Historia inazungumza mambo mazuri juu ya Afrika. Inaitaja Afrika kama chimbuko la maendeleo. Binadamu wa kwanza duniani anatajwa kuishi Afrika. Olduvai Gorge iliyopo Arusha nchini Tanzania, inatajwa kama eneo alikoishi binadamu wa kale zaidi ya miaka milioni mbili iliyopita.
Taifa la Misri ndilo chimbuko la maendeleo duniani. Herufi zinazotumika leo za kusoma na kuandika zilianzia Misri. Kuna ushahidi usiotiliwa shaka kuwa miaka 16,000 kabla ya Kristo, kando ya Mto Nile barani Afrika kulikuwapo shughuli za kilimo.
Zipo historia nyingi na za kuvutia. Afrika ina madini, maliasili, maji baridi na viumbe vya baharini, lakini kwa bahati mbaya hadi leo ndilo bara lenye mataifa masikini kuliko yote duniani. Kati ya nchi masikini na zenye madeni makubwa 39 duniani, nchi 33 zipo kusini mwa Jangwa la Sahara.
Sitanii, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanahusisha umasikini wa Afrika na mikasa inayoanzia kwenye utumwa, ukabaila, ubwenyenye, ukoloni mamboleo, na mfumo mpya wa vyama vingi uliokuja bila mwongozo. Kila anayeamka asubuhi anaanzisha chama akiwa na malengo binafsi.
Machi 14, mwaka huu, China wamemchagua Rais mpya, Xi Jinping, anayemrithi Rais Hu Jintao. China na Tanzania zimekuwa nchi rafiki tangu mwanzoni mwa miaka ya 1950 wakati waasisi wa nchi hizi, Mwalimu Julius Nyerere na Mwenyekiti Mao Tse Tung wa China wakiwa katika harakati za ukombozi.
Viongozi hawa walifungua milango ya udugu. Nimelazimika kuandika makala haya, baada ya kupata na kushuhudia taarifa za heshima ya aina yake tuliyopewa na Rais mpya wa China, Mheshimiwa Xi. Mheshimiwa huyu ameamua kuacha mataifa mengine yote na kuja Tanzania kama nchi ya kwanza kwa bara la Afrika.
Tanzania inakuwa nchi ya pili kutembelewa na Rais huyu baada ya Urusi, baada ya kutangazwa rasmi kuwa Rais wa China Machi 14. Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ameujulisha ulimwengu kuwa Rais Xi atatumia ujio huu kutangaza Sera ya China juu ya Afrika leo.
Sitanii, hii ni heshima kubwa iliyotupatia China. Nitafafanua ninachokifahamu kidiplomasia, na faida tunazotarajia kupata Watanzania kwa ujio huu wa Rais wa China. Hii ni neema. Tunapaswa kuikumbatia fursa hii na kuomba Mungu atupe moyo wa kujituma. Kabla sijaingia kwa undani, niiguse kidogo Afrika.
Afrika imeendelea kuwa bara masikini si kwa sababu watu wake ni wavivu, bali kutokana na mfumo ulioachwa na wakoloni. Mwanazuoni Mtanzania Shaaban Robert katika moja ya maandiko yake, alipata kuhoji iweje “Tuzalishe tusichokula na kula tusichozalisha?”
Hiki ndicho kifo cha Afrika. Tumeachwa yatima kitambo. Wakoloni waliondoka, lakini walituacha kwenye nchi hizi kama mashamba yao. Tunaamka alfajiri tunakwenda shambani, tunalima, tunapalilia, tunavuna na kuwapelekea mavuno mabwana wakubwa.
Hivi leo katika mfumo huu uliopo nani anaweza kula katani? Nani anaweza kubwia kahawa yote tunayozalisha. Nani anakunywa kakao inayopandikizwa kwa kasi. Korosho ndiyo zingekuwa na manufaa, lakini tulipojenga viwanda vya kubangua korosho wakasema wanahitaji korosho ghafi. Viwanda vikafa.
Wanatudanganya na misaada. Kila mwaka tunatangaziwa nyongeza ya misaada, lakini si fursa za biashara. Leo tungehamasishwa tangu enzi za Uhuru tukalima mahindi, mpunga, karanga, alizeti, ndizi, mtama na ulezi, kama hakupata soko tungekula wenyewe. Thubutu ugome kuuza kahawa uone utazifanyia nini!
Hata viwanda vya pamba Wazungu hawakutaka tuvimiliki. Kiwanda kama cha Urafiki kilichojengwa kwa msaada wa Kichina, wamefanya kila mbinu kikaelekea kufa. Badala ya kutuwezesha tutengeneze nyuzi, wanatutaka tuuze pamba nje na kununua nguo kutoka kwao. Hili ndilo chimbuko la umasikini.
