Dekula Kahanga

Na Moshy Kiyungi

Dekula Kahanga ni mwanamuziki aliyetokea nchini na kujikita katika jiji la Stockholm nchini Sweden. Ameweza kutafuta mafanikio hadi kuunda bendi yake anayojulikana kama Dekula band.

Kabla ya kwenda nchini humo, Kahanga alikuwa mpigaji wa gitaa la solo katika bendi ya Maquis Original, iliyokuwa ikipiga muziki wake katika ukumbi wa Lang’ata,  Kinondoni jijini Dar es Salaam katika kipindi cha miaka ya 1980 na 90.

Dekula ambaye ni maarufu kwa jina la ‘Vumbi’,  aliwahi kutamka kwamba mafanikio yoyote katika maisha ni lazima mtu kuwa na malengo, na dhamira ya dhati, hatimaye kufanya uamuzi mgumu.

Akasema baadhi ya uamuzi mgumu alioufanya ni kuondoka katika bendi ya Maquis Original, na `kutokomea’ kwenda Sweden bila kujua atakuwa mgeni wa nani huko ughaibuni.

Vumbi anaeleza kwamba hivi sasa hajutii uamuzi huo kwa kuwa amepata mafanikio, ikiwa ni pamoja na kumiliki bendi yake.

Amesema bendi hiyo hupiga muziki kwa mkataba mara mbili kwa mwezi katika ukumbi wa Lala Vin jijini Stockholm, Sweden.

Dekula Band ina wanamuziki mahiri kutoka nchi mbalimbali duniani, wakiwemo Luhembwe Mwanahita ‘Bobo Sukari’ ambaye ni mwimbaji na kunengua, Sammy  Kasule anayeimba, kupiga gita la besi, drums na kinanda.

Wengine ni Joe Gerald Nnaddibanga anayeimba, kupiga konga na kucheza Christina Frank na Marceline Kouakoua.

Vumbi mwenyewe `analicharaza’ gitaa la solo na rhythm pamoja na Arne Winald ambaye ni mbonyezaji wa kinanda.

Safu hiyo kwa pamoja huufanya muziki wao kukubalika kimataifa hadi kupata mialiko lukuki ndani na nje ya Sweden hususani barani Asia, nchini Marekani, Japan,  Falme za kiarabu na Afrika.

“Hakuna kitu muhimu kama kuwa na mahusiano  mema na baadhi ya watu kutoka nchi mbalimbali ninazotembelea. Nimefikia kuweza kuongea  kwa ufasaha lugha tano tofauti za Kiswahili, Kiingereza,  Kifaransa, Lingala na Kiswidish,” amesema.

Alizaliwa Aprili, 2, 1962 katika kijiji cha Lumera, wilaya ya Kivu  Kusini huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Dekula ni mtoto wa kwanza kati ya watoto kadhaa wa Aloyce Obeid Dekula,  aliyekuwa mfanyakazi katika Serikali ya iliyokuwa Zaire (DRC) ikiongozwa na Mobutu Sseseseko.

Alipata  elimu ya sekondari katika shule mbili tofauti za Bukavu na Uvira huko DRC. Alihitimu kidato cha nne  mwaka 1979. Mwaka 1980, safari yake katika muziki ilianza kwa kujiunga na bendi za Bavy National na Grand Mike Jazz, ambako alikutana na wanamuziki akina Kyanga Songa na Issa Nundu.

Akiwa huko kwao wilaya ya Kivu, ‘Vumbi’ alikuwa msikilizaji mzuri wa Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD), akipenda kusikiliza nyimbo za bendi kama Morogoro Jazz, Jamhuri Jazz, Tabora Jazz, Nyamnyembe Jazz,  NUTA Jazz,  Mlimani Park, Maquis du Zaire na Orchestra Safari Sound.

