Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule ametoa wito kwa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kuwafuatilia wamiliki wa viwanda wasiofuata sheria ya usalama wa kazi ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Mtambule amesema hayo jana Aprili 19, 2024 wakati akifungua mafunzo kuhusu usalama na afya mahali pa kazi kwa wahariri wa vyombo vya mbalimbali vya habari iliyoandaliwa na OSHA.

Amesema OSHA wanatakiwa kuwa wakali kwa wamiliki wa viwanda ambao wanaovunja sheria pamoja na kuwasajili kwenye mfumo ya kielekroniki ili kuwabaini na kuwachukulia hatua.

Amesema kutokana na jitihada zinachukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita kuhamasisha uwekezaji nchini, shughuli nyingi za kiuchumi zimekuwa zikianzishwa na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi jambo linalohitaji wahusika katika uzalishaji kuwa na uelewa wa kutosha wa masuala ya afya na usalama kazini.

“Uchumi wa nchi yetu unakuwa kwa kasi na uwekezaji unaongezeka kila siku. Mathalani Wilaya ya Kinondoni pekee kwasasa ina zaidi ya viwanda 150 ukiachilia mbali shughuli nyingine za kiuchumi zinazoajiri mamilioni ya Watanzania. Hivyo, unaweza kuona ni kwa jinsi gani kuna umuhimu wa kuhakikisha sehemu za kazi zinakuwa na mifumo imara ya kulinda nguvukazi pamoja kuhakikisha kwamba waajiri na wafanyakazi wanakuwa na uelewa wa kutosha juu ya taratibu muhimu za usalama na afya mahali pa kazi,” amesema Mtambule.

Hata hivyo ametoa wito kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini kutumia nafasi zao kuwaelimisha waajiri na wafanyakazi kuhusiana na uzingatiaji wa kanuni bora za usalama na afya katika sehemu za kazi ili kupunguza ajali, magonjwa na vifo vinavyoweza kusababishwa na vihatarishi vya usalama na afya mahali pa kazi.

“Ili kufanikisha jukumu hilo la kuelimisha jamii ya waajiri na wafanyakazi, OSHA inawahitaji wahariri kama wadau muhimu ambao mnaweza kufikisha elimu hiyo kwa haraka zaidi na ndio maana wameona ni vema mkapatiwa mafunzo haya. Hivyo, niwapongeze kwa kazi kubwa mnayofanya lakini ninawaomba muendelee kushirikiana na OSHA na Serikali kwa ujumla katika kuhabarisha na kuwaelimisha Watanzania kuhusiana na masuala mbali mbali likiwemo suala usalama na afya kazini.”

Aidha, DC Mtambule ameipongeza OSHA kwa kazi nzuri ya kusimamia utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 pamoja na kanuni zake na amewataka watendaji wa Taasisi hiyo kuendelea kufanya kazi kwa weledi na kuwachukulia hatua waajiri wote wanavunja sheria husika.

Naye Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda amesema katika kipindi cha miaka mitatu (2021-2023) Wakala umefanikiwa kuongeza idadi ya maeneo ya kazi yaliyosajiliwa kutoka 4,336 hadi 30,309 ambapo ongezeko hilo ni sawa asimilia 276.

“Aidha idadi ya kaguzi zilizofanyika zimeongezeka kutoka kaguzi
104,203 hadi kufikia kaguzi 776,968 sawa na asilimia 132. Kaguzi hizo zinahusisha Ukaguzi wa Jumla, Ukaguzi Maalum kama vile Ukaguzi wa Usalama wa Umeme, Vyombo vya Kanieneo, ukaguzi wa vifaa vya kunyanyulia vitu vizito, ukaguzi wa kiegonomia pamoja na tathmini ya vihatarishi vya kimazingira.

“Pia kumekuwa na ongezeko la asilimia 175 ya Wafanyakazi waliopata mafunzo ya Usalama na Afya mahali pa kazi kutoka wafanyakazi 32,670 hadi kufikia Wafanyakazi 47,090,” amesema Mwenda.