DC ILALAKesho ni Jumatano Desemba 9. Tarehe kama hii mwaka 1961 nchi ya Tanganyika ilipata Uhuru wa bendera baada ya kutawaliwa kwa mabavu kwa kipindi cha miaka ipatayo 77 na wakoloni wa Kijerumani na wa Kiingereza.

Kwanza ni Wajerumani waliotawala kwa miaka ipatayo 34 (1885-1919) na kufuatiwa na Waingereza kwa miaka 43 (1919-1961). Katika kipindi chote hicho maendeleo ya kijamii yalikuwa  duni na uchumi wa nchi ulikuwa kwa faida ya wakoloni. Nchi zao zilifaidika sana na rasilimali zetu.

Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, na wananchi wa Tanganyika walidai wapewe Uhuru na kurudishiwa utu na heshima yao. Kazi ilifanyika na Uhuru kupatikana. Waingereza na jamaa zao walifunga virago na kurudi kwao Ulaya.

Baadhi yetu tulikuwapo pale Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, tukishuhudia bendera ya Mwingereza ikiteremshwa na bendera ya mbantu – mtu mweusi – ikipandishwa kwa mbwembwe, furaha na amani. Hakika ulikuwa usiku wa furaha saa 6 pale vigelegele, nderemo ziliposikika na kufuatiwa na milio ya fataki. Nchi yote ilizizima kwa shangwe na furaha. Hii ni siku adhimu sana kwa Watanzania.

Nasema ni siku adhimu kwa sababu matokeo ya Uhuru wa Tanganyika na Mapinduzi ya Zanzibar Januari 12, 1964  ni baadhi ya sababu zilizonasibisha nchi mbili hizo kuunda Muungano wa Jamhuri ya Tanzania, chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanganyika na Sheikh Abeid Amani Karume wa Zanzibar.

Kila mwaka Watanzania tunasherehekea sherehe za Uhuru. Mwaka huu ipo tofauti na sherehe tulizozizoea za kutumia muda, nguvu, upendo na fedha katika kucheza michezo, ngoma na kuandaa tafrija za kunywa vinywaji na vileo pamoja na kula vyakula aina aina hadi kusaza na kutupa majaani.

Mwaka huu sherehe kama hizo hazipo. Mkuu wa nchi, Rais John Pombe Magufuli, amezuia utaratibu huo na badala yake kuwaagiza wananchi watumie nguvu na muda wao kufanya usafi katika maeneo ya makazi yao. Fedha iliyotengwa kwa shughuli za sherehe zitumike kugharamia vitendea kazi vitakavyotumika katika kazi hiyo.

Agizo limepokewa kwa mikono miwili na wananchi na viongozi wa Serikali kuanzia ngazi ya kitongoji, kijiji, mtaa, mji na jiji. Wote wamo katika hekaheka za kufanikisha jambo hilo. Binafsi natanguliza pongezi za awali katika kutekeleza agizo hilo.

Hili ni agizo linalodhihirisha maana mojawapo ya Serikali ya Awamu ya Tano inayotaka kuleta mabadiliko ya kweli katika kujenga, kuboresha na kustawisha maisha na afya njema ya kila Mtanzania, ili awe na uwezo wa kufanya kazi zake na za Taifa kwa furaha na fanaka.

Naamini Watanzania wameona, wamesikia na wamekuwa wahanga wa magonjwa yanayotokana na uchafu katika maeneo tunamoishi. Magonjwa hayo kama vile ya kuumwa na macho, kuharisha, kupata homa ya matumbo, malaria, kipindupindu n.k. Leo malaria na kipindupindu yanatusumbua mno.

Rais Magufuli ametuzindua  Watanzania tuachane  na kipindupindu. Badala ya kusherehekea siku ya Uhuru  kwa shangwe, vigelegele, nyimbo na michezo bila kusahau vileo na mapochopocho, tuelekeze fikra, nguvu na shangwe katika kuhamasishana na kufanya usafi kuanzia nyumbani, barabarani hadi sokoni.

Tuzibue mifereji na mitaro yenye maji machafu yasituame tena. Tuchome moto takataka na majani. Tufukie madimbwi yenye maji machafu na kutia dawa katika malindi ya vyoo. Tufyeke vichaka na nyasi na kunyunyuzia dawa za kuua wadudu na viluwiluwi vinavyosababisha magonjwa yanayotokana na uchafu.

Utamaduni huu mpya wa kufanya usafi wa maeneo badala ya kufanya sherehe una dalili za wazi za kumjengea Mtanzania mabadiliko katika afya ya mwili wake na mila ya kupenda kufanya kazi na kuondoa gharama ya matumizi ya fedha pasipo na sababu za kimaendeleo.

Huu uwe ni mwanzo wa kampeni za kudumu za usafi wa maeneo na mazingira. Utamaduni wa usafi wa mwili na roho. Fedha itumike kwa manufaa ya wananchi wala si kwa manufaa ya wachache. Tubuni pia siku nyingine ambazo si za sherehe kama hizi tuwe tunafanya usafi. Kiongozi wetu amekwisha tuonesha kwa kauli na kitendo utamaduni huu unawezekana. Tuendelee nao. Inawezekana.

2961 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!