Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Dar

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo amesema kuwa, kupitia dhamana ya kuongoza Serikali na nchi, kitahakikisha urafiki wa muda mrefu kati ya CCM na Chama cha Kikomunisti cha Cuba (CPC) na uhusiano wa Tanzania na Cuba unaendelea kuimarika zaidi, kwa ajili ya manufaa na maendeleo ya watu wa pande hizo mbili, kupitia ushirikiano imara kwenye nyanja za kilimo, afya na elimu.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo (kulia) akizungumza na Balozi wa Cuba nchini Tanzania Yordenis Despaigne Vera, wakati balozi huyo alipofika kumtembelea.

Katibu Ndugu Chongolo ametoa kauli hiyo leo Jumatano, Novemba 2, 2022, wakati alipokuwa akizungumza na Balozi wa Cuba nchini Tanzania Yordenis Despaigne Vera, wakati balozi huyo alipofika kumtembelea, Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam.

Chongolo amefafanua kuwa, Tanzania na Cuba kupitia vyama vya CCM na CPC kwa miaka 60 sasa, zimekuwa na ushirikiano na urafiki wa kihistoria, ulioasisiwa tangu wakati wa viongozi waasisi wa mataifa hayo, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Fidel Castro katika nyanja mbalimbali za maendeleo.

Amesema kuwa viongozi wa sasa, kupitia vyama na serikali hizo, wanao wajibu mkubwa wa kuimarisha zaidi na kuuendeleza kwa ajili ya tija na ustawi kwa jamii za nchi hizo.

Kwa upande wake, Balozi Yordenis Despaigne Vera ameeleza kuwa ni muhimu na lazima, kwa pande hizo mbili kuendelea kufanya kufanya kazi kwa pamoja zaidi ili kuendeleza uhusiano na urafiki ulioanzishwa na waasisi hao na kujengewa misingi imara kwa miaka kupitia vyama vya CCM na CPC.

By Jamhuri