CRB yaonya makandarasi wanaoghushi nyaraka

Na Mwandishi Wetu

Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), imewaonya makandarasi wenye tabia ya kughushi nyaraka ili waonekane wana vigezo vya kusajiliwa daraja la kwanza au la pilli ili wapate zabuni kubwa za ujenzi.

Onyo hilo limetolewa mwishoni mwa wiki jijini Dodoma na Msajili wa bodi hiyo, Mhandisi Rhoben Nkori, wakati akizungumza na makandarasi kwenye mafunzo ya siku mbili kuhusu kazi za ubia (JVs).

Amesema bodi hiyo imekuwa ikiwajengea uwezo makandarasi wa ndani ili waweze kufanyakazi na makandarasi wakubwa na hatimaye waweze kufanya miradi hiyo wenyewe baada ya kupata uzoefu.

“Lengo lingine ni kuwajengea uwezo wa kushirikiana wenyewe kwa wenyewe, mnaweza kuwa makandarasi wa daraja moja mkafanyakazi mnapeana uzoefu na mkautumia kufanyakazi kubwa,” amesema

Mhandisi Nkori alisema CRB hivi karibuni imepokea maombi mengi ya kampuni za ukandarasi zinazotaka kupanda madaraja.

“Unakuta kampuni inaomba kuongezewa daraja lakini ukiifanyia tathmini haina hizo sifa za hilo daraja analotaka, mwingine anataka daraja la kwanza mwingine la pili sasa picha hiyo inatuonyesha kwamba kuna miradi mingi mikubwa kwenye sekta inayohitaji makandarasi wakubwa,” amesema Mhandisi Nkori.

“Nawashauri wakandarasi wadogo na wakati wajitahidi kushirikiana na makandarasi wakubwa ili kwanza wapate uzoefu wa kufanyakazi kubwa badala ya kukimbilia kuomba kupanda daraja, wengine wanaghushi hadi nyaraka waonekane wamekua na vigezo vya kusajiliwa daraja la kwanza au la pili,” amesema

Alisema iwapo makandarasi watafanya miradi kwa ushirikiano wa kweli tofauti na ile ambayo wakubwa wanawasindikiza wadogo watapata uzoefu wa kazi hizo.

“Kuna tabia wakandarasi wadogo wanatafuta zabuni wakishapata zabuni lakini anamtafuta mkandarasi mkubwa washirikiane ingawa eneo la ujenzi anakauwa Yule mkandarasi mdogo na kwa kuwa hana uwezo mkubwa kazi zinamshinda na lawama zinakuja kwa makandarasi wa ndani,” amesema

“Kwa kuondoa changamoto hiyo naomba kuwasisitiza kwamba kama umeamua kweli kufanya kazi ya ubia uwe ubia wa kweli siyo ule wa kusindiizana, unaweza kumsindikiza mtu kumbe uwezo wake ni mdogo sana mwisho wa siku jina la kampuni yako ambalo ndilo lilishawishi zabuni kupatikana linachafuka,” amesema

Amesema bodi hiyo itakapobaini makandarasi wanaofanya ubia wa ujanja ujanja itawachukulia hatua kali ili wasiendelee kuchafua sekta nzima ya ujenzi kwa kuonekana ubabaishaji wa aina hiyo.

Alisema serikali imeonyesha nia ya kutenga miradi kwa makandarasi wa ndani kwa lengo la kuwajengea uwezo hivyo watakapoipata waonyeshe uwezo kwa kuifanya kwa ufanisi na kwa wakati.

“Mnapokuwa kwenye mafunzo kama haya muwe makini na mafunzo haya mkayafanyie kazi ili miradi ile ya serikali itakapotolewa muifanye kwa ufanisi na serikali ione umuhimu wa kuendelea kutenga miradi mingi kwa makandarasi wa ndani,” alisema Mhandisi Nkori.

Alisema ni vizuri mkandarasi anapoona hawezi kuifanya kazi aliyoomba awashirikishe wenzake ili waifanye kwa ubia na kuikamilisha kwa wakati na kwa ufanisi hali ambayo itaivutia serikali kuwapa miradi mingine.

“Utakapofanya miradi mingi ya ubia na ukaona kabisa kwamba umepata uzoefu wa kazi kubwa kubwa, unawataalamu wa kutosha, mitambo na kiuchumi uko vizuri basi milango ya bodi iko wazi ulete maombi yako kama utaonekana unasifa utapanda,” amesema

Msajili Msaidizi wa CRB, Mhandisi David Jere alisema mafunzo hayo yamewashirikisha makandarasi 103 wa madaraja mbalimbali kwenye mikoa yote nchini.

Amesema lengo la mafunzi hayo ni kuwaelekeza makandarasi namna ya kufanya kazi kwa ubia wenye tija na kuwawezesha kukua ili waweze kutekeleza miradi mikubwa kama walivyo wageni.

Amesema mara kadhaa kumetokea changamoto mbalimbali kama kampuni ziliingia ubia bila kuzingatia misingi ya ubia hali ambayo inakwamisha miradi ya ujenzi.

“Kwa hiyo mafunzo haya ni muhimu kuwaandaa kuingia kwenye ubia wenye tija kama vile kufahamiana vizuri baina ya wanaoingia ubia na wajue mkataba unaainisha wajibu wa kila mbia kwenye huo mkataba na asipotimiza wajibu wake nini kinachofuata ili kuondoa misuguano,” amesema