Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amesema viongozi wa ngazi mbalimbali wakiwemo wakuu wa Wilaya, wenye viti wa Serikali za mitaa na watendaji wa vijiji kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika kutunza vyanzo vya maji na uhifadhi wa mazingira.

Akizungumza leo Juni 16, 2023 mbele ya wananchi wa Jimbo la Kibakwe mkoani Dodoma akiwa katika ziara yake ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkuu pamoja na kukagua uhai wa Chama , Chongolo amesema ni vema viongozi wa ngazi zote wakasimamia vema vyanzo vya maji.

“Hapa Kibakwe kulikuwa na mazingira mazuri kwa wakati huo sio ya sasa, mazingira ya wakati huo kulikuwa na uoto wa asili mwingi sana , kulikuwa na maji yanayotiririka mlimani, kulikuwa na mazingira mazuri ya kilimo yanayofaa kwa kilimo na maisha,

“Sasa tumekuwa waharibifu namba moja hilo halikubaliki , na mmi ni kiongozi nimepewa dhamana, nikifika nikamwambia haribuni kesho na keshokutwa laana ya uharibifu wa mazingira itakuwa ya kwetu ,mateso ya uharibifu yataturudia sisi na kizazi chetu kijacho…

” Sisi tusiwe daraja la kuharibu mazingira tukawarithisha ukame ,tukawarithisha jangwa vijana ,watoto na wajukuu Wetu. Ni lazima tujue tunawajibu wa kulinda vyanzo vya maji na niseme hapa kuna Serikali kuanzia ngazi ya Kijiji.

“Mkuu wa Mkoa hili jambo tutaliwekea utaratibu kama kwenye Wilaya hawawezi kusimamia kuhakikisha vyanzo vya maji vinalindwa maana yake kuna haja ya kufanya jambo la tofauti ,haiwezekani tukachezea vyanzo vya maji ambavyo ndivyo vinavyojenga uhakika wa maisha yetu.

” Maji ni uhai tukichezea vyanzo vya maji tunachezea uhai wetu ,hatuwezi kuruhusu hilo hata kidogo na kiongozi kuja kukudanganya unajua nenda panda mpaka mwisho,hakutaki wewe ,haitaki kesho yako ,mimi ni kiongozi mwenye dhamana nawatamani sana muendelee kukipenda Chama Cha Mapinduzi lakini mkipende kwa kuambiwa ukweli.

“Na sio tofauti mjue huo ndio msingi na Mkuu wa Wilaya anawajibu wa moja kwa moja wa kusimamia hilo ,sio vinginevyo ,hawezi maana hatendei haki ,yeye ni msimamizi wa kamati ya usalama ya Wilaya. Vyanzo vikiharibiwa madhara yake ni kwamba hawakutimiza wajibu wao ,ni lazima tulinde vyanzo vya maji, ” amesema Chongolo.

Amesisitiza Chama Cha Mapinduzi kinataka kuona vyanzo hivi vikipimwa na kulindwa kwani viakachwa vikaharibiwa litakuwa ni Taifa la hovyo huko mbele kwani vyanzo vya maji vikiharibiwa hata Serikali ikitoa fedha Sh.bilioni moja maji hayatapatikana.

“Lazima kwanza uwe na chanzo cha maji kama mtu hawezi kutii sheria ajue yeye si rafiki wa wengine na hatua za kisheria dhidi yake haziepukika , hapa maji yalikuwa mengi sana kwenye kile chanzo chenu sasa hivi hayatoki.

” Kuna baadhi ya Wenyeviti na watendaji wa Vijiji wamekuwa na kawaida ya kuuza maeneo ambayo yamehifadhiwa kwa ajili ya matumizi maalum acheni kufanya hivyo , ni wajibu wenu kuyalinda, kuwakamata wanaoharibu vyanzo vya maji sio suluhisho.

“Nimekuwa Mkuu wa Wilaya uliza kwangu nilikopita kama mtu alikuwa anaweza kuchezea hawa watendaji wote walikuwa wamenyooka ,viongozi wa ngazi zote mmepewa dhamana na Serikali yenu,timizenu wajibu wenu ,timizeni wajibu wenu msikae pale kutengeneza urafiki wa kukusanya sadaka kwa uharibifu.

” Hilo halikubaliki kwa sababu kesho na keshokutwa matatizo yanabebwa na Serikali,simama kwenye mstari kutimiza wajibu wenu na mmi nitafuatilia kile chanzo kwa makini kujua na vyanzo vingine vyote nitafuatilia,nitafuatilia na katika kufuatilia kitu ambacho Mwenyezi Mungu amenipa ni hicho.

“Kufuatilia sio kazi ngumu , nikisema nataka kuja hapa muda wowote wote hawa watajipanga mstari kunileta na nitakapokuja sitawaambia wote, nitakuja moja kwa moja kwenye chanzo nikitoka mtakuja kuona matokeo yake , hatuwezi kukaa na nchi kila mtu anaota sharubu kufanya anachotaka.

” Lazima watu waheshimu sheria , waheshimu maeneo maalum yenye tija kwa nchi na sio vinginevyo, mkiwa hapa na uhakika wa maji mtandoka kwenye tatizo la kipindupindu ,mtaondokana magonjwa ya tumbo pamoja na kuondoka katika matatizo mengine.”

By Jamhuri