Tanzania na Zambia zilipokuwa na shida ya kweli ya reli, Shirika la Fedha Duniani (IMF) lilikataa kutukopesha. Likasema mradi huo haukuwa kipaumbele kwa mataifa yetu. China kwa uungwana wakatujengea reli hii kama msaada. Wazungu waliposikia China inajenga Reli hii ya Uhuru, wakasema nao wako tayari kuijenga, Mwalimu Nyerere akakataa.
Mataifa ya Asia yanayosifiwa kwa maendeleo, Hong Kong, Korea Kusini, Singapore na Taiwan wameweza kukuza uchumi kwa asilimia 7 na zaidi kati ya miaka ya 1960 na 1990 mfululizo kwa sababu wamewezeshwa na mataifa yaliyoendelea.
Mataifa haya yamepewa fursa za masoko bila masharti. Hata walipopewa misaada walipewa misaada ya maana si sawa na hii tunayopewa visima vya maji na vyandarua inayolingana na kumwekea mgonjwa dripu ya maji. Waliongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi na wakapewa fursa ya kuwekeza katika elimu. Nchi hizi zimeweza kutoa elimu ya msingi kwa wote miaka ya 1970, huku Korea ya Kusini ikitoa elimu ya sekondari kwa wote ilipofika mwaka 1988.
Huku wakijua fika kuwa bila kuwekeza katika elimu hakuna maendeleo, miaka ya 1980 Afrika ikalazimishwa kuingia katika Mpango wa Marekebisho ya Uchumi (SAPs). Mpango huu ulikuja na mkakati wa uchangiaji wa huduma.
Tukaambiwa tuchangie katika elimu, afya, huduma za jamii na kupunguza wafanyakazi serikalini. Unawaambia wananchi waliokuwa wanalipwa mshahara kidogo ukawafukuza kazi, bila pato mbadala kuwa sasa wachangie gharama za elimu, matibabu na nyingine.
Kilichofuata ni kiama. Hadi SAPs zinaletwa Tanzania mwaka 1987 kiwango cha kujua kusoma na kuandika kilikuwa asilimia 94. Kufikia mwaka 2000 kiwango cha elimu kilikuwa kimeshuka hadi asilimia 40. Benki ya Dunia ikaingilia kati chini ya Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (PEDP).
Mwaka 1994 Mwalimu Nyerere alipata kuhojiwa na mwandishi mmoja wa vyombo vya Magharibi, akamuuliza ilikuwaje sera ya Ujamaa ikashindwa hasa upande wa elimu, naye akamjibu hivi: “Chini ya Ujamaa asilimia 94 ya wanafunzi walikuwa wanajua kusoma na kuandika, leo hali ni kinyume. Unaweza kuwa na maelezo bora ni zipi sera nzuri kati ya Ujamaa na hizi za kibepari.” Mwandishi alibaki kinywa wazi.
Sitanii, nchi zilizoendelea zimeweka mipango kama AGOA na EBA kwa nchi za Afrika kuuza kwenye masoko yao, lakini masharti yanayoambatana na mikataba hiyo ni sawa na kutuambia tusiende kuuza kwao. Wanaweka viwango ambavyo hata mbinguni havipo.
Kwa mfano, kahawa chini ya mpango wa ‘Organic Farming’, wanasema ikitokea mtu aliyepuliza dawa za wadudu kwenye shamba jingine akakatiza katikati ya shamba lako kabla hajaoga, kahawa yako inapoteza sifa ya kuwa organic. Sifa hii ni ya kupika. Ni kikwazo cha makusudi kutuzuia tusiingie katika masoko yao. China hawana ulaghai kama huu. Wakikupa fursa haiambatani na masharti.
Wazungu hawako tayari kuifundisha Afrika jinsi ya kuvua samaki, ila mara zote wako tayari kutununulia samaki. Hivi tutaendelea hivi hadi lini? Mwenyekiti Mao alipata kusema hivi: “Haijalishi paka ana rangi nyeusi au nyeupe, ilimradi akamate panya.”
Mao alikuwa akiwaamsha Waafrika katika usingizi. Alitaka kuwaeleza kuwa Waafrika waondokane na ulevi wa kudhani maendeleo lazima yaletwe na Wazungu. Mwalimu Nyerere alisema enzi za uhai wake kuwa “Huhitaji kuwa Mkomunisti kufahamu kuwa tunayo mengi ya kujifunza kutoka China.”
Dhana hii ya Mwalimu Nyerere inaungwa mkono na Rais wa Zimbabwe, Robert Gabriel Mugabe. Mugabe ana sera yake ya ‘Angalia Mashariki’. Anamaanisha kuwa nchi za Magharibi tayari zimeridhika na hazina la kuzisaidia nchi za Afrika. Kwani wanafikiria kutoa misaada zaidi kuliko biashara.
