Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Dalaam
SHIRIKISHO la Wenye Viwanda (CTI), limeseme kuwepo kwa utitiri wa tozo katika kila mkoa na halmashauri kumekuwa kikwazo katika ustawi wa biashara na uwekezaji nchini.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Shirikisho hilo, Leodegar Tenga katika warsha maalumu ya kuwajengea uwezo wadau wa sekta ya viwanda vya chakula na vinywaji kupitia utafiti uliofanywa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Utawala Bora na Maendeleo ya Wajasiliamari Dk Donath Olomi.
Utafiti huo ulioangazia namna tozo hizo zilivyo kikwazo kwa wafanyabiashara kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Tenga alisema Dk Olomi ni mtafiti msomi na ameainisha vitu vingi ikiwamo mapendekezo ya kufuata kuondoa vikwazo hivyo, akisisitiza kuwa lengo ni kuwapa nafasi nzuri wafanyabiashara wakubwa wanaotamani kuja kuwekeza nchini.
Tenga alisema athari ya utofauti wa tozo unaathari kibiashara ikiwamo kuongezeka kwa bei za bidhaa, na hivyo kusababisha mlaji kununua bidhaa ya bei ndogo kwa gharama kubwa.
“Kwa mfano mtu amevuna mazao yake Mbeya sasa ili aje kuuza Dar es Salaam kwenye soko kubwa atalazimika kusafirisha, sasa anatozwa huko akifika Iringa anatozwa tena, njiani pia hivyohivyo anakutana na tozo nyingine akifika Dar es Salaam nako anakutana na tozo nyingine,” alisema.
“Tunataka huyi mfanyabiashara akishatozwa Mbeya asitozwe tena sehemu nyingine, tunapaswa tuwe na utaratibu ambao utatambua kama ameshatozwa, hatujafanikiwa kuondoa vikwazo. Tusipofanya hivyo tunawakwamisha hawa wafanyabiashara au watafanya ujanja wa kutoa rushwa njiani ili kupunguza hizo tozo,” alisema Tenga
Naye Dk. Olomi alisema kutokana na utafiti alioufanya alipendekeza kuwe na uwazi kuhusu tozo hizo akifafanua kwamba katika halmashauri karibu zote tozo hizo hazijatangazwa mahali popote hivyo mwekezaji anayataka kuwekeza hawezi kujua viwango vya tozo na kama ziko kwa mujibu wa sheria au siyo.
Pia alipendekeza serikali iangalie namna ya kuondoa tozo zinazokinzana na kujirudia rudia kwenye mikoa na halmashauri nchini akitolea mfano kwamba mtu akiingiza lori mjini (kariakoo) kwaajili ya kupakia au kuondoa bidhaa atakutana na tozo ya maegesho.
Alisema pia lori hilo litatozwa malipo ya kuingia katikati ya Jiji na wakati mwingine haijulikani wapi ni mwisho wa kulipia kwa hiyo kuna maeneo kama hayo yanahitaji marekebisho.
Alisema mkanganyiko mwingine ni zile tozo zinazotozwa na halmashauri na nyingine serikali kuu. “kwa mfano tozo ya kupima afya kwenye viwanda unatozwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahala Pa kazi (OSHA) lakini pia serikali za mitaaa kiutaratribu zinatofautiana kama unapima magonjwa yanayoambukizwa unapimwa na halmashauri na yale yasiyoambukiza unapimwa na OSHA na tozo wanayotoza kwa mtu mmoja ni sh 70,000 sasa ukiangalia hii haijakaa sawa,”
“Hizi tozo zisiwepo kama zinania ya kukomoa wenye viwanda bali zitumike kuweka mazingira mazuri kwahiyo kuna changamoto za aina hiyo,” alisema Dk Olomi.
Mhandisi wa Viwanda Mkuu Kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Karoline Varelian alisema serikali itachukua mapendekezo ya wadau hao, kuchambua na kuyafanyia kazi ili kuweka mazingira rafiki.
Alisema tayari Wizara imeshaanza kuzifanyia marekebisho baadhi ya sera na sheria ila kwa sasa watakwenda kuyafanyia kazi kwa haraka mapendekezo yaliyotolewa na wadau ili kuondoa mlalamiko ya wenye viwanda.
Alisema tozo zimekuwa nyingi na kuahidi kuwa watapitia ushauri uliotolewa kwenye utafiti uliofanywa na Dk Olomi ili kuwapunguzia mzigo wafanyabiashara hususani wenye viwanda vya chakula na vinywaji.