Chonde chonje wavuta sigara

Mhariri,

Ninajitokeza kutumia fursa hii kutoa wito kwa watu wote wanaovuta sigara kuacha kasumba mbaya ya kuvuta sigara katika msongamano wa watu, kwa sababu vitendo hivyo vina athari kubwa zaidi za kiafya kwa wasiotumia bidhaa hiyo.

Ikumbukwe kwamba hata watengenezaji wa sigara huweka maneno ya kutahadharisha matumizi ya bidhaa hiyo kutokana na kutambua madhara yake kwa afya ya binadamu. Hata hivyo, baadhi ya watu wameendelea kupuuza tahadhari hiyo kwa kuendelea kuvuta sigara!

 

Lakini kinachoogopesha zaidi ni pale wataalam wanapotueleza kwamba watu wanaoweza kuathiriwa zaidi na sigara ni ambao hawatumii sigara! Kwamba moshi wa sigara unaotolewa na wavutaji una madhara makubwa zaidi kwa watu wasiyo wavutaji!

 

Miongoni mwa madhara ya sigara yanayotajwa na wataalam wa afya ni kuathiri mapafu na kupunguza nguvu za uzazi. Tunaona kwamba sigara kama ambavyo watengenezaji wenyewe wamekuwa wakithibitisha, ina madhara makubwa katika mwili wa binadamu.

 

Ni kwa sababu hiyo, ninaona umuhimu wa kuwakumbusha wavutaji wa sigara kuepuka tabia mbaya ya kuvuta sigara kwenye misongamano ya watu sokoni, sitendi, kwenye magari, dukani, hoteli na baani. Ikumbukwe kwamba kuna sheria ya kupiga marufuku watu kuvuta sigara katika mazingira ya aina hiyo, ingawa utekelezaji wake bado ni dhaifu!

 

Ninawaomba wavuta sigara wanaoendelea kukaidi onyo linalotolewa na watengenezaji wa bidhaa hiyo kujali afya za wasiovuta sigara kwa kuwa ndiyo wanaokabiliwa na hatari kubwa ya kuathiriwa na sumu iliyomo kwenye sigara.

 

Chonde chonde wavutaji wa sigara, heshimuni sheria iliyowekwa na Serikali kuhusu matumizi ya sigara. Lakini pia acheni kupuuza tahadhari inayotolewa na watengenezaji wa sigara.

 

Mtetezi wa afya njema, Igunga – Tabora