Nimeishi katika nchi za Ulaya. Ninaloweza kukujulisha nao wanaangalia Mashariki kwa sasa. Ndiyo maana Waziri wa Fedha wa Marekani, Jacob Lew, siku nne tu tangu Rais Xi alipotangazwa, alikwenda Beijing kupeleka salamu za pongezi za Rais Barrack Obama.
Leo China imeikopesha Marekani kuliko taifa jingine lolote duniani. Asilimia kubwa ya deni la taifa la Marekani wanadaiwa na China. China ina uchumi mkubwa wa pili duniani. Benki za China zinakopesha kwa riba ndogo na Wachina hawana longolongo. Ukikubaliwa mkopo leo unapata siku hiyo hiyo, bila kusubiri Wazungu wanachoita ‘No Objection’ inayotolewa baada ya miezi sita tangu siku ya uamuzi wa kukupa mkopo ulipofikiwa.
China sasa imekuja hapa kwetu. Inasema inataka kuwekeza. Kampuni kutoka China imedhamiria kujenga Bandari ya Bagamoyo. Hii itakuwa bandari ya Kizazi cha Nne. Itaweza kuhudumia makontena hadi 20,000 kwa mwaka. Bandari ya Dar es Salaam kwa sasa inahudumia kontena 800,000 kwa mwaka.
Wenye kujenga bandari hii wanajenga barabara mpya kutoka Bagamoyo hadi Chalinze. Wanaunganisha reli ya Tazara na Reli ya Kati kwenda Bagamoyo. Kuna mpango pia wa kuimarisha Reli ya Kati iweze kuzifikia nchi za Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Rwanda, Burundi, Zambia na Uganda.
Kwa sasa kampuni za China zimewekeza katika migodi huko Zambia, madini mbalimbali huko DRC, madini ya chuma hapa kwetu – Liganga na Mchuchuma, na wanauangalia kwa jicho zuri mgodi wa Nikeli Kabanga Ngara. Madini yote haya yanapaswa kusafirishwa nje ya nchi.
Sitanii, taarifa nilizopata Bagamoyo kwa kupitia mpango wa Ukanda Huru wa Biashara, wanapanga kujenga hadi viwanda vya kuunganisha na kuzalisha magari. Kampuni kadhaa za Japan zinasema uchumi wa dunia baada ya kuhama kutoka Ulaya ukaenda Amerika mwishoni mwa miaka ya 1800, umehama tena kutoka Amerika kwenda Asia mwishoni mwa miaka ya 1900 na kabla ya mwishoni mwa miaka ya 2000 utahamia Afrika.
Wameamua kuchukua nafasi mapema. Maelezo niliyopata uchumi wa China na Bara Asia sasa umekua na hivyo viwango vya maisha vimepanda. Kama ilivyotokea kwa Ulaya na Marekani, wanaona sehemu ya kuhamishia viwanda ni Afrika ambapo mishahara inayolipwa bado ni midogo na utaalamu unakua kwa kasi.
Tanzania imechaguliwa na mataifa mbalimbali kwa sababu kuu mbili za msingi. Moja ni asili ya kijiografia, ambapo inazungukwa na nchi nane na inapakana na Bahari ya Hindi. Mtaji mwingine ni umoja, amani na utulivu alioujenga Mwalimu Nyerere. Wanaona ni heri kuwekeza katika nchi yenye utangamano.
Jingine linalotajwa ni ugunduzi wa gesi asilia katika maeneo mbalimbali ya nchi hii. Gesi iliyogunduliwa ina uwezo wa kuzalisha umeme wa kutosha Afrika nzima kwa muda wa miaka 600 ijayo. Uwezekano wa kuzalisha umeme kwa njia ya maji nao bado upo. Hali kama hii ndiyo iliyoitajirisha Urusi.
Kuna madini ya kutosha na kwa bahati ya Mwenyezi Mungu Tanzania ni kitovu au katikati ya safari za kuelekea ncha zote za dunia. Hii inawapa uhakika kuwa kwa kuwekeza Tanzania wanaweza kusafirisha bidhaa zitakazozalishwa kwenda sehemu yoyote duniani.
Sitanii, ziara ya Rai Xi ni fursa kwa Tanzania. Tujipange kusomesha watu wetu na kuwaandaa kuchukua nafasi. Utabiri uliopo ni kwamba kama Tanzania haitakumbwa na vurugu za kisiasa ndani ya miaka 20 na 30 ijayo, itakuwa na uchumi mkubwa kuliko nchi yoyote barani Afrika na itakuwa kati ya nchi 20 tajiri duniani.
Ndiyo maana Ujerumani enzi hizo waliichagua kama koloni lake. Mungu atupe nini? Karibu Rais Xi, Watanzania tutakukumbuka kwa uamuzi wako wa kuja Tanzania kutangaza sera China juu ya Afrika.