Na Kija Elias,JamhuriMedia,Moshi

Jeshi la Polisi Mkoani Kilimanjaro limemtia mbaroni Dk. Wilson Solly kwa tuhuma za kuwatapeli malimilioni ye fedha vijana zaidi ya 76 kutoka mikoa mbalimbali kwa kutumia jina la aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi William Lukuvi.

Mtuhumia huyo alikamatwa Septemba 15 katika eneo la makazi ya askari wa jeshi hilo (Police Line), akitoa mafunzo kwa vijana hao wanaodaiwa kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Tanga huku akiwahadaa kuwa atawapatia ajira baada ya kumaliza mafunzo.

Kamishna msaidizi wa Jeshi la Polisi mkoa wa Kilimanjaro (ACP) Simon Maigwa, alithibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na kwamba Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi na pindi utakapokamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.

ACP Maigwa amesema uchunguzi wa awali baada ya kuwasiliana na viongozi wanaotajwa, kamanda walisema hawamtambui na kutaka sheria kuchukua mkondo wake.

Kamanda Maigwa amesema Polisi ilifanikiwa kuokoa fedha zaidi ya Sh milioni 2.1 ambazo tayari baadhi ya vijana walishalipa kama gharama za utengenezaji vyeti baada ya mafunzo.

Amesena mtuhumiwa huyo ataendelea kushikiliwa hadi hapo ushahidi utakapotikana ikiwemo kuwasiliana na baadhi ya mikoa ambayo anadaiwa kufanya mafunzo.

Hata hivyo alipoulizwa kuhusu elimu yake mpaka kujiita daktari Solly amesema yeye si daktari wa kitaaluma bali ni wa Biblia akidai amesomea Theolojia.

Akizungumza na wanahabari kabla ya kukamatwa na Polisi, mtuhumiwa huyo alijinadi kuwa Mkurugenzi wa Mradi wa Ujuzi na Ajira Tanzania na kwamba yupo mjini Moshi kwa kumwakilisha Waziri Lukuvi.

Amesema amekuwa akipita katika maeneo mbalimbali ya Tanzania kwa ajili ya kutoa elimu kama hizo na lengo kubwa la mradi huo ni kuwaelimisha vijana kuhusiana na masomo au fani za ujuzi, kwani vijana wakitapa ujuzi wanauwezo wa kujiajiri wenyewe na ni rahisi pia kuajiriwa Serikalini.

Vijana hao wanadaiwa kutozwa shilingi 35,000 kila mmoja kama gharama za fomu za kujiunga na mafunzo hayo na baada ya baadhi kutilia shaka walitoa taarifa Polisi na mtuhumiwa huyo kutiwa mbaroni.

Hata hivyo alipotafutwa Mbunge wa Jimbo la Isman Lukuvi, kuzungumzia kama kweli alimtuma huyo, alikataa kumtambua na kusema hakuna aliyemtuma Moshi wala huwa hafanyi mafunzo kama hayo.

By Jamhuri