DAR ES SALAAM

Na Mwalimu Samson Sombi

Janga la virusi vya corona vinavyosababisha homa kali ya mapafu limeendelea kuitikisa dunia tangu kugundulika kwake katika Jiji la Wuhan nchini China, Desemba 2019.

Dunia haikuwa makini na kuchukua tahadhari kubwa wakati ugonjwa huo unaikumba China, badala yake kila nchi iliendelea na shughuli zake huku baadhi ya mataifa makubwa kama Marekani yakidhihaki na kuuita ugonjwa huo kuwa ni virusi vya China.

Baada ya mwezi mmoja virusi vya corona vilianza kusambaa kwa kasi sana katika mataifa mbalimbali yakiwamo ya Afrika. Kasi hiyo ilitokana na mataifa mengine kutokuwa na hofu juu ya ugonjwa huo wakati China ikiendelea na mapambano ya kuudhibiti.

Pamoja na ugonjwa huo kusababisha vifo vya watu wengi katika mataifa mbalimbali kuwahi kutokea tangu Vita ya Kwanza na ya Pili vya Dunia, 1914 – 1918, kisha 1935 – 1945. 

Ugonjwa huo pia umetikisa na kuyumbisha uchumi wa mataifa mbalimbali.

Nchi za Afrika hazikusimama pamoja katika mapambano dhidi ya COVID -19 badala yake kila nchi ilipambana kwa namna tofauti, hali iliyosababisha taharuki kwa baadhi ya nchi katika mapambano hayo.

Afrika ambayo ni bara lenye utajiri mkubwa wa rasilimali, bado kuna changamoto kubwa katika matumizi sahihi ya rasilimali hizo pamoja na rasilimali watu.

Pamoja na mambo mengine, Afrika ilifanikiwa katika harakati zake za kudai uhuru, baada ya baadhi ya nchi kuungana na kuwa na nguvu ya pamoja na sauti moja katika kulikomboa bara hili kutoka katika makucha ya wakoloni. 

Mei 25, 1963, zaidi ya nchi 20 za Afrika zilizopata uhuru zilitia saini makubaliano ya kuundwa kwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) na kupewa jukumu la kuhakikisha nchi zote za Afrika zinapata uhuru na kujitawala zenyewe na hatimaye kujitegemea kiuchumi.

Umoja huo ambao kwa sasa unafahamika kama AU, ulikuwa pia na jukumu zito la kudumisha na kulinda amani na umoja wa Waafrika huku suala la kupambana na ukoloni mamboleo likipewa kipaumbele.

Wakati huu wa janga la corona, AU pamoja na jumuiya zake imeonyesha udhaifu mkubwa baada ya kushindwa kusimama imara katika umoja kwa mapambano dhidi ya COVID – 19 na kusababisha kila nchi kupambana kwa namna yake katika vita hii ya tatu ya dunia.

Kinachogharimu nchi za Afrika katika mapambano dhidi ya corona ni utegemezi wa misaada ya fedha, vifaa na wataalamu kutoka mataifa makubwa ya Magharibi, ambayo na yenyewe yameathiriwa kwa kiasi kikubwa na janga hili tofauti na mategemeo ya wengi.

Udhaifu mwingine unaoonekana katika nchi nyingi za Afrika ni kutokuwa na sekta imara ya afya. Nchi nyingi hazina bajeti ya kutosha ya sekta ya afya. Idadi ndogo, ya wataalamu na mazingira magumu ya kazi ya madaktari na wataalamu mbalimbali wa afya na ustawi wa jamii.

Aidha, nchi nyingi hazina bajeti ya kutosha ya majanga kama ya magonjwa ya mlipuko, raia wengi kutokuwa na bima za afya, pamoja na makundi maalumu kwenye jamii kama wazee, watoto, watu wenye ulemavu na wajawazito kutopewa kipaumbele katika masuala ya afya.

Inaelezwa kuwa huduma kwa watu wenye magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, pumu, kiharusi, ugonjwa wa moyo na matatizo ya HIV hayajawekewa msisitizo wa kutosha.

Hayo pamoja na mambo mengine yamechangia kwa kiasi kikubwa kusambaa na kuleta madhara makubwa kwa virusi vya corona Afrika.

Afrika ikiwa na idadi ya watu bilioni 1.3, kwa wastani mataifa mengi yana madaktari wawili wanaohudumia watu 10,000. 

Mfano Nigeria, taifa lenye idadi kubwa ya watu barani Afrika, ina madaktari wanne kwa kila watu 10,000; Kenya ina madaktari wawili kwa watu 10,000 huku Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ikiwa na daktari mmoja kwa watu 10,000!

Hii ni kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ambalo linapendekeza daktari mmoja kwa kila watu 1,000.

Mwaka jana wakati ugonjwa huo unapamba moto, hapa Afrika ilielezwa kuwa katika mataifa 41 kuna uhaba wa mashine 2,000 za kupumulia katika vituo vya afya vya umma.

Kama hiyo haitoshi Mei 3, mwaka jana, Rais Dk. John Magufuli alieleza wasiwasi wake kuhusu mashine za kupima ugonjwa wa corona zilizokuwapo katika maabara ya taifa baada ya mashine hizo kutotoa majibu sahihi ya vipimo vya corona kwa wagonjwa waliopimwa ikiwa ni pamoja na  wanyama na baadhi ya matunda kama mapaipai kufanyiwa vipimo hivyo.

Katika kikao cha viongozi wa AU mwaka 2011, nchi nyingi ziliahidi kutenga asilimia 15 ya bajeti zao kuboresha sekta ya afya, maarufu kama Azimio la Abuja.

