Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

MKUU wa Wilaya ya Nzega Naitwapwaki Tukai, amesema atakula sahani moja na anayehujumu vyandarua vya serikali.

Amesema iwapo atabaini yupo anauza au kufugia kuku kwa kisingizia kuwa vinapunguza nguvu za kiume hatamvumilia.

Akizungumza jana mkoani Tabora, katika usambazaji wa vyandarua unaofanywa na Bohari ya Dawa (MSD), Naitwapwaki amesema, hatakubali kuona jitihada za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan za kuboresha maisha ya Watanzania na sekta ya afya yanarudishwa nyuma kwa makusudi, hususani kwa kukwamisha mradi huo wa usambazaji wa vyandarua kwa wananchi.

Amesema, atahakikisha anakula sahani moja na anayehujumu vyandarua hivyo kwa kuwa anajua wapo waliojipanga kuvifanyia biashara kwa kuwauzia wenye maduka.

“Nzega inahitaji watu waaminifu sitavumilia mtu atakayeuza vyandarua vya serikali wafanyabiaahara msijaribu nikikuta dukani kwako wewe ni muhujumu, utalipa vile ninavyotaka mimi au kufilisiwa hii ni mali ya serikali.

“Niwatake wanawake wenzangu msikubali kudanganywa na kukimbiwa kitandani, mwanaume hawezi kukosa nguvu kwa kulala katika neti yenye dawa kama huna nguvu huna tu,”amesisitiza.

Naitwapwaki, amewataka wananchi wa wilaya hiyo kulinda familia zao kwa kuwa hakuna kiongozi wa nchi anataka kuona anapoteza nguvu kazi yake hivyo, Rais Dk. Samia anajua thamani ya Watanzania.

Amesitiza kuwa, iwapo atabaini yupo mwananchi anahujumu vyandarua hivyo kwa kufugia kuku atalipa faini kwa kutozwa vyandarua vingine 10.

Kwa upande wa wananchi wa Nzega akiwemo Richard Sendela mkazi wa Utemi Nzega Mjini, amesema vyandarua hivyo ni muhimu hivyo, wanaishukuru serikali kwa kuwafikia wale wenye hali ya chini ambao hawakuwa na uwezo wa kununua vyandarua vya famili nzima kwa kaya.

“ Mimi natumia vyandarua hivi na nimeoa tangu mwaka 1970 nina mke mmoja tumezaa watoto tisa na nina wajukuu 30 na nguvu bado ninazo hayo ni maneno ya uongo vijana wetu wale vizuri,”amesema.

Kaimu Meneja wa MSD Tabora Adonizedeck Tefurukwa, aliwahakikishia wananchi wa Nzega kiwa wote walio katika mpango wa kupewa vyandarua hivyo baada ya kujiandikisha katika kaya zao watapata kwani vipo vya kutosha.

By Jamhuri