Wakristo wengine wanafikiria kwamba kukataa chanjo ya UVIKO-19 kunaonyesha jinsi imani yao ilivyothabiti kwa Mungu. 

Wanaofikiria hivyo wangekuwa katika nafasi ya Yesu kwenye kinara cha hekalu, wangeepuka kutumia ngazi kushuka chini na kuamua kujitupa chini ili kuthibitisha kwamba kweli wanaamini ahadi za Mungu. 

Lakini hiyo si imani, bali ni uzushi (presumption) – ni kile Yesu alichokiita ‘kumjaribu Mungu’:

‘Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mji mtakatifu, akamweka juu ya kinara cha hekalu, akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua; Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe. Yesu akamwambia, Tena imeandikwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako’ (Mathayo 4: 5-7)

Ni wakati gani kumtumaini Mungu kunakuwa kumjaribu Mungu? Mtu anapochukua hatua zinazomweka katika hatari ili amlazimishe Mungu amwokoe. Tuepuke uongo wa Ibilisi. Imani ya kweli hudhihirishwa kwa matendo mema. Yakobo anauliza:

‘Ndugu zangu, yafaa nini, mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je, ile imani yaweza kumwokoa?’ (Yakobo 2:14)

Kisha Yakobo anajibu:

‘Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake. Lakini mtu atasema, Wewe unayo imani, nami ninayo matendo. Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu.’ (Yakobo 2:17-18)

Hivyo basi, imani yetu ituhamasishe kuchukua hatua sahihi. Mungu anao uwezo wa kutubariki bila sisi kufanya chochote, lakini Biblia inakemea uvivu. Vivyo hivyo, Mungu anaweza kutulinda bila chanjo, lakini ni wajibu wetu kuchanjwa. 

Kuchanjwa ni udhihirisho wa imani yetu katika vitendo. Hii ndiyo aina ya imani inayotunusuru. Na ndiyo maana wale wanaochanjwa wengi wapo salama. 

 1. 6. Chanjo za UVIKO-19 zilizoidhinishwa ni salama

Kuna tetesi nyingi za uzushi zinazokuza madhara ya chanjo za UVIKO-19 ili kuficha ukweli na kukatisha watu tamaa wasipate chanjo. Ukweli ni kwamba kwa watu wengi sana, chanjo hazina madhara makubwa isipokuwa maudhi madogo madogo, kitu ambacho ni cha kawaida kwa dawa na chanjo nyingine. 

Maudhi ya chanjo ni kama kuumwa kichwa, homa, uchovu wa mwili, na mahali palipochomwa sindano kuuma – na kwa kawaida, yote haya huisha ndani ya siku mbili tu. Kwa watu wengi, maudhi yanaweza yasijitokeze kabisa.

Madhara makubwa ya chanjo ni ya nadra sana, na hutokea ndani ya mwezi mmoja, na uwezekano wa kutokea ni mdogo kuliko uwezekano wa kupata ajali ya gari. 

Kwa mfano, mtu mmoja miongoni mwa 2,900,000 waliopata chanjo ya Johnson & Johnson anaweza kufa kwa tatizo la kuganda damu kutokana na chanjo hiyo. Uwiano huu ni mdogo sana ukilinganishwa na uwezekano wa kufa kwa ajali ya gari. 

Kwa Tanzania, takwimu za mwaka 2019 zinaonyesha kuwa takriban watu watatu kwa kila Watanzania 100,000 wamo kwenye hatari ya kufa kwa ajali za barabani.

Nchini Uingereza kila mwaka mtu mmoja miongoni mwa 20,000, yumo kwenye nafasi ya kufa kwa ajali ya gari. Hata hivyo, pamoja na hayo hakuna mtu anayesita kupanda gari!

Zaidi ya hapo, aliyekataa chanjo akipata UVIKO-19, ana uwezekano mkubwa (asilimia 30-70) wa damu kuganda kwa sababu ya korona. Kwa kifupi, uwezekano wa kuganda damu au kufa kutokana na chanjo ni mdogo sana na nadra ukilinganisha na uwezekano wa kuganda damu kutokana na maambukizi ya UVIKO-19 kwa mtu ambaye hajapata chanjo.

