Mwanangu John, sasa  ni mwezi mmoja tangu tulipoachana na ukawa mtu wa Serikali, ule uwezo niliokuwa nao wa kuongea na wewe jioni kibarazani haupo tena, nikitaka kukuona ni lazima nipite mageti saba ya walinzi ambao watajiridhisha na sababu zangu za kukuona.

Haya ni matatizo ambayo sikujua; laiti ningejua basi ningekushauri usigombee huo userikali.

John, wakati unachukua fomu ya kugombea userikali kuna wengine walikuwa tayari wamezindua kampeni kwa mbwembwe za ajabu, wakinadi kuyashughulikia matatizo ya Watanzania ambayo yamelifikisha Taifa hili hapa baada ya miaka hamsini ya uhuru, wakinadi kuuchukia umaskini na kuleta mabadiliko, sasa naona unataka kupishana na sera zao, na lazima upishane kwa kuwa na wewe ulikuwa na mtazamo wako katika uongozi.

John, kumbuka kuwa kila mtu ana maono yake, wapo watakaoona kuwa unakosea, inawezekana hata mimi nikawa naona hivyo hivyo lakini wewe simamia maono yako ili mwishowe uweze kujibu maswali utakayoulizwa na waliokupa kura zao.

Ndiyo, utaulizwa juu ya kukidhi matakwa yao, utaulizwa juu ya ahadi ulizotoa, utaulizwa juu ya maendeleo ya Taifa lao na maswali mengi kutoka pande mbalimbali nchini.

 John, huku mitaani na vijijini kuna kesi kubwa ya kusutana, kuna kesi ya kudai kura zao, watu wanagombana kwanini kura ya urais hawakukupatia japo tayari wewe ni rais wa nchi hii,  sielewi kwanini wanasutana lakini jibu utakuwa nalo kwanini wagombane leo baada ya kukaa Ikulu kama Rais kwa muda wa mwezi mmoja na siku kadhaa.

John, wakati ukizunguka nchini kuomba kura za wananchi ili wakupe ridhaa ya kuwaongoza, ulisema mambo mengi mno ambayo ni kero za muda mrefu kwa wananchi, wapo wengi wagombea wenzio ambao nao walinadi sera zao, si vibaya nikasema labda wapiga kura walikuelewa wewe vizuri kuliko wengine, na ndiyo maana ukapata ushindi ambao siwezi kusema ni wa kishindo, uchaguzi ulikuwa ni mgumu na kama huamini angalia mikanda ya video ya wagombea wenzako ambako kuna watu walikuwa wakizimia na kwako wapo ambao walidiriki kukuzomea.

John, siku chache baada ya kuingia Ikulu watu walianza kukuelewa ulikuwa unamaanisha nini, walikuelewa vizuri sana siku ya kulizindua Bunge, wakakuelewa zaidi ulipoanza na suala la ukwepaji kodi, wakazidi kukuelewa zaidi ulipokataa safari za nje na matumizi mabaya ya fedha katika sherehe na badala yake kuelekeza fedha hizo katika shughuli za kimaendeleo, walikuelewa zaidi baada ya uteuzi wa Waziri Mkuu ambaye naye halikuwa matarajio ya Watanzania lakini wanaona anachokifanya sasa ni kwa faida ya Watanzania, wapo wanaosema unaweza kuwa na unafuu wewe lakini PM akawa kizingiti.

John, kama uchaguzi ukifanyika leo, nakuhakikishia utashinda kwa asilimia zote isipokuwa za mafisadi, wezi na wavivu.

John wapo wanaosema ni nguvu ya soda lakini kuna imani kubwa na wewe kutokana na kumtanguliza Mungu na kuanza kupambana na vigogo ambao walikuwa hawaguswi na mkono wa Serikali.

Sina hakika lakini yapo mengi yanayosemwa juu ya utawala wako, wapo hata wanaodiriki kukuomba usifanye uteuzi wa mawaziri kwa kuwa wanaona wewe na PM mnatosha mkisaidiana na makatibu wakuu, wapo wanaosema unaweza kuchagua mawaziri wale wa michakato, kufanyia kazi, upembuzi yakinifu na tutajadiliana katika meza.

Watanzania hawa John umewakosha na wengi wanakuombea maisha marefu ili uweze kutatua kero zao, wanasubiri kwa hamu kuona haki na uhuru wao unapatikana, wanasubiri kuona fedha zao zilizoliwa na wajanja wachache zinarejeshwa, wanataka kuona kila mtu analipa kodi, wanataka kuona heshima ya nchi duniani inarudi, wanataka kuona mizahamizaha na maisha ya watu inapotea.

John, umetupa jiwe msituni na unaposikia kilio cha mtu mzima jua kuwa jiwe limefika utosini kwake, watu waligeuza nchi hii kuwa mali yao binafsi, waligeuza mapato ya Taifa kuwa yao binafsi, tuliowaamini kumbe walikuwa wanatuchinja tukiwa hai, leo uongozi wako wa mwezi na ushei tunashuhudia utendaji kazi makini na wa dhati kabisa kiuzalendo.

John, nakushauri, fanya kazi ili nasi tufanye kazi, ulipoanzia isiwe mwisho na watu wakapata sababu ya nguvu ya soda, usiogope kitu japokuwa kuna watu wenye nguvu kuliko katapila, muombe Mungu nasi tunakuombea na kukulinda ili utusaidie kutuondoa katika mateso tuliyokuwa nayo.

John, sikuombei kura, lakini nakuombea ulinzi kwa Mungu.

 

Wasaalamu

Mzee Zuzu

Kipatimo.

1296 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!