Ndugu Rais, lengo la maandiko yetu siku zote siyo kukosoa. Udhaifu wa kuandika kwa sababu
unampenda mtu au unamchukia mtu, Mwenyezi Mungu katuepusha nao.
Hatuandiki kwa ushabiki wa kumshabikia mtu au chama fulani. Wala hatuandiki hapa kwa lengo
la kusifia au kupongeza.
Tunaandika kile ambacho tunaamini kuwa ni ukweli mtupu, kwa lengo la kushauri tu. Tunaamini
kuwa kwa hizi busara zetu ndogo tulizojaaliwa na Muumba wetu, hatukujaaliwa kwa ajili yetu
bali kwa ajili ya waja wake. Itikadi yetu ni nchi yangu kwanza mengine yanaweza kufuata.
Yanayofanyika katika nchi yetu sasa kwa jina la siasa siyo siasa, bali ni unyama wa kishamba
uliokithiri katika fikra za baadhi ya wale waliopaswa kutuongoza.
Tunatengeneza nchi ya visasi kwa kuwasikiliza walionyimwa busara! Kiongozi mwenye busara
hukesha akijikumbusha kuwa uongozi wake una ukomo, hivyo siku moja utakoma.
Atakuwa siyo kiongozi tena. Wengine watakuwa ndiyo viongozi. Wanaopanga miaka saba sasa
na wanaopanga kuondoa ukomo wa uongozi ni wale waliokosa busara ya kujua kuwa, hakuna
makali yasiyokuwa na ncha.
Sifa ya kiongozi bora na raha ya kuwa kiongozi wa watu ni kupendwa na unaowaongoza.
Kulazimisha ni kuipumbaza nafsi yako mwenyewe! Kiongozi chukizo kwa watu wa Mungu ni
kiongozi chukizo kwa Mungu mwenyewe!
Ndugu Rais, haya mambo mengi makubwa yanayotendeka sasa huburudisha mwili tu, bali uovu
tunaoutenda siku zote huuchoma moyo wa mwanadamu, kama mkuki wa moto uchomavyo.
Na kwa sababu hiyo, uovu wa kiasi chochote ukipimwa katika mizani ni mzito zaidi kuliko mema
yote. Uovu mmoja unaweza ukafuta mazuri mia hata zaidi. Lakini ni vigumu sana kuona mema
yakifuta maovu.
Kama mema yangekuwa na uwezo wa kufuta uovu, basi mazishi ghali na ya kifahari
aliyofanyiwa marehemu Akwilina Akwilini yangezima uchungu uliomo katika vifua vya
Watanzania nchi nzima.
Lakini badala yake, yaliongeza huzuni, simanzi na majonzi kwa watu wa nchi hii. Hii ni ishara
itakayodumu kama chapa katika maisha yetu. Mwenye haki ya kuhukumu ni Mwenyezi Mungu
peke yake, naye ameiishaiandika hukumu yake.
Walioutekeleza unyama huo wanatembea na hukumu hiyo juu ya vichwa vyao, mpaka siku yao
ya mwisho!
Ndugu Rais, ukomo wa uongozi unapofika unyama wote uliotendwa katika nchi huchanua na
kujielekeza kwa Kiongozi Mkuu, kwa kuwa yeye ndiye mlipaji mkuu wa yote, yaliyotendwa na
wateule wake!
Ole wetu sisi, ole wetu sisi kama tuyafanyayo leo yanatutengenezea visasi vyetu kesho.
Kwelikweli nawaambieni, hiyo siku pekee, yatakuwa magumu kwetu! Oh, magumu kwetu! Oh,
itakuwa sawa na shubiri! Bali wanaheri wanaolia sasa kwa kuwa furaha yao kesho itafanana na
ile ya kuiona pepo ya Mwenyezi Mungu!
Ndugu Rais, ukatili wanaotendewa wananchi na wanaoitwa wasiojulikana hujawahi
kushuhudiwa katika nchi hii tangu uhuru!
Laana zinazotolewa na wananchi tena wengine kutoka mbali huko vijijini yanaonesha wananchi
wengi wameikatia tamaa nchi yao!
