Na Pendo Nguka, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania Deodatus Balile amewaasa waandishi wa habari nchini kuongeza nguvu katika kuandika na kuripoti habari zinazohusu matumizi ya nishati ya jua hasa katika sekta ya kilimo na uhifadhi wa mazao.
Amesema vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee ya kuibua mijadala na kuelimisha jamii kuhusu namna teknolojia hii nafuu na rafiki wa mazingira inavyoweza kubadilisha maisha ya Watanzania wengi hususa wale wa vijijini.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa ripoti maalumu inayoangazia namna vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti kuhusu matumizi ya nishati jua katika kilimo Balile ameeleza kuwa nishati ya jua imekuwa suluhisho kwa wakulima.
“Waandishi wa habari wanatakiwa kuandika habari zenye mtazamo wa ajenda za kijamii na tusisubiri kuandika habari za matukio tu bali tunatakiwa tuonyeshe jinsi nishati ya jua inavyotumika kupunguza gharama, kuongeza tija kwa wakulima na kusaidia wananchi kuendesha shughuli zao kwa ufanisi mkubwa,” Amesema Balile
Aidha ameongeza kuwa nishati ya jua inaweza kubadilisha mfumo wa kilimo nchini, kwani wakulima wengi wamekuwa wakitegemea mvua za msimu. Kwa kutumia teknolojia za kupampu maji zinazoendeshwa na jua, wakulima wanaweza kulima kwa mwaka mzima.
Hii ni hatua kubwa ya kupunguza utegemezi wa mvua na kuongeza uzalishaji wa chakula.
“Kwa mfano kuna wakulima wa ndizi ambao wamefanikiwa kukaushia ndizi zao kwa kutumia umeme wa jua na kuziuza sokoni,” amesema Balile
Kwa upande wake Dk. Daris Mukiza mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesisitiza kuwa nishati ya jua ni nyenzo ya maendeleo endelevu kwa kuwa ni salama kwa mazingira na haina gharama kubwa za uendeshaji na inaweza kutumika katika shughuli nyingi za kiuchumi.
“Tunapaswa kuondoa dhana potofu kuwa kilimo ni cha msimu na kwa kupitia nishati ya jua, wakulima wanaweza kuwa na uzalishaji endelevu, kulima wakati wowote na kuongeza kipato cha familia zao,” amesema Dk. Mukiza.
Ripoti iliyozinduliwa imebainisha kuwa vyombo vya habari nchini bado havijatoa kipaumbele cha kutosha katika kuandika makala na kuripoti kwa kina kuhusu matumizi ya nishati ya jua. Hali hiyo imesababisha wananchi wengi, hasa wakulima wadogo, kutokuwa na taarifa za kutosha kuhusu namna wanavyoweza kunufaika na teknolojia hii.

Aidha, ripoti hiyo imeonyesha kuwa baadhi ya wakulima wamekuwa wakiona nishati ya jua kama gharama kubwa ya kuanza, bila kujua kwamba faida zake za muda mrefu ni kubwa zaidi kuliko gharama wanazotumia sasa kwa kulipia umeme au kutegemea mvua.
Iwapo waandishi wa habari wataandika simulizi za mafanikio ya wakulima waliokwisha tumia teknolojia hiyo ya nishati jua katika kilimo basi itakuwa rahisi kwa jamii kuona uhalisia wake na kuhamasika zaidi.
Kupitia makala hizi zinazoonyesha ni kwa namna gani nishati ya jua inaweza kutumika katika kilimo wananchi wataelewa kuwa nishati ya jua si chanzo cha mwanga pekee, bali ni injini ya maendeleo ambayo inaweza kuongeza thamani ya mazao, kukuza kipato cha kaya na kuchangia kwa kiwango kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa taifa.