Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

SHIRIKISHO la Wenye Viwanda Nchini (CTI) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya  Biashara (TanTrade), wameandaa maonyesho makubwa ya kimataifa ya viwanda ambapo zaidi ya viwanda 200 vya ndani na nje ya nchi vitashiriki maonyesho hayo.

Mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa maonyesho hayo ya Tanzania International Manufactures TIMEXPO 2023, yatakayofanyika kuanzia Oktoba 4-6 kwenye ukumbi wa Diamond Jubelee,  anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za CTI jana, Mkurugenzi wa CTI, Leodger Tenga, amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki maonyesho hayo ili kujionea teknolojia mpya na bidhaa mbalimbali kutoka ndani na nje.

Mkurugenzi wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), Leodeger Tenga akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maonyesho ya viwanda yanayotarajiwa kuanza wiki ijayo jijini Dar es Salam. Kushoto ni Mkurugenzi wa Uhamasishaji Biashara wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (Tantrade), Fortunatus Mhambe na kulia ni Mkurugenzi wa Huduma za Wanachama CTI, Neema Mhondo

“Maonyesho kama haya ambapo wenye viwanda pekee wanakuja kuonyesha teknolojia mpya mbalimbali wanazotumia kwenye uzalishaji wa bidhaa zao ni mara chache sana kutokea hapa nchini ndiyo maana sisi CTI na Tantrade tunayachukulia maonyesho haya kwa umuhimu mkubwa sana,” alisema Tenga.

“Viwanda vyote vikubwa hapa nchini vimo na wahusika wameshajiandikisha na tunawaomba wote washiriki kwasababu hili ni jambo lao waje kuonyesha nini wanafanya ili tuweze kutangaza sekta hii ya uzalishaji viwandani ambayo tunaona ndiyo sekta mhimili wa uchumi wetu,” alisema  Tenga

Alisema kwenye maonyesho hayo viwanda vikubwa duniani vikiwemo vile vinavyotengeneza ndege vitashiriki na kwenye maonyesho hayo vitaonyesha namna ndege zinavyotengenezwa kuanzia hatua ya awali kabisa mpaka kupaa angani.

Naye Mkurugenzi wa Uhamasishaji Biashara wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (Tantrade), Fortunatus Mhambe, alisema maonyesho hayo ni makubwa ya aina yake kuwahi kutoka nchini hivyo aliwataka watanzania washiriki kikamilifu.

Alisema Tantrade imekuwa ikiandaa maonyesho ya viwanda mara kadhaa lakini mwaka huu imeona ije na picha nyingine tofauti kuonyesha bidhaa za viwandani pekee kama hatua ya kuimarisha uhusiano wa sekta binafsi na sekta ya umma.

Mkurugenzi wa Uhamasishaji Biashara wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (Tantrade), Fortunatus Mhambe, akizungumza kuhusu maonyesho ya kimataifa ya viwanda maarufu TIMEXPO 2023 yanayotarajiwa kuanza Oktoba 4 hadi 6 Dar es Salaam. Anayefuata ni Mkurugenzi wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), Leodegar Tenga na Mkurugenzi wa Huduma za Wanachama CTI, Neema Mhondo

“Kwetu haya ni mafanikio makubwa sana kwasababu tumeona viwanda mbalimbali vitakavyoshiriki kwa upande wa kilimo, teknolojia, ujenzi, kemikali za viwandani wote hawa wamesema watashiriki kuonyesha huduma zao kwa hiyo tunapenda kuendelea kuwahamasisha waendelee kujiandikisha washiriki maonyesho,” amesema Mhambe.

Amesema maonyesho hayo yatakuwa fursa kubwa kwa wenye viwanda kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili kwani viongozi wa taasisi mbalimbambali za serikali wakiwemo mawaziri watashiriki.

“Haya hayatakuwa maonyesho tu bali fursa muhimu kwa wenye viwanda kuelezea changamoto zao na kupata majibu ya hapo hapo. Wananchi nao waje waone ubunifu na teknolojia mbalimbali za kisasa zitakazokuwepo pale hii ni fursa ambayo siyo ya kukosa na kutakuwa na kiwanda cha kutengeneza ndege kitaonyesha kinavyotengeneza kuanzia mwanzo,” amesema

Mkurugenzi wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), kushoto Leodeger Tenga akizungumza na wageni walioshiriki mkutano na waandishi wa habari.
Mkurugenzi wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), kushoto Leodeger Tenga akizungumza na wageni walioshiriki mkutano na waandishi wa habari.
Mkurugenzi wa Uhamasishaji Biashara wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (Tantrade), Fortunatus Mhambe, akizungumza kuhusu maonyesho ya kimataifa ya viwanda maarufu TIMEXPO 2023 yanayotarajiwa kuanza Oktoba 4 hadi 6 Dar es Salaam. Anayefuata ni Mkurugenzi wa Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), Leodegar Tenga na Mkurugenzi wa Huduma za Wanachama CTI, Neema Mhondo
 

By Jamhuri