Haya ni lazima wanaotukuambie baba yetu! Umetuhimiza tuwe wakweli na tuiseme kweli huku
tukimtanguliza Mungu mbele.
Hata hapa tuandikapo tunamtanguliza Mungu ili akujalie utambuzi kwamba tukuambiayo ni kwa

mapenzi ya nchi yetu, watu wake na wewe mwenyewe baba, lakini hasa kwa mapenzi ya
Mungu wetu!
Nchi imefikia mahali damu ya Mtanzania kumwagika haitishi tena! Mwenye uwezo wa
kuirudisha nchi katika amani tulioikuta ni wewe pekee.
Mwenyezi Mungu akutangulie! Ndugu Rais, waraka wa maaskofu naamini umekubaliwa na
waumini wengi na hata wasio waumini wa Ukatoliki waliomo ndani ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM).
Hivyo hivyo, kwa tamko la Marekani (US) na tamko la Jumuiya ya Ulaya (EU) wako wanawema
katika nchi hii ambao wanaafiki ukweli.
Wakati utakapowadia mwanamwema aliniambia utabiri wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Nyerere, kuwa upinzani wa kweli utatoka ndani ya CCM yenyewe, utatimia. Hili halihitaji utabiri!
Nchi inahitaji upinzani bila kujali hao wapinzani watakuwa ni nani. Kuona upinzani ni uadui ni
kukosa busara. Wanaong’ang’ania madaraka wapambane kwa hoja.
Wanawema nawaambia kila mara kuwa hao wote hakuna anayempigania masikini. Wote ni
waheshimiwa wanatafuta utukufu zaidi kwa kushika mamlaka ya nchi!
Ndugu Rais, unafanya mambo mengi mema na makubwa kwa ajili ya nchi yetu na kwa ajili ya
watu wetu, lakini kwa haya yanayotendeka nchini wananchi wanakuwa kama hawayaoni.
Kazi iliyotukuka inayofanywa na wanamwema. Waziri Mkuu wetu anafifishwa na matukio ya
kinyama.
Bila matukio haya maovu mwanamwema William Lukuvi kwa kazi njema anayoifanya sasa,
angeng’ara kama baba ulivyong’ara wakati wa Rais Benjamin Mkapa kwa barabara zako.
Hata Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete, alipokupa wizara aliyonayo Lukuvi sasa, bado ulikuwa na
utendaji wa hali ya juu.
Ninakushukuru binafsi kwa sababu bila wewe hujaja, sisi tuliokuwa huku mashambani
ingetuchukua muda mrefu kupata hati. Baba asante, leo mimi nina hati ya banda langu.
Lukuvi angeng’ara kama alivyong’ara mwanamwema Augustino Mrema, wakati wa utawala wa
Rais (mstaafu) Ali Hassan Mwinyi.
Lakini matukio ya kinyama yanamfifisha. Tutaendelea hivi mpaka lini? Tufike mahali baba
tutafakari!
Kama ni wapinzani tumewajengea huruma kubwa kutoka kwa wananchi. Wananchi waonapo
viongozi wao wakiwaongoza kwa upendo hupata hamasa ya wao nao kuchapa kazi zaidi kwa
ajili ya maendeleo yao na nchi yao.
Kama kujibu wananchi nao huwaheshimu viongozi wao na kuwapenda kutoka katika vifua vyao.
Hiyo husababisha hata wananchi kwa wananchi kupendana. Ni kwa namna hii tu nchi hupata
ustawi na watu wake.
Ni vigumu sana nchi kupata maendeleo ikiwa wako katika magomvi ya wao kwa wao na
misuguano isiyokwisha.
Ndugu Rais, tukubali kuwa ni kosa kubwa kwa baadhi ya viongozi wetu kukiri mbele ya
wananchi kuwa, kuna wahalifu walioishinda Serikali kwa sababu imeshindwa kuwajua.
Ukishakiri kuwa kazi imekushinda muungwana huachia ngazi. Kung’ang’ania unawasukuma
wananchi wakuhesabu kuwa wewe ni sehemu yao.
Baba turudishie amani kwanza mengine yote yatafuata!

4638 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!