Na Michael Sarungi
Ukarabati unaofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam, umewezesha ongezeko la kuhudumia
shehena za mizigo kutoka tani milioni 10 kufikia tani milioni 16 kwa mwaka.
Kiwango hicho kinatarajiwa kuongezeka kufikia tani milioni 25 mwaka 2030, ikichochewa na
kasi ya ukuaji wa biashara ya bandari inayolazimu kuwapo mageuzi yanayogusia ukarabati huo.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko,
amesema hayo wiki iliyopita wakati akitoa taarifa ya maendeleo ya mradi wa uboreshaji wa gati
namba 1 hadi 7 kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa.
Mhandisi Kakoko amesema, TPA iliingia mkataba na kampuni ya M/s China Harbor Engineering
Construction Co. Ltd (CHEC) ya China, ili kuiboresha bandari hiyo kuifanya kuwa miongoni
mwa zilizo kubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Mkataba wa mradi huo utakaohusisha ujenzi wa gati mpya ya kupakulia magari, ulisainiwa Juni
10, 2017, ukigharimu Sh bilioni 336,641 na kwamba utakamilika ifikapo Juni 20, 2020.
Mhandisi Kakoko amesema gati mpya itakuwa na urefu wa mita 330 na kina cha mita 12.9
wakati yadi ya maegesho itakuwa na mita za mraba 69,000.
Amesema uboreshaji huo umegawanyika katika maeneo mawili makuu ya kuongeza kina hadi
kufikia mita 14.5 katika eneo la kupakulia na kupakia mizigo na uboreshaji gati namna 1 hadi 7.
Mhandisi Kakoko amesema mkandarasi anaendelea kutengeneza nguzo ambazo ni muhimu
kwa ujenzi unaofanyikia ndani ya maji. Nguzo hizo zinaingizwa kutoka China na zinatarajiwa
kukaguliwa na Mhandisi Mshauri Machi mwaka huu.
Naye Profesa Mbarawa amesema pamoja na uboreshaji huo, Serikali inaendelea na ujenzi wa
miundombinu wezeshi ya reli na barabara, ili kuhakikisha mizigo haikai muda mrefu bandarini
hapo.
Amesema ujenzi wa reli ya kisasa kwa kiwango cha standard gauge kutoka Dar es Salaam
kwenda mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kigoma, na ufufuaji wa reli ya Tazara kutaongeza ufanisi
kwenye bandari hiyo.
Kwa mujibu wa Profesa Mbarawa, mradi huo utakapokamilika, bandari hiyo itakuwa na uwezo
wa kupokea meli kubwa kutoka nchi kama China, Uingereza, Japan, Marekani na nchi
nyinginezo duniani.
Amesema lengo ni kuona mpaka mradi huo unakamilika, bandari hiyo itakuwa na gati nane
zenye vina vya maji vitakavyomudu kubeba meli kubwa.
Amesema matarajio yaliyopo ni kuongeza gati kufikia 15 na kuifanya bandari hiyo kumudu
ushindani barani Afrika.
Profesa Mbarawa amewataka wakandarasi wanaojenga mradi huo, kuhakikisha unakamilika
kwa wakati ili Tanzania na nchi za Rwanda, Uganda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo (DRC), Zambia, Malawi na Zimbabwe zianze kunufaika mapema.
Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya China Harbor Engineering, Frank Underwood,
amesema wanafanya kazi ‘usiku na mchana’ kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.
Amesema nia ya kampuni yake ni kuiboresha Bandari ya Dar es Salaam kuwa ya mfano kama
zilivyo nyingine maarufu duniani.

2226 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!