Wakristo wengi wakielimishwa, wataridhia kuvumilia maudhi madogo madogo ili kuchangia ile faida kubwa ya kinga ya jamii, ambayo inaweza kuokoa maisha ya wengi. 

Ingawa chanjo ni hiari, kama inavyoainishwa na Serikali ya Tanzania, kwa Wakristo, Yesu aliagiza wema wa wafuasi wake uwe zaidi ya ule wa waandishi na Mafarisayo (Mathayo 5:20). 

Kama Mkristo mmoja anayo fursa ya kutenda mema kwa jamii, kuokoa maisha ya wengi kwa gharama ndogo sana binafsi (maudhi madogo madogo ya chanjo), basi kwetu Wakristo, fursa hiyo inatakiwa tuichukulie kama wajibu. 

Hivyo, msukumo (motivation) wa chanjo kwa Mkristo, si sahihi kuishia tu kwenye kujifikiria faida yake binafsi au afya yake mwenyewe, bali pia kama dhamira ya kujali mchango wake kusaidia afya ya jamii kwa ujumla wake.

 1. 7. Kukataa chanjo huchangia kudorora kwa tahadhari nyingine

Kukataa aina moja ya kinga, huchangia kuzorota kwa tahadhari nyingine. Kwa mfano, wakati viongozi wa makanisa waliposisitiza kuhusu kuchukua tahadhari, waumini wengi walisikiliza na kutii. Walipoacha kusisitiza na kupuuza uwepo wa ugonjwa, au walipolikalia kimya suala la chanjo, waaumini nao waliacha kuchukua tahadhari nyingine. 

Ukipata fursa ya kutembelea makanisa mengi utaona kwamba hata utaratibu wa kuvaa barakoa wakati wa ibada umeachwa na kwingine hata maji tiririka na sabuni kwa ajili ya kunawa mikono hakuna.

Sayansi inaonyesha kukiwa na mkusanyiko wa watu ndani ya jengo, pasipo na mzunguko mzuri wa hewa, watu wakiongea au wakiimba bila kuvaa barakoa, hushirikiana hewa inayopumuliwa (shared respiratory air with expired aerosols). 

Kama wote hawajavaa barakoa, hatari ya maambukizi huwa ni kubwa. Kukiwa na hatari kubwa ya maambukizi inamaanisha kwamba kama mtu mmoja tu ana virusi vya korona (hata bila kuwa na dalili), maambukizi huweza kutokea kwa vile vimelea vya kirusi huyu hudumu angani kwenye hiyo hewa wanayoshiriki kwa muda mrefu.

Iwapo kwenye mkusanyiko huo kuna mtu mmoja tu mwenye udhaifu kiafya (vulnerable person), madhara ya maambukizi yatakuwa makubwa.

Hivyo, ingefaa Wakristo tuwe na mwelekeo chanya kuhusu kinga zote zilizothibitishwa (zikiwamo chanjo dhidi ya UVIKO-19). Kufanya hivi kutasaidia sehemu za ibada zisiwe sehemu za kusambaza magonjwa na kusababisha vifo.

 1. 8. Kufa kwa sababu ya kutojikinga kwa makusudi si mapenzi ya Mungu

Mojawapo kati ya ujumbe mkuu kutoka kwa wachungaji na Wakristo wengi wakati wa misiba, ikiwa ni pamoja na inayosababishwa na korona, ni kwamba mapenzi ya Mungu yametimia. 

Kwa upande mmoja inafariji kujua kwamba aliyefariki dunia alikuwa amekaa vizuri na Mungu. Pia tunakubali kabisa kwamba mapenzi ya Mungu hukamilika kwa njia mbalimbali. 

Lakini usemi wa ‘mapenzi ya Mungu’ unaweza kusababisha watu kuacha kuwajibika kwa kuchukua tahadhari, au kwa kutathmini mambo yaliyosababisha mtu kupata maambukizi. 

Kwa upande mwingine, ukizungumzia kuhusu matendo ya binadamu yaliyosababisha mtu fulani kuugua na kuzidiwa hata kufa, mara nyingi hukatizwa na sauti zinazosema: “Acha tu, maana yote hayo ni mapenzi ya Mungu.” Hivyo, kunakuwa na utamaduni unaojijenga wa kutotathmini matendo yetu na kutumia ‘mapenzi ya Mungu’ kama kisingizio cha kuficha kutowajibika kwetu.

