Na Suzy Butondo,JamhuriMedia, Shinyanga

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Joseph Mkude amewashauli viongozi wa sekta mbalimbali katika wilaya ya Kishapu kutumia takwimu za sensa, ili kuleta umakini na ufanisi kwa kuzingatia idadi ya wananchi katika kutatua mipango ya maendeleo na kujiondoa kwenye umasikini.

Hayo ameyasema leo February 13,2024 kwenye mafunzo ya usambazaji na matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi kwa viongozi na makundi mbalimbali, ambao ni watendaji wa vijiji, kata, maafisa tarafa na viongozi mbalimbali katika wilaya ya Kishapu Mkoani hapa, ambapo amewaomba viongozi wote kutumia takwimu, ili kujielekeza kujiondoa kwenye umasikini.

Mkude amesema mafunzo haya yataongeza umuhimu mkubwa kwa wana Kishapu na yatazingatia mahitaji halisi na kuhakikisha mipango ya wilaya inafanikiwa kiurahisi kwa sababu idadi ya watu na makazi itakuwa inajulikana.

Meneja Idara ya Mifumo ya Takwimu za kijiografia Benedict Mugambi akitoa ufafanuzi kwa viongozi, kwenye mafunzo ya matokeo ya Sensa wilayani Kishapu

“Niwaombe viongozi wangu wote tuliopata mafunzo hapa tuichukue hii elimu tuwapelekee na wenzetu ambao hawapo katika mafunzo haya ili wajue, kijiji chetu, kata yetu wilaya yetu ina watu wangapi, kama kuna mahitaji mbalimbali yakiwemo ya sekta ya elimu, sekta ya afya, barabara na maji yatekelezwe kwa kuzingatia takwimu husika,”amesema Mkude.

“Ni lazima kuwe na mipango bora kwa kutumia takwimu,napenda niwakumbushe kwamba matumaini yatawezesha kuwa na mabadiliko chanya, kwani katika uzinduzi wa sensa Rais wetu Samia Suluhu alisisitiza kwamba sensa itasaidia kupanga mipango ya maendeleo na kuhakikisha yanatekelezwa kwa wakati,”ameongeza Mkude.

Kwa upande wake meneja idara ya NBS mifumo ya takwimu za kijiografia Benedict Mugambi amewakaribisha wadau wote wazifikie ofisi za takwimu ili waweze kupatiwa matokeo mbalimbali wanayohitaji, kwani kila kijiji kimefikiwa,kaya na majina halisi ambazo zinaeleza anaishi na familia ngapi na ana choo au hana, hivyo takwimu zote zinaeleza.

Naye mtakwimu Mwinyi Omary kutoka NBS akiwasilisha taarifa za usambazaji na uhamasishaji wa matumizi ya matokeo ya Sensa ya mwaka 2022, amesema Tanzania kwa sasa ina idadi ya watu Milioni 61.7, ambapo kwa Mkoa wa Shinyanga wapo Milioni 2.2, na wilaya ya Shinyanga ni 468.661, Kahama Manispaa 453,654, Ushetu 390,593, Msalala 378,214, Kishapu 335,483 na Manispaa Shinyanga Idadi ya watu ni 214,744.

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Joseph Mkude ajizungumza kwenye mafunzo ya matokeo ya sensa kwa viongozi mbalimbali kutoka wilaya ya Kishapu

Mwenyekiti wa vyama vya watu wenye ulemavu Shivyawata wilaya ya Kishapu Seif Rashid amesema Sensa imewasaidia kujitambua na kujua wako wangapi watu wenye ulemavu kwa wilaya ya Kishapu, ili hata wanavyofanya vikao vyao wakiambiwa kuwasilisha wanawasilisha takwimu za ukweli.

“Pia tunashukuru sana kwa kupata mafunzo haya ya matokeo ya sensa mwaka. 2022, lakini tulipendelea tuwezeshwe wenye uoni hafifu tukuziwe herufi tuzione kwa usahihi, na kwa wale wanaotumia nucta nundu kwa wakati mwingine wapewe hizo alama ili watoe maoni yao kiusahihi zaidi,”amesema Rashid.

Diwani wa kata ya Kiloleli Edward Manyama amesema mafunzo hayo yatawasaidia kwenda kuwaelimisha wananchi juu ya kuhesabiwa ili kwa mara nyingine waweze kujitokeza kwa wingi wasiogope kwa sababu serikali inania nzuri ya kufanya maendeleo pale panapoonekana kunahitajika kufanya jambo furani.

Viongozi mbalimbali wa vijiji na kata wakiwemo madiwani wakimsikiliza mkuu wa wilaya akitoa ufafanuzi kwenye mafunzo ya matokeo ya Sensa wilayani Kishapu
Diwani wa Kata ya Kiloleli Edward Manyama akiulizia jambo kwenye mafunzo ya matokeo ya Sensa Kishapu
Meneja wa Odara ya amifumo ya Takwimu za kijiografia Benedict Mugambi akikabidhi ramani ya wilaya ya Kishapu kwa viongozi wa wa wilaya ya Kishapu
Mwenyekiti wa chama cha watu wenye ulemavu Wilaya ya Kishapu Shivyawata Seif Rashid akizungumza baada ya kumaliza mafunzo ya matokeo ya Sensa wilayani Kishapu ambaye aliomba watu wenye uoni mdogo waongezewe saizi za maandishi ili waweze kuona vizuri maandishi