DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Serikali imeanza kutoa takwimu za mwenendo wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona unaofahamika kwa jina la UVIKO-19, zikionyesha kuwa watu 719 wamekwisha kufariki dunia kutokana na ugonjwa huo nchini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, hadi Septemba 27, mwaka huu, jumla ya watu 25,846 wameambukizwa ugonjwa huo huku kukiwa na vifo vitano vipya.

Mei mwaka jana serikali ilisitisha utoaji wa taarifa za mwenendo wa UVIKO-19 na kusababisha malalamiko kutoka jumuiya ya kimataifa pamoja na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO).

Taarifa hiyo ya pili kutolewa ni ya wiki ya Septemba 18 hadi 24, 2021, inayoonyesha pia kwamba vipimo vipya vimefanyika kwa watu 7,281.

“Vipimo vipya 6,772 vimefanywa kwa wasafiri wanaokwenda nje ya nchi na 6,692 wanaoingia nchini,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo ikiongeza kuwa jumla ya vipimo 304,450 vimekwisha kufanyika.

Kwa wiki hiyo, hakuna mfanyakazi wa sekta ya afya aliyegundulika kuwa na UVIKO-19, ingawa kwa ujumla tangu ugonjwa huu uingie nchini, wafanyakazi 3,316 wa sekta hii wameugua au kugundulika kuwa na virusi hivyo, huku mmoja kati yao akifariki dunia.

Taarifa hiyo ya kina inaonyesha kuwa wagonjwa waliowahi kulazwa hospitalini kwa matatizo ya UVIKO-19 nchini ni 4,355, kati yao 237 ndio waliohitaji uangalizi maalumu (ICU).

Ndani ya wiki hiyo moja, watu 358 walikuwa wamelazwa hospitalini; 45 wakiwa ICU.

Hatua mbalimbali tayari zimekwisha kuchukuliwa kupambana na UVIKO 19 nchini, ikiwamo kuiwezesha mikoa ya Songwe, Mbeya, Pwani na Morogoro katika kupambana na ugonjwa huu.

409 Total Views 6 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!