Kamwe hatomsahau  John Luanda katika historia ya maisha yake, kwa kuwa huyo ndiye aliyekuwa chanzo cha yeye kuingia hapa Tanzania.

Luanda alikuwa akimiliki Chamwino Jazz,  aliwachukua kutoka DRC akiwa na wenzake  akina Bwami Fanfan, Sisco Lunanga na Baposta kwa madhumuni ya kujiunga katika bendi yake ya Chamwino.

Mwaka 1980, Vumbi alikutana na mwanamuziki  Chimbwiza Nguza Mbangu ‘Viking’ katika ofisi za ubalozi wa Kongo hapa nchini.

Nguza wakati huo alikuwa mpiga gita la solo pia alikuwa ni mmoja kati ya  wanahisa wa Orchestra   Maquis Comapy  (OMACO) na  mmoja kati ya viongozi wa bendi ya Orchestra Maquis du Zaire.

Katika maongezi yao, Chimbwiza  Nguza alimpa mwaliko yeye na wenzake kwenda kuburudisha kwenye ukumbi wa White House, uliokuwa maeneo ya Ubungo jijini Dar es Salaam.

Walipopanda jukwaani waliweza kuzikonga nyoyo za wapenzi wa muziki waliokuwa wamefurika ukumbini humo pamoja na wanamuziki wa bendi hiyo ya Maquis du Zaire.

Dekula Kahanga baadaye aliitwa na uongozi wa bendi ya Maquis du Zaire akina Chibangu Katai ‘Mzee Paul’, Mutombo Lufungula ‘Audax’ na Mbuya Makonga ‘Adios’ wakimtaka aandike barua ya kuomba kujiunga na bendi yao kwa mkataba usio na mshahara.

Alitakiwa na bendi hiyo ili kuziba nafasi ya Nguza ambaye alikuwa tayari ameanza mgomo baridi. Vumbi alikubali na akajiunga na Maquis du Zaire.

Vumbi anaikumbuka siku mmoja wakipiga muziki katika ukumbi wa  Temeke Stereo,  alimuona Nguza  akiwa amejibanza pembeni mwa ukuta ukumbini humo huku akisikiliza midundo inavyounguruma..

Lakini  viongozi wake akiwemo Chibangu Katai ‘Mzee Paul’ na  Ilunga Lubaba, walimwamuru aendelee kushika ‘mpini’.

Aliachiwa   kulivurumisha gitaa hadi  mwisho wa onyesho hata mpiga solo Ilunga Lubaba hakutaka kuligusa siku hiyo. Baada ya hapo kwa adabu zote alikwenda kumsalimia na Nguza pale alipo naye hakusita kumpa hogera kwa kazi  nzuri.

 Baadhi ya nyimbo lizoweza kupiga gitaa ni katika nyimbo za Makumbele, Ngalula Seya Malokelee, Karubandika, Mage, Dora mtoto wa Dodoma, Clara, Mwana yoka ya Babote, Nimepigwa ngwala na nyingine nyingi pasipo kutofautisha kati yake na Nguza.

Baadae bendi hiyo ilisambaratika na kuzinduliwa upya ikiwa na majina ya Maquis Original. Bendi hiyo ilikuwa ikipiga muziki wake katika kumbi za Wapi Wapi’s Bar pale Chang’ombe, Temeka Kata ya 14 kabla ya kuweka makao yake makuu katika ukumbi wa Lang’ata Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Baada ya mazoezi makali katika bendi hiyo, Oktoba 10, 1989 walirekodi nyimbo za Mashoga, Tipwatipwa, Hali Ngumu, Ossa, Marusu, Mangolibo, Kisebengo na zingine nyingi zote hizo akilicharaza gitaa la solo.

Wakati huohuo Maquis Original aliwapata wanamuziki wengine watatu toka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakiwamo waimbaji Bobo Sukari, Fred Butamu na mcharazaji gitaa la solo Kivugutu Moto na Chacho.

2431 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!