Umekuwa wimbo wa kila ufikapo msimu wa mvua za masika, kuwasikia viongozi wa Serikali wakihimiza kwamba waishio mabondeni wahame, kwa vile wanaishi kwenye mazingira hatarishi ya maisha yao na mali zao.
Ni sawa na sahihi kabisa. Watu hawa wanatakiwa aidha, wahame wenyewe, au wahamishwe na Serikali, lakini wahamie wapi au wahamishiwe wapi? Hili ni swali ambalo nimekuwa nikijiuliza kila mwaka ufikapo msimu wa mvua za masika, na nimeshindwa kupata jibu kwa vile Serikali miaka yote imekuwa ikisisitiza uhamaji kutoka mabondeni bila ya kuagiza wahamie wapi! Hadi najiuliza kwamba au ni kauli za kisiasa tu?
Jiji la Dar es Salaam ambalo ndilo uso wa Tanzania, halikujengwa kwa utaratibu wa kisasa wa mipango miji. Utakuta kwamba ni asilimia 10 tu ya jiji hili ndiyo inayokidhi taratibu za mipango miji, na asilimia 90 iliyobakia jiji limejengwa holela tu! Na hii imesababishwa na Serikali kujisahau kwa miaka mingi kwa kushindwa kuweka mikakati endelevu ya mipango miji kwa kupima idadi kadhaa ya viwanja kila mwaka kulingana na ongezeko la watu, na kuwagawia wananchi viwanja hivi kwa bei ya Serikali na si kwa bei ya kuruka!
Serikali imekuwa ikipima viwanja mara kadhaa lakini vinavyopimwa ni vichache mno ikilinganishwa na idadi ya ongezeko la watu katika jiji hili. Hata hivyo, baadhi ya waliopewa mamlaka ya kupima na kugawa viwanja hivi hawafuati utaratibu wa kuvigawa, na matokeo yake mtu mmoja anaweza kupewa viwanja 10 kwa bei kubwa ikilinganishwa na bei iliyopangwa na Serikali.
Wale wasiokuwa na uwezo wa bei za kuruka, basi hubakia bila viwanja na kuwakuta wakijitafutia namna ya kupata ardhi kwa bei nafuu ili mradi waweze kujihifadhi, jambo lililochangia kwa kiasi kikubwa kuwa na makazi yasiyotambulika na hatarishi kwa maisha ya watu na mali zao hasa wakati wa mvua za masika.
Nasikitika kwamba kauli za kuwahimiza waishio mabondeni kuhama zinatolewa wakati wa msimu wa mvua za masika tu, mvua zikipita basi na Serikali nayo inakuwa imechoka na inaamua kupumzika hadi msimu mwingine wa mvua uje ndipo tena ianze kuwahimiza watu waishio mabondeni wahame, na wakati mwingi matamko haya hutolewa wakati mvua zipo katikati na watu tayari wapo juu ya mapaa ya nyumba zao!
Je, mtu aliyeko juu ya paa la nyumba atahamaje? Amepanda juu ya paa kwa kuyakimbia maji! Sasa ukimwambia ahame kipindi hicho atahamaje au atahamia wapi wakati mvua zinanyesha kila mahali? Tukiendelea na matamko kama haya yanayotolewa kipindi cha mvua za masika tu, na mvua zikiisha tunaendelea na maisha yetu ya kila siku, tutajikuta nyumba zilizopo mabonde ya Kinondoni na Magomeni zitafika Muhimbili; na zilizopo mabonde ya Kigogo, Buguruni na Vingunguti zitaungana na Tabata!
Sasa mabonde yote yakiwa yameshajengwa nyumba za kuishi, gereji na viwanda, tutaendelea na matamko ya kusisitiza watu wahame au tutaona ndiyo utaratibu wetu?
Watu waliojenga mabondeni wamejinyima na kujitahidi sana, na wengine wameweza kujenga nyumba zenye thamani kubwa na wanaishi mabondeni kwa miaka zaidi ya 30, sasa tunaposisitiza wahame sijui tunawatarajia wahamie wapi wakati katika Mkoa wa Dar es Salaam hakuna hata mita moja ya mraba unayoweza kusema haina mwenyewe, kila hatua ina mwenyewe, lakini Serikali inasisitiza waliojenga mabondeni wahame. Sawa ni lazima wahame, lakini wahamie wapi?
Nadhani ni jambo muhimu kama Serikali ingeliweka utaratibu maalum wa kuzihesabu nyumba zote zilizojengwa maeneo hatarishi ya mabondeni, na kupiga marufuku kujengwa nyumba mpya katika maeneo hayo, na baada ya hapo kuhakikisha kwamba inapima viwanja maeneo yanayokubalika na kisha kuwagawia viwanja hivyo kwa bei ya Serikali, wale wote ambao wamejenga katika maeneo hatarishi ya mabondeni, ili Serikali inapotoa tamko kwamba waliojenga mabondeni wahame, kauli hiyo iwe na ‘logic’ na msukumo wa kisheria, na isiwe ni wakati wa masika tu, hapana, bali iwe ni utaratibu maalum wa Serikali wa kuhakikisha kwamba wale wote waliojenga mabondeni wanaondoka katika kipindi kitakachokuwa kimewekwa na Serikali.