Ni mataifa machache tu yametekeleza ahadi hiyo ambayo ni Rwanda, Malawi, Mauritius na Seychelles. Mengi yameshindwa kutekeleza kutokana na changamoto za kiuchumi na bajeti tegemezi.

Azimio hilo lililenga kuhakikisha sekta ya afya inapewa uzito unaostahili. Kadiri muda unavyosonga mbele, mataifa mengi yanashindwa kutekeleza ahadi hiyo muhimu ikiwamo Nigeria, taifa lenye uchumi mkubwa barani Afika.

Ofisa Mkuu wa AMREF (Afrika), Dk. Githinji Gitahi, anasema inaonekana Afrika imepiga hatua za kujitolea lakini katika hali halisi hakuna hatua zilizopigwa, kwani mataifa mengi ya Afrika bado ni tegemezi katika sekta nyingi, ikiwamo sekta muhimu ya afya.

Kwa mujibu wa Dk. Gitahi, Rwanda inaendelea kupiga hatua kufikia mpango wa afya kwa wote lakini bado kuna changamoto kadhaa.

Tanzania nayo imepiga hatua; kwa mujibu wa Rais wa Chama cha Madaktari (MAT), Dk. Elisha Osati.

“Ukiangalia vipengele vya afya kwa wote, Tanzania ina miundombinu mizuri. Tumejitahidi sana katika ujenzi,” anasema Dk. Osati.

“Hata hivyo changamoto ipo upande wa ufadhili kwa kuwa bajeti ya Tanzania bado haijafikia kiwango cha asilimia 15 inayopendekezwa,” anabainisha mtaalamu huyo.

Ghana inatajwa kuwa na ufanisi katika sekta ya afya lakini inakabiliwa na changamoto ya ufadhili.

Dk. Lydia Osane Selby, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bima ya Afya nchini humo, anasema: “Bila shaka sera maalumu kama hii inakabiliwa na changamoto mbalimbali lakini tutaendelea kuzitatua kadiri ya uwezo wetu.”

Uganda inaelezwa kuwa serikali yake ilianza utekelezaji wa baadhi ya sera zilizolenga kuwapunguzia mzigo watu maskini, lakini changamoto kubwa imekuwa ni ufinyu wa bajeti.

Imefahamika kuwa kutokana na ufinyu wa bajeti katika sekta mbalimbali kwa mataifa ya Afrika, wataalamu wengi wakiwamo wa afya wamekimbilia mataifa ya ng’ambo kufanya kazi huko kutokana na ugumu wa maisha na mazingira magumu ya kufanyia kazi hapa Afrika.

Katika mapambano dhidi ya COVID -19 tumesikia na kushuhudia maeneo mbalimbali hapa Afrika jinsi madaktari na wauguzi wanavyofanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi kutokana na ukosefu wa vifaa maalumu vya kujikinga na virusi vya corona wakati wa kuhudumia  wagonjwa (PPE), hali iliyosababisha baadhi yao kupoteza maisha.                                                  

Kumekuwa pia na migomo ya mara kwa mara ya wataalamu wa afya wakidai stahiki zao na madai ya kuongezewa mishahara kutokana na mazingira magumu ya kazi.

Wakati mapambano hayo yakiendelea, baadhi ya nchi za Afrika; ikiwamo Madagascar na Tanzania, matumizi ya tiba asili yalichukua sura mpya.

Nchi hizi zimeonekana kufanikiwa katika matumizi ya tiba hizo huku mataifa mengine yakibeza na kuchukua hatua za kujifungia (lockdown) kama njia kuu ya kupambana na janga hilo.

Siku za hivi karibuni kumepatikana chanjo ya COVID -19, Chanjo imepokewa kwa hisia tofauti na baadhi ya mataifa ya Afrika. Mengi yakitaka kufanyiwa utafiti wa kina na wataalamu wa ndani kabla ya kuanza kutolewa kwa wananchi.

Aprili 6, mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan aliunda kamati maalumu ya tathmini ya ugonjwa wa corona nchini na kutoa ushauri namna ya kukabiliana na ugonjwa huo.

Mei 17, mwaka huu, kamati hiyo ilikamilisha kazi ya kufanya tathmini dhidi ya ugonjwa huo na kukabidhi ripoti hiyo kwa Rais, ikiwa na mapendekezo 19.

Katika mapendekezo hayo, kamati imeshauri njia mbalimbali zitakazowezesha serikali kupata fedha kutoka ndani ya bajeti ya serikali na wadau wa maendeleo yakiwamo mashirika ya kimataifa na sekta binafsi kwa ajili ya kugharamia vifaa tiba, mafunzo na chanjo.

Mhadhiri (mstaafu) wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Dk. Flat Mfangavo, anasema viongozi wa kisiasa Afrika wanapaswa kutambua na kuthamini mchango wa wataalamu wa afya na kuwa tayari kupokea ushauri wa kitaalamu katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikumba Afrika.

“Changamoto kama hizi hufanya watu wafikirie zaidi na kutafuta ufumbuzi wa kudumu badala ya kutegemea kila kitu kutoka mataifa tajiri,” anasema Dk. Mfangavo.

Ofisa Uvuvi Mwandamizi Mkoa wa Geita, Tito Mlelwa, anasema Afrika inapaswa kujitegemea katika nyanja zote, ikiwamo sekta ya afya kwa sababu tuna rasilimali na wasomi wa kutosha.

0755 985966

Rais wa Chama cha Madaktari (MAT), Dk. Elisha Osati
470 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!