Tunaamini yanaweza kuwa mapenzi ya Mungu kwa mtu kufa, lakini kwamba ni kifo gani kinamkuta mtu, hasa kwa sababu zitokanazo na afya, hilo limo mikononi mwetu. 

Ni wajibu wetu kutenda haki na yaliyo mema kwa nguvu zetu zote, akili zetu zote na moyo wetu wote, na ikiwa mtu amefariki dunia, tunaweza kuwa na amani mioyoni mwetu, tukijua kwamba tumefanya wajibu wetu, na yaliyotokea ni mapenzi tu ya Mungu, kwani hatujachangia kwenye kuleta ugonjwa au kifo. 

Ni vema nafsi zetu zisituhukumu kwa hilo ili tuwe na ujasiri mbele ya Mungu. Kwa maana imeandikwa:

‘Watoto wadogo, tusipende kwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli. Katika hili tutafahamu ya kwamba tu wa kweli, nasi tutaituliza mioyo yetu mbele zake, ikiwa mioyo yetu inatuhukumu; kwa maana Mungu ni mkuu kuliko mioyo yetu naye anajua yote. Wapenzi, mioyo yetu isipotuhukumu, tuna ujasiri kwa Mungu; na lolote tuombalo, tunalipokea kwake, kwa kuwa tunazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake’ (1 Yohana: 3 18-22)

Kama tumechangia katika kueneza maambukizi na Mkristo akaugua na kufa, itaondoa ujasiri wa kusema kwamba yalikuwa ni mapenzi ya Mungu. Yesu alikuja ili tuwe na uzima, kisha tuwe nao tele. Anasema:

‘Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.’ (Yohana 10:10)

Tunachojaribu kusema ni kwamba kuna haja ya kuweka msisitizo mkubwa katika ibada zetu makanisani kwa kuwataka washirika/washiriki waache uzembe na kutokujali, badala yake wazingatie hatua zote za tahadhari kwa ajili ya kujikinga binafsi na kuwakinga wengine.

 1. 9. Maombi yanatakiwa kuambatana na kutii

Maombi ndiyo njia kuu tuliyopewa Wakristo kuwasilisha hoja zetu mbele za Mungu. Sambamba na maombi ni muhimu kusikiliza sauti ya Mungu inasema nini katika janga hili na kutii maagizo yake. Mara nyingi huwa tunaomba tukitegemea majibu fulani kama ilivyo mitazamo na matarajio yetu. 

Lakini Mungu hujibu zaidi ya matarajio, na kama Wakristo hatutakuwa makini, tunaweza kushindwa kutambua majibu ya maombi. 

Kwa mfano, tunaweza kumuomba Mungu pesa za kununua chakula, lakini Mungu anaweza kujibu kwa kutuletea chakula chenyewe, au tunaweza kumuomba Mungu chakula, lakini yeye akatupatia fursa ya kazi ya kufanya ili tupate kipato cha ziada kukutana na mahitaji.

Inawezekana tumemuomba Mungu ufumbuzi wa tatizo la UVIKO-19, na inawezekana tumepewa majibu kwa kupatikana chanjo, lakini kwa sababu sisi tunategemea muujiza wa aina nyingine, labda tunashindwa kufahamu jibu la Mungu linapokuja, hasa kama tunahitajika na sisi kufanya wajibu fulani. 

Kuna baadhi ya Wakristo wakishauriwa kupata chanjo wanasema kwamba wao wamekwisha kumuomba Mungu kuwalinda na ugonjwa huu. Hii inaonyesha baadhi ya Wakristo wamejikita kwenye theolojia ya ‘AU’. Yaani, maombi AU tahadhari, badala ya kufuata theolojia ya ‘PAMOJA NA’: Yaani maombi PAMOJA NA tahadhari. 

Mungu hufanya kazi kupitia sisi (Warumi 8:28). Hivyo kama tukiacha kushirikiana na Mungu, tutakuwa tunakwepa wajibu wetu kama Wakristo. 

Kwa sababu tayari tumepewa ufumbuzi mkubwa wa kisayansi kuhusu kupunguza maambukizi ya UVIKO-19, itakuwa ni vema Wakristo tukumbushane kuhusu maombi PAMOJA NA kuishi kwa hekima, tukitumia maarifa tuliyopewa na Mungu katika kuudhibiti ugonjwa huu. Mtume Paulo anasema:

“Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima; mkiukomboa wakati kwa maana nyakati hizi ni za uovu. Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana.” (Waefeso 5:15-17)

Kinachoendelea sasa miongoni mwa Wakristo ni kufanya maombi huku wakikataa chanjo au hata tahadhari nyingine. Tunapochagua silaha moja na kuacha nyingine (theolojia ya ‘AU’) inakuwa ni kujidhoofisha wenyewe. Kinga thabiti ya kuzuia maambukizi ya korona inatokana na kutumia silaha zote kwa pamoja, yaani maombi (uhitaji wa kinga na uponyaji vilivyo juu ya uwezo wetu) PAMOJA NA kuchukua tahadhari na kukubali chanjo (kinga zilizo ndani ya wezo wetu). 

 1. 10. Chanjo si Mpinga Kristo

Katika tetesi, dhana potofu na nadharia-njama (conspiracy theory) zilizojitokeza katika kipindi hiki cha korona, ni hofu iliyojengwa na vikundi fulani vya wahubiri, wakitishia Wakristo kwamba chanjo inawapa watu alama ya 666 ya ‘mnyama’ wa pili aliyeandikwa katika kitabu cha Ufunuo, Sura ya 13. 

Mnyama huyu wa pili au ‘Mpinga-Kristo’, anaelezwa kuwasababisha binadamu kumsujudia mnyama wa kwanza, kuwakosesha binadamu na kufanya ishara. Mnyama huyo anaelezewa zaidi:

“Naye awafanya wote, wadogo kwa wakubwa, na matajiri kwa maskini, na walio huru kwa watumwa, watiwe chapa katika mkono wao wa kuume, au katika vipaji vya nyuso zao; tena kwamba mtu awaye yote asiweze kununua wala kuuza, isipokuwa ana chapa ile, yaani, jina la mnyama yule, au hesabu ya jina lake. Hapa ndipo penye hekima. Yeye aliye na akili, na aihesabu hesabu ya mnyama huyo; maana ni hesabu ya kibinadamu. Na hesabu yake ni mia sita, sitini na sita.’ (Ufunuo 13:12-14)

Andiko hili liliandikwa na Yohana katika karne ya kwanza. Waliandikiwa Wakristo wa zamani wasikubaliane na tawala zinazopingana na Mungu. 

Na kwetu sisi Wakristo wa leo ujumbe wake wa kinabii kwetu unahusu tu mamlaka zilizopo na zijazo duniani zinazopingana na Mungu.Mamlaka inayosaidia raia wake kupata afya, au kujikinga na maradhi, haipingani na Mungu, kwa sababu uponyaji na afya hutoka kwa Mungu.

Tetesi kwamba chanjo ya kuzuia ugonjwa wa korona ndiyo alama ya mpinga Kristo, ni dhana potofu isiyoendana na tafsiri sahihi ya Neno la Mungu.

Hitimisho

Ni vema tukajikumbusha kuwa chanzo cha maarifa ni kumcha Mungu kama alivyoandika Mfalme mwenye hekima, Suleiman, katika Mithali 1:7 na Mungu aliwahi kusema watu wake “wanaangamia kwa kukosa maarifa.” (Hosea 4:6). Tumche Mungu na kutumia maarifa aliyotupatia kufanya uamuzi sahihi kuhusu chanjo.

Makala hii imeandikwa na wanazuoni waliobobea katika nyanja mbalimbali ambao ni Mwidimi Ndosi (PhD), Mhadhiri Mwandamizi Chuo Kikuu cha West of England; Aikande Kwayu (PhD), Mwanasayansi ya Jamii na Mwandishi; Chambi Chachage (PhD), Profesa Msaidizi Chuo Kikuu cha Carleton; Charles Makakala, Jr na Mathew Mndeme (PhD), Mtafiti na Hhadhiri, Idara ya Sayansi ya Kompyuta, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; na kuchapwa kwa idhini ya tovuti ya udadisi.com – MHARIRI.

369 Total